Habari za Punde

Kilimo yaizuia mikungu ya ndizi iliyopenyezwa Zanzibar

Madina Issa na Khamisuu Abdallah
JUMLA ya mikungu ya ndizi 200 yenye thamani ya shilingi milioni 3.3 aina ya mtwike kutoka Tanzania bara zimekamatwa na Idara ya Kilimo Maliasili Zanzibar kufuatia kuwepo marufuku ya kuingizwa bidhaa hizo Zanzibar.

Mkuu wa kitengo cha utibabu wa mimea na ukaguzi wa mazao, Zainab Salim Abdalla alisema serikali iliweka marufuku kuingiza ndizi kutoka Tanzania bara kutokana na kuwepo maradhi ya ‘banana bantichop’ pamoja na ‘bektiria root’.

Akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Mwanakwerekwe, mkuu huyo alisema marufuku hiyo ya kuletwa ndizi imewekwa kwa lengo la kuzuia migomba ya Zanzibar kushambuliwa na maradhi hayo.

Alisema ndizi hizo zilikamatwa juzi katika soko kuu la Mwanakwerekwe na hivyo hazifai na ni vyema zikaangamizwa ili kuepusha kujitokeza kwa maradhi ya migomba.

Alisema kuwa wafanyabiashara wengi wamekuwa wakikiuka sheria zinazowekwa jambo ambalo limefanya kuuzwa kwa bidhaa ambazo zinahatarisha afya ya walaji.

Kufuatia hali hiyo aliwasihi wafanyabiashara hao wakati wa kuleta bidhaa zao kuhakikisha wanapata vibali cha biashara, ili waweze kuepukana na usumbufu watakaoupata katika uuzaji wa bidhaa zao.

Zainab alisema wafanyabiashara mbalimbali wametakiwa kufuata sheria za kuuza mazao ili kuepukana na biashara zao kuangamizwa na badala yake kupata hasara.

Alifahamisha kuwa karantini ya kupiga marufuku uingizwaji wa mazao ya aina hiyo wameitoa tangu mwezi wa Ramadhani mwaka jana kupitia vyombo mbali mbali vya habari na kuwataka wafanyabiashara wengine kutonunua bidhaa za ndizi kutoka Tanzania bara.

Nae mkuu wa kilimo soko la Mwanakwerekwe, Omar Rajab Omar alisema mfanyabiashara huyo alimkamata akiwa anaingiza bidhaa hizo usiku katika soko hilo kwa madhumuni ya kuziuza huku mmiliki huyo akiwa hana kibali cha kuletea mazao hayo.

Aliwataka wafanyabiashara kufuata agizo la serikali na waache ubishi na kuingiza bidhaa zilizokuwa haziruhusiwi ndani ya nchi kwani itawapeleka kupata hasara.

Aliongeza kuwa hapo awali walikuwa hawafahamu kama ndizi hizo zinatoka Tanzania bara kwani zilishushwa katika bandari ya Malindi Zanzibar zikitokea kisiwani Pemba, lakini mara baada ya kuzichunguza ndipo walipobaini kuwa zinatoka Tanzania bara.

Nae mmiliki wa bidhaa hizo Saleh Hamad Abdallah, alikiri kupakia bidhaa hizo na kusema kuwa hazitoki Tanzania bara pekee bali pia zipo ambazo zinatoka katika kisiwa cha Pemba.

Alisema kuwa alikuwa hafahamu kama bidhaa za aina hiyo haziingizwi nchini kutoka nje ya Zanzibar.





No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.