Habari za Punde

ZMA na SUMATRA zajipanga kutekeleza majukumu kwa mashirikiano


Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda akiwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi nje ya ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Mweni mara baada ya kutoa salamu za pole kufuatia msiba wa meli ya M.V.Skagit hivi karibuni. Nyuma yao ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohd Aboud Mohd.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Balozi Rosemery Migiro akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiwasilisha salamu za pole kufuatia msiba wa ajali ya meli ya M.V. Skagiti hivi karibuni

Na Othman Khamis Ame

Kazi kubwa inayozikabili Serikali zote mbili Nchini Tanzania kwa hivi sasa ni kuhakikisha zinaridhia ushirikiano wa Mamlaka za Usafiri wa Baharini Bara { Sumatra } na ile ya Zanzibar { ZMA } katika kutekeleza majukumu yao kwa pamoja. 

Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda alitoa ushauri huo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Baraza la Wawakilishi Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. 

Mh. Pinda ambaye amekuwa Zanzibar kutoa Mkono wa pole kufuatia ajali ya Meli ya M.V. Skagit iliyotokea hivi karibuni karibu na kisiwa cha Chumbe alisema ushirikiano huo ulenge zaidi katika suala la usimamizi na ukaguzi wa pamoja wa vyombo vya Baharini. 


Waziri Mkuu Mizengo Pinda alifahamisha kwamba Taasisi hizo mbili za usimamizi wa usafiri wa Baharini ndizo dhamana za kulinda maisha ya wasafiri wanaotumia bahari kati ya Tanzania Bara na Zanzibar. 

Alisisitiza kwamba si vyema kwa Serikali zote mbili zikaendelea kuona hitilafu zinazoepukika zinatokea wakati uwezo wa kuziondoa unawezekana. “ Wananchi wanaweza kutuona Viongozi tunapuuza na hatutaki kuchukuwa hatua zinazopelekea kuleta majanga na hatimae kusababisha maafa”. Alisisitiza Waziri Mkuu Mizengo Pinda. 

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alimueleza Waziri Mkuu kwamba Serikali tayari imeshatoa agizo kwa Uongozi wa Mamlaka za usafiri wa baharini ni lazima kufanya uhakiki wa vyombo vyote kwa mujibu wa uwezo wa chombo husika. “ Ni imani ya Serikali kwamba mamlaka za Usafiri wa Baharini Bara { Sumatra } na ile ya Zanzibar { ZMA } zitajizatiti kutekeleza majukumu yao”. Alifafanua Balozi Seif. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba katika kupata Meli ya uhakika ya usafirishaji wa uhakika wa Wananchi na Mizigo Serikali imeamua kudokoa fedha katika vifungu vya bajeti ya mwaka huu katika kila Taasisi yake kwa ajili ya ununuzi wa Meli hiyo. 

Alisema katika hatua hiyo makusanyo hayo yanatarajiwa kuanzia shilingi Bilioni 17 kwa hatua ya mwanzo makato yatakayokuwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. 

Hata hivyo Balozi Seif aliendelea kusisitiza kwamba Taasisi au Kampuni yoyote itakayofikia uamuzi wa kununua chombo chochote cha usafiri wa baharini lazima ipate kibali kutoka Serikalini. “ Serikali kamwe haitokuwa tayari kutoa kibali iwapo maombi ya Taasisi hizo kwenye manunuzi ya vyombo hivyo haitafikia kiwango kunachokubalika kitaalamu”. Alisisitiza Balozi Seif. 

Baadaye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipokea salamu za rambi rambi kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa Balozi Rosemary Migiro. 

Katika mazungumzo yao Balozi Bigiro alisema upo uwezekano wa kufungua majadiliano kati ya Taasisi za Umoja wa Mataifa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika jitihada za kutafuta nguvu za pamoja za kukabiliana na maafa wakati yanapotokezea. 

Balozi Migiro alisema baadhi ya Taasisi za Umoja huo zimejengewa uwezo na vifungu vya kusaidia kukabiliana na maafa katika nchi wanachama hasa kwenye mazingira ya kitaalamu zaidi. 

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alimpongeza Balozi Rosemary Migiro kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuiwakilisha vyema Tanzania katika Umoja wa Mataifa. “ Tanzania inajivunia kutoa Kiongozi ndani ya Mamlaka ya Umoja wa Mataifa tena cha kufurahisha zaidi ni Mwanamke”. Alieleza furaha yake Balozi Seif. 

Balozi Seif alimueleza Naibu Katibu Mkuu huyo mstaafu wa Umoja wa Mataifa kwamba Zanzibar Taasisi za Umoja huo hivi sasa ziko karibu zaidi kiutendaji na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

Alisema hatua hiyo imepelekea Zanzibar kuboresha mfumo wa kuwa na Taasisi za Kimataifa katika sehemu moja ambao umeanza kuleta faida na matumaini makubwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.