Na Hassan Hamad, OMKR
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha vitambulisho vya taifa kunakotarajiwa kuanza Oktoba 10.
Alisema suala la vitambulisho limekuwa na umuhimu wa kipekee duniani
katika kutunza kumbukumbu na mipango ya kitaifa, hivyo wananchi wasipuuze
kujiandikisha.
“Wananchi tafadhalini musipuuze, nendeni mkajiandikishe ili
mpate vitambulisho vya taifa, na nakwambieni mkipuuza mtakujajuta baadae,” alitahadharisha
Maalim Seif na kuongeza.
“Hivi sasa tunasikia kuna baadhi ya maeneo wananchi waliokataa
kuhesabiwa katika sensa ya watu na makaazi iliyomalizika hivi karibuni nchini
kote, hawapatiwi huduma katika maeneo yao, kwa hivyo nakunasihini sana wananchi
msipuuze kabisa.”
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama cha CUF, alitoa
kauli hiyo wakati akizungumza na wanachama wa CUF na wananchi baada ya kufungua
tawi la chama hicho jimbo la Magogoni wilaya ya magharibi Unguja.
Aidha Maalim Seif aliwaonya watendaji wanaoendelea kuwahangaisha
wananchi wakati wanapoomba kupatiwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi kuwa,
wanakwenda kinyume na maagizo ya Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein, na
kwamba watachukuliwa hatua za kisheria kwa kukaidi amri hiyo.
Alisema katika baadhi ya maeneo yakiwemo mikoa ya Pemba pamoja
na mkoa wa Kaskazini Unguja, hali ya upatikanaji wa vitambulisho hivyo imekuwa
ikienda vizuri lakini tatizo kubwa zaidi limekuwa likijitokeza katika mkoa wa mjini
magharibi, jambo ambalo halitofumbiwa macho.
“Vitambulisho hivi ni haki ya kikatiba ya kila Mzanzibari
aliyetimiza masharti ya ukaazi, leo anajitokeza sheha anawaambia wananchi kuwa
hatoi barua hadi mtu atimize umri wa miaka 50,”, alielezamaalim Seif.
Aliwataka watendaji wa ofisi ya vitambulisho vya Mzanzibari
Mkaazi kufanya kazi kwa uadilifu na kuepuka kutumiwa vibaya na viongozi kwa
maslahi ya kisiasa.
“Unapomkosesha mwananchi kitambulisho unakusudia nini, huu ni
ukiukwaji wa katiba na lazima tuukomeshe,” aliongeza.
Akizungumzia kuhusu nia ya kujiuzulu kwa Naibu Katibu Mkuu wa
CUF Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu, Maalim Seif amewathibitishia wanachama juu ya
ukweli wa jambo hilo, na kuwataka wasifadhaike kwani anafanya hivyo kwa nia njema.
“Jussa bado ni mwanachama kindakindaki wa CUF na ni mjumbe wa
baraza kuu la uongozi ndani ya chama chetu, lakini baada ya kutuletea maoni
yake tuliona sababu zake ni za msingi na hakuna haja ya kumzuia kutimiza
maamuzi yake,” alisema.
Alisema ifikapo Oktoba 10, Jussa atakuwa si Naibu Katibu Mkuu
tena wa CUF na kwamba viongozi wanatafakari juu ya kumpata mwanachama
atakaekaimu nafasi hiyo.
Ametaja sababu za msingi zilizotolewa na Jussa kutaka kujiuzulu
kuwa ni pamoja na kumuwezesha kupata muda wa kutosha kushugulikia maendeleo ya
jimbo lake la Mji Mkongwe pamoja na kufanya utafiti kabla ya kuibana serikali
katika vikao vya Baraza la Wawakilishi.
Katika Mkutano huo, Maalim Seif alikabidhi baskeli tisa kwa
ajili ya makatibu wa matawi ya CUF katika jimbo la Magogoni, kigari kwa ajili
ya Ali Khamis Ali pamoja na shilingi 300,000 kwa ajili ya kikundi cha ushirika
cha jimbo hilo.
No comments:
Post a Comment