Habari za Punde

UTOAJI MAONI KATIBA MPYA , Urais wa Tanzania uwe kwa Zamu

Na Mwantanga Ame 

HUKU zoezi la utojia wa maoni kwa ajili ya katiba mpya ya Tanzania, wananchi wa wilaya ya Kusini Unguja wameibuka na mawazo tofauti wanayotaka yaingizwe katika katiba hiyo, ikiwemo wananchi kupewa uwezo wa kuawajibisha Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. 

 Wananchi hao walieleza hayo jana huko Kibuteni wilaya ya Kusini Unguja, walipojitokeza mbele ya kamati ndogo ya Tume ya kukusanya maoni ya katiba mpya. 

 Akitoa maoni yake, Rajab Haji Dawa alisema katiba mpya uwape uwezo wananchi kuwachukulia hatua Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pale watakaporidhika kuwa wameshindwa kutekeleza wajibu wao. 


 Alisema mfumo uliopo hivi sasa hautoi haki kwa wananchi ya kuwawajibisha viongozi wa aina hiyo wanaoonekana hawawajibiki na wenye kushindwa kutekeleza majukumu yao. “Wapo baadhi ya Wabunge na Wawakilishi wanaonekana kushindwa kutekeleza majukumu ya msingi waliyopewa na wananchi, lakini wananchi waliowachagua wanashindwa kuwawajibisha”, alisema mwananchi huyo. 

 Alisema mfumo uliopo haumuwezeshi mwananchi ambaye ndiye aliyemchagua Mbunge ama Mwakilishi kumuwajibisha hadi pale atakapomalizika muda wake wa miaka mitano au afariki dunia.

 Eneo jengine alilochangia mwananchi huyo ni nafasi ya Urais wa Tanzania kufanywa kwa awamu kati ya Zanzibar na Tanzania bara na isiwe unafanyika kwa kuangalia upande mmoja. Akizungumzia suala la Muungano, alisema unapaswa kuangaliwa upya kwa kupunguzwa mambo ya Muungano huku suala la mafuta na gesi asilia kila upande ushughulikie pekeyake. 

 Maoni mengine yaliyotolewa ni pamoja na suala la kodi ambapo ilipendekezwa kuwa kodi zinazokusanywa Zanzibar zisanywe na Mamlaka ya Zanzibar na matumizi yake yabakie Zanzibar. 

 Wakizungumzia mgawanyo wa madaraka katika nafasi za kibalozi, wananchi hao walisema nafasi hizo zitolewe kwa usawa baina ya Tanzania bara na Zanzibar, pamoja na mgawanyo sawa wa misaada kutoka nje. 

 Nae, Khamis Juma Ameir, (39), akitoa maoni yake alisema mabadiliko ya katiba yanapaswa kuliangalia suala la uteuzi wa nafasi ya Urais wa Zanzibar, ufanywe Zanzibar na sio Dodoma. 

 Alisema tatizo la Rais wa Zanzibar kuchaguliwa Dodoma limekuwa likiwafanywa wananchi wengine kutokubaliana na uchaguzi huo nma kuona kama vile wanalazimishwa wamkubali huyo huyo waliyeletewa. 

Akitoa maoni juu ya serikali alisema ni vyema serikali zikawa tatu ikiwepo ya Zanzibar, Tanganyika na serikali ya Muungano kuliko ilivyo hivi sasa hali inayosababisha kuwepo kwa kero. 

 Kwa upende wake Subira Ayoub Mwalimu, alisema mabadiliko hayo ya katiba yanahitaji kuona Wabunge na Wawakilishi kunakuwa na uwiano pamoja na nafasi za uteuzi katika taasisi mbali mbali za serikali. 

 Kuhusu Elimu ya Juu Mwananchi huyo alipendekeza kuona linaondolewa katika mambo ya Muungano ili suala hilo libakie kusimamiwa na Zanzibar. 

 Hali ya zoezi hilo tangu limeanza kufanyika limeonekana kwenda kwa amani huku wananchi wakipewa uhuru wa kutosha kutoa maoni yao . 

Upande mwengine zoezi hilo pia limeonekana kutawaliwa zaidi na maoni kwa njia ya barua ambapo kwa siku ya jana zaidi ya barua 40 ziliwasilishwa kutoka kwa wananchi wa Kibuteni na Michamvi. 

 Wananchi hao wataendelea tena kutoa maoni yao katika kijiji cha Kizimkazi Mkunguni na Kizimkazi Dimbani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.