Habari za Punde

Polisi adaiwa kumtelekeza msichana aliyemzalisha



Joseph Ngilisho, Arusha
MSICHANA mwenye umri wa miaka 20 (jina linahifadhiwa) mkazi wa kijiji cha Nduruma wilaya ya Arumeru, amemlalamikia askari polisi mmoja, aliyefahamika kwa jina la Said Rashird wa kituo kikuu cha polisi jijini kwa kumtelekeza baada ya kumzalisha.

Akizungumza kituoni hapo, aliwaambia wandishi wa habari kwamba, alizaa na askari huyo mtoto wa kiume aitwaye Nasri Said ambaye sasa ana umri wa miezi nane baada ya kuishi kama wapenzi na askari huyo katika makazi ya askari jijini hapa.

Msichana huyo aliendelea kudai mbele ya wandishi wa habari waliokuwa wamekusanyika ofisini kwa kamanda wa polisi mkoa wa Arusha kufuatilia habari za kipolisi kwamba alitokea kupendana na askari huyo hatimaye kuishi naye katika nyumba za askari zilizoko maeneo ya kituo kikuu cha polisi ambapo baada ya miezi kadhaa askari huyo alimlazimisha kumzalia mtoto bila kufunga naye ndoa.

“Baada ya miezi kadhaa ya kuishi naye akawa ananilazimisha kumzalia mtoto bila ndoa ambapo nikimuuliza alikuwa anasema  kuwa ananipenda hakuna shida tutaoana baada ya kuruhusiwa kuoa na mwajiri wake, kwani kwa sasa hawaruhusiwi kuoa kutokana na cheo chake, hivyo baada ya kuona kero za kuzaa zinazidi niliamua kubeba mimba ambapo ndipo hapo matatizo yalipoanzia”, alisema .


Aliongeza: “Baada ya kubeba mimba na kufikia miezi 8 mwanamme akawa ananinyanyasa na kunipiga kila siku hadi kutokwa damu puani hali iliyonisababisha kumwambia naenda kwetu.”

 “Baadae aliniambia nichukue kila ninachoweza kuchukua na baada kuchukua alikuja nyumbani kwetu wakati sipo na kuvichukua na kwenda polisi kuandika maelezo kuwa mimi nimemvunjia nyumba na kumwibia vitu”, alidai.

Asha ambaye alikuwa akiangua kilio mbele ya kamanda wa polisi mkoa, alidai kuwa hayupo tayari kuondoka ofisini hapo hadi apatiwe msaada huku akitishia kumwacha mtoto huyo ofisini,hali iliyomlazim kamanda huyo kumbembeleza kwa muda mrefu.

Alidai kwamba hali hiyo imemsababishia usumbufu mkubwa kwani wazazi wake wamechukia kutokana na askari huyo kuwadharau na kutumia uaskari wake kuwatishia ndugu zake kuwa atawashtaki hali iliyowafanya ndugu hao kukosa amani.

Alisema kutokana na wazazi wake na ndugu wengine kumchukia alilazimika kuomba hifadhi kwa mama yake mdogo.

“Huko nilidhani nitapata ahueni kutokana na manyanyaso lakini huko nako niliambulia kipigo kutoka kwa mwanamme huyu na hatimaye kusababisha mama mdogo naye kunifukuza”, alieleza kwa masikitiko huku akiwa amembeba mtoto wake Nasri ambaye alionekana kuwa na siha njema na mchangamfu wakati wote.

Alidai baada ya kufukuzwa nyumbani kwa askari huyo, yeye alikuwa akimfuata siku moja moja kumtaka kumpatia fedha za matumizi ya mtoto lakini alikuwa anaambulia matusi na kejeli.

Aidha alidai kuwa kutokana na mpenzi wake huyo kukataa kutoa fedha za malezi ya mtoto wao, aliamua kwenda kumshitaki Idara ya Ustawi wa Jamii, ambako alisema walipewa barua kumpelekea Mkuu wa polisi kituo cha kikuu.

“OCS alimwita mzazi mwenzangu huyo na kumkabidhi barua ya Ustawi wa Jamii ambapo aliahidi kutoa matumizi ya mtoto lakini hadi sasa hakuna chochote anachotoa kwa ajili ya mtoto na zaidi ya hayo mwanzoni mwa Oktoba alikana kumtambua huyu mtoto na hata mimi mama yake,”alilalamika.

Kutokana na hali hiyo, aliliomba jeshi la polisi kumsaidia kumsimamia askari huyoili mtoto wake apate matunzo mazuri kwani ni haki yake.

Mwandishi wa habari hizi alipowasiliana na Kamanda wa polisi wa mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, kuhusiana na madai ya msichana huyo, alitoa kauli tata.

Kwanza alisema asingeweza kuzungumzia suala hilo kwa madai kwamba hayo ni mambo binafsi lakini pia alisema kwa kuwa malalamiko hayo yanamhusisha askari wake atayafuatilia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.