Habari za Punde

Hamad Masoud awaomba radhi wapiga kura wake


Kwa kuamua kujiuzulu bila ya kuwashauri

Na Abdi Suleiman, Pemba

Aliyekuwa Waziri wa Miundo mbinu na Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambae pia ni mwakilishi wa jimbo la Ole, wilaya ya Wete Mkoa wa kaskazini Pemba, Hamad Massoud Hamad, amewaomba radhi wapiga kura wake, wa jimbo la Ole kwa uamuzi wake wa kujiuzulu bila ya kuwashauri.

Mwakilishi huyo, aliyasema hayo jana huko Maambani Ole, wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa jimbo la Ole, kwa mara ya kwanza baada ya kujiuzulu wadhifa huo.

Hamad Massoud alisema kuwa, uamuzi aliouchukuwa wa kuamua kujiuzulu kwake ni sahihi na wa kishujaa, na alifanya hivyo baada ya kuwashauri viongozi wake wakuu wa chama chake, na ndipo alipomuandikia barua Rais  wa Zanzibar.


“Nimefanya kitendo bila ya kuja kuwashauri sio kwa sababu ya ujeuri, sio najua sana mimi ni mwakilishi na uwaziri, katika kitu ninacho kiheshimu ni heshima nilioyopewa na watu wa ole ambao ndio nyinyi” Alieleza Mwakilishi Hamad Massoud.

“katika siasa za Zanzibar Ole ndiko kwenye chuo cha siasa, kwasababu ya umoja na ukarimu wa watu wa Ole, na ndio waliomuweka madarakani kwa kura 5564 sawa na asilimia 86 niliteuliwa kuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano”alifahamisha Hamad.

Alieleza kuwa baada ya kutafakari Julai 20 aliamua kumuandikia barua Rais ya kujiuzulu kwake, baada ya kushauriana na viongozi wenzake wa CUF,  na Rais kuliridhia ombi la kujiuzulu kwake.

Aidha aliwataka wananchi wasisikitike wala kuhuzunika kutokana na na uamuzi wake aliouchukuwa, na kuwaomba wamuunge mkono kufuatia uamuzi wake aliouchukua.

Kwa upande wao wananchi wa jimbo hilo la Ole, wamesema kuwa, kujiuzulu kwake ni moja ya kuonyesha ukokamavu wa kisiasa sambamba na kukijengea heshima chama chao cha wananchi CUF.

Wananchi hao walifahamisha kuwa, Mwakilishi wao, ni muda mfupi tokea kuchaguliwa kwake lakini mafanikio makubwa yamepatikana katika Wizara ya Miundo mbinu na Mawasiliano  hususan suala la ujenzi wa barabara na Uwanja wa Ndege wa Zanzibar.

“Kujiuzulu, kumeleta faraja kubwa kwake na kwa taifa nzima kwani ni kaonyesha ujasiri wa kukomaa kisiasa na kisaikolojia, sambamba na kukijengea sifa chama chetu cha Cuf” walifahamisha wananchi hao.

Walifahamisha kuwa kujiuzulu kwa Mwakilishi huyo, ni heshima kubwa kwa serikali yao ya umoja wa kitaifa, kwani tayari wako baadhi ya viongozi wanatuhumiwa kwa kuiba mamilioni ya shilingi, huku wakishindwa kujiuzulu.

Naye mwenyekiti wa CUF wilaya ya Wete, Khalfan Moh’d Issa, amesema kuwa, kujiuzulu kwa Hamad Massoud ndio utamaduni wa chama chao, kwa viongozi kusamehe maslahi yao binafsi kwa lengo la kuijengea hashima Serikali ya Zanzibar.

Mwenyekiti huyo, alisema kuwa Zanzibar imefika wakati kwa viongozi wake watakaobainika na kashafa ya aina yoyote kuweza kujiuuzulu, ili kuepuka kuitia aibu serekali yao.

Naye aliyekuwa Mwakilishi wa jimbo la Chambani Abassi Juma Muhunzi, aliwataka wananchi wa Ole kumuunga mkono mwakilishi wao, kwani kufanya hivyo ni kumekijengea heshima kubwa chama chao na kuonyesha ujasiri wa kisiasa.


Muhunzi alisema kuwa, kitendo alicho kifanya Hamad Massoud ni kitendo cha kishujaa, na kitu ambacho hakijawahi kutokea tokea mwaka 1964, hivyo kiwe mfano kwa viongozi wa Zanzibar, watanzania na Afrika mashariki na kati ambapo utamaduni huo haupo.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.