Habari za Punde

Zeco yarudisha huduma ya Umeme Hospitali ya Micheweni



MAFUNDI wa Shirika la Umeme Zanzibar ZECO tawi la Pemba, wakiwa katika harakati za kufunga transfoma mpya ilionunuliwa na ZECO kwa shilingi 20 milion, baada ya iliokuwepo kuungua wiki iliopita na kusababisha hospitali ya Micheweni Pemba kutumia taa aina ya vibatali ambapo kwa sasa huduma hiyo imerudi kama kawaida. (picha na Haji Nassor, Pemba)



 
Na Haji Nassor, Pemba

BAADA ya kukaa takriban wiki mbili wananchi wa Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, kukosa huduma ua umeme kufuatia transfoma iliokuwa ikisambaaza umeme kuungua, hali hiyo sasa imetuwama kufuatia Shirika la Umeme Zanzibra kufunga transfoma mpya.

 

Hafla ya ufungaji wa mashine hiyo mpya, ilifanyika jana mbele ya uongozi wa Wilaya na wananchi kadhaa waliohudhuria kutokana na kukosa huduma hiyo tokea katikati ya mwezi huu jambo lilizorotesha shuguli zinazotegea nishati hiyo ikiwa ni pamoja na Hospitali.

 

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamilika kwa kazi ya ufugaji wa transfoma hiyo na huduma hiyo kurejea katika halia yake ya kawaida, Msaidizi Afisa Uhusiano wa ZECO tawi la Pemba, Faki Othuman Sharif alisema kuwa jumla ya shilingi 20 milion zilitumika kununua mashina hiyo.

 

Alisema kuwa fedha zote hizo zimetolewa na ZECO ambapo mashine hiyo mpya (100 kv) ilinunuliwa Mkoani Arusha Tanzania bara na inauwezo mkubwa wa kusambaaza huduma ya umeme katika eneo hilo la Micheweni.

 

Faki alieleza kuwa, Shirika la Umeme kwa sasa limejipanga vyema katika kutoa huduma bora kwa wananchi na ndio maana muda mfupi tu, tokea kuungua kwa transfoma hiyo ikaharakisha kurejesha huduma kwa wananchi.

 

‘’Sisi Shirika la umeme kwa sasa tumejipanga vyema, maana dharura kama hizi wala hatuwashirikishi wananchi kama lazima watoe fedha, illa ZECO ndio hugharamia fedha zote na kuhakikisha tunawarejeshea wananchi huduma’’,alifafanua .

 

Aidha aliwataka wananchi wa maeneo mbali mbali kuhakikisha wanatoa taarifa za haraka Shirika la Umeme pale ambapo kumejitokeza hitalafu ya umeme badala ya kukimbilia kwenye vyombo vya habari ambapo msaada wake huchelewesha.

 

Hata hivyo ameupongeza uongozi wa Wilaya ya Micheweni na wananchi wote, kwa kuwa wastahamilivu katika kipindi chote cha ukosefu wa huduma hiyo, hadi hapo juzi iliporejea kama kawaida.

 

‘’Katika hili tunampongeza sana Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Juma Abdallah (mzee wa busara) kwa kuwatuliza wananchi wakati sisi ZECO, tulipokuwa katika mchakato wa kutafuta transfoma mpya’’,alizidi kufafanua.

 

Wakizungumza na mwandishiwa habari hizi, baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Micheweni walielezea kufurahishwa kwao na ZECO kwa kutimiza ahadi yao kama walivyoahidi juu ya kurejesha huduma hiyo.

 

Walisema kuwa kwa sasa Serikali kupitia Shrika hilo la Umeme, limejipanga kwa nia thabiti ya kuwaletea maendeleo wananchi na kutimiza ahadi wanazozitoa ambapo ni tofauti na miaka mengine.

 

Mutribu Hamad Mabarouk alisema kuwa, hawakutarajia kuwa huduma hiyo ingeweza kurudi juzi, kwani walidhani kuwa ahadi iliotolewa ni ya kuwatuliza wananchi na ingechukua hata wiki tatu.

 

Nae Mwanafunzi wa Skuli ya Micheweni sekondari anaesoma darasa la kumi na moja (FIII) Issa Omar Fundi, alisema kuwa kwa sasa wamepata matumaini maana hata kwa wale waliokuwa wakiendelea na masomo ya usiku majumbani yatarudi kama kawaida.

 

Shirika la umeme Zanzibar ZECO, limekuwa halina utaratibu wa kuwachangisha fedha  wananchi pale transfoma inapoungua au kuharibika, ambapo mchango hujitokeza iwapo wananchi wameomba transfoma kwa ajili ya kuunganisha huduma ya umeme katika vijiji vyao.

1 comment:

  1. sijui mpaka lini watu wataacha kufanyishwa kazi kienyeji, hakuna cha gloves, miwani wala kofia ngumu......tutafika?

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.