Kifo cha Daudi Mwangosi: Unyama huu hadi lini?
Sikika imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa
za kifo cha mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten mkoani Iringa, Daudi
Mwangosi.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari, marehemu
Mwangosi alikuwa kazini akitimiza wajibu wake wa kutafuta habari. Tumestushwa
zaidi baada ya kuona picha za mnato zikionyesha jinsi ambavyo mtu anayedaiwa
kuwa ni mwandishi huyo akishambuliwa na idadi kubwa ya askari polisi na baadae
kupoteza maisha.
Katika siku za karibuni, tumeshuhudia ongezeko
la matumizi ya nguvu kupita kiasi yanayofanywa na jeshi la polisi, ambayo siyo
tu yanasababisha uharibifu mkubwa wa mali za wananchi bali pia baadhi yao
kupoteza maisha. Mfano, mwezi uliopita, tuliarifiwa kuwa kijana aliyeuawa mkoani
Morogoro alikuwa akiuza magazeti na wala hakuhusika katika vurugu kwa namna
yoyote. Vivyo hivyo, marehemu Mwangosi alikuwa akitimiza wajibu wake wa uandishi
wa habari.
Uhai ni haki ya kikatiba ya kila Mtanzania.
Hivyo, ni jukumu la polisi kulinda maisha na uhai wa wananchi wote bila kujali
itikadi au kazi zao.
Hakuna sheria inayohalalisha kujeruhi, kutesa
wala kuua mwananchi yeyote kwa sababu tu ati amekataa kutii amri ya polisi.
Sikika inasikitishwa zaidi na utamaduni unaozoeleka ndani ya jeshi la polisi
kwamba matukio ya kujeruhi, kutesa au vifo ni halali iwapo wanasiasa au wananchi
hawakutii amri.
Kwa mtazamo wetu, amri ya serikali au polisi
haitakiwi kuwa juu ya Katiba inayolinda haki ya kuishi. Hivyo, kisingizio cha
kukiuka amri ya polisi hakitakiwi kuwa sababu ya kujeruhi wala kuua binadamu
yeyote. Hata kama polisi watatoa maelezo kukanusha kuwa picha ya mtu anayeteswa
si mwandishi, je wanayo haki ya kumjeruhi, kumtesa au kumdhalilisha mtanzania
yeyote kama inavyoonekana kwenye picha hizo?
Tangu matukio haya ya kujeruhi, kutesa na hata
kuua wananchi yalipoanza, hakuna hatua za dhati zilizochukuliwa na serikali wala
jeshi la polisi. Vitendo hivi vinavyofanywa na polisi siyo tu vinapunguza imani
ya jeshi hilo kwa wananchi, bali pia vinakiuka wajibu wa msingi wa jeshi hilo
ambao ni kulinda usalama wa raia.
Ni matumaini yetu kwamba waliohusika na kifo
cha Daudi Mwangosi na watanzania wengine waliopoteza maisha katika mazingira ya
aina hii, watachukuliwa hatua stahiki. Pia, maaskari wanaoonekana katika picha
hizo wakimtesa na kumnyanyasa raia wafikishwe kwenye vyombo vya sheria ili iwe
funzo kwa wengine.
Tunatoa pole nyingi kwa familia na ndugu wa
marehemu Daudi Mwangosi pamoja na tasnia ya habari hapa nchini.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema
peponi, Amen.
No comments:
Post a Comment