Na Othman Khamis, OMPR
MJUMBE wa Kamati Kuu ya
Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Balozi Seif Ali Iddi amema jumuiya za chama
zinaweza kukosa ufanisi kutokana na tabia ya baadhi ya viongozi kudharau wanachama
waliokubali kujitolea kuimarisha chama hicho.
Kauli hiyo aliitoa wakati akiufungua mkutano
mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mikoa miwili ya magharibi na mjini
katika ukumbi wa mikutano ofisi ya CCM mkoa Amani mjini Zanzibar.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa
Pili wa Rais alisema ipo tabia chafu iliyojengeka ndani ya chama kwa baadhi ya wanachama
kumuepuka mwanachama anayepoteza muda na nguvu zake kwa ajili ya kutetea na
kukisimamia chama katika utekelezaji wa sera zake.
Aliwataka wanachama na viongozi hao kuhakikisha
wanachagua wanachama wanaoelewa wajibu na dhamana zao katika jumuiya na chama
chenyewe.
Alifahamisha kwamba umoja wa vijana
pamoja na ule ya wanawake (UWT) zina mkono mkubwa na mrefu ndani ya chama kwa
sababu ya nguvu na wingi wao.
Hivyo alisema ni wajibu kwao
kuhakikisha wingi na nguvu hizo zinalindwa na kuenziwa ipasavyo.
Aliwatahadharisha vijana kuwa makini
katika ulinzi wa chama chao kwa vile zipo dalili zilizoanza kujichomoza za
kuvamiwa kwa jumuiya hiyo kwa malengo ya watu wachache wanaoelekeza nguvu zao
katika uchaguzi wa urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wa mwaka 2015.
“Kinacholeta tabu hivi sasa ambacho vijana
wameanza kutumiwa kwa nafasi ya urais wa Jamuhuri ya Muungano wa mwaka 2015. Msikubali
Jumuiya yenu ikatumiwa kwa maslahi binafsi,” alitahadharisha Balozi Seif.
Aliwataka wanachama wote wenye nia ya
kutaka kugombea nafasi hiyo ni vyema wakasubiri wakati utakapowadia na liliopo
sasa ni kuendelea kushirikiana na viongozi wenye dhamana hiyo katika kuwaletea
maaendeleo wananchi.
Akigusia suala la Muungano,aliwakumbusha
vijana kuwa CCM bado inaendelea kutetea sera za serikali mbili ambazo kila
mpenda maendeleo ameshuhudia ufanisi uliopatikana.
Alisema wapo baadhi ya watu
wanaochukia mfumo huo lakini alisisitiza kwamba wataendelea kuchukia kwa sababu
bado unaonekana kupendwa na wananchi pamoja na wanachama ambao ndio waamuzi
wakati wa mchakato wa mabadiliko ya katiba ya muungano wa Tanzania.
Akimkaribisha Balozi Seif, Mwenyekiti
wa UVCCM mkoa mjini magharibi anayemaliza muda wake, Tauhida Galos Nyimbo
aliwaasa vijana kuelewa kwamba kazi yao ni kujitolea wakati wote.
Alisema tabia ya baadhi ya wanachama
kujaziwa fomu za uongozi inadhoofisha nguvu za chama kwa vile muda mwingi wa
watu hao hutegemea kupata kipato zaidi badala ya kujitolea.
No comments:
Post a Comment