Na
Ramadhan Himid
MKUU wa jeshi la Polisi, Saidi Ali Mwema
amesema jamii inahitaji kupewa elimu zaidi katika suala zima la kusimamia
ulinzi na usalama ili kujiepusha na viashiria vya uvunjifu wa amani na usalama
nchini.
Aliyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya
uongozi wa kati wa sajini meja, stafu sajenti na sajenti katika viwanja vya polisi
Ziwani .
Alisema jamii hainabudi kuwaelekeza vijana wao
katika kudumisha na kusimamia amani iliyopo kwani taifa lolote lisilo na amani
na usalama haliwezi kujiletea maendeleo .
Alisema suala la kudumisha usalama wa nchini
sio la polisi pekee bali kila mmoja kwa nafasi yake ana wajibu wa kuhakikisha
kwamba analinda maisha yake binafsi na maisha ya wenzake.
Sambamba na hilo alitilia mkazo sera ya polisi
jamii ambayo ndiyo nyenzo pekee inayotoa mashirikiano ya jeshi la polisi na
wananchi katika kupunguza matatizo yao katika maeneo wanamoishi.
Mwema alisema Tanzania inakabiliwa na changamoto za viashiria vya uvunjifu wa amani kwa baadhi ya watu kujiingiza katika vitendo vya vurugu na migogoro isiyo na tija kwa utashi na maslahi yao binafsi.
Aliitaka jamii kutowafumbia macho watu wachache wanaochochea fujo kwani uchunguzi unaonyesha kwamba kila penye migogoro na vurugu baadhi ya watu huwa wanatononoka na ndio maana hawako tayari kuona watu wengine wanaishi kwa usalama na amani.
"Kila mtu binafsi kuanzia nyumbani kwake, mtaani, kitongoji na taifa kwa ujumla ahakikishe kwamba amani inadumishwa na kuondosha dalili zote za viashiria vya uvunjifu wa amani,”alisisitiza .
Mbali na kutilia mkazo suala la ulinzi na
usalama aliwataka wahitimu hao kutoa huduma bora kwa wateja ili kuondokana na
malalamiko dhidi yao kutoka kwa wateja hao wanaowahudumia.
Awali Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali
Mussa alitoa wito kwa wananchi kuunga mkono sera ya polisi jamii na ulinzi shirikishi ili kukabiliana na kero
mbali mbali za kihalifu nchini.
Kwa upande wake mkuu wa chuo cha taaluma za
Polisi Zanzibar(ZPA), Ramadhan Mungi alisema wahitimu hao wamefunzwa kwa
kuzingatia ueledi wa hali ya juu na hivyo kuwataka wawe chachu kwa wenzao ambao
wanakwenda kuwasimamia katika sehemu zao za kazi kwa kutumia kauli mbiu
yao"jifunze, elewa ,fanya kwa usahihi).
Mafunzo hayo ya mwezi mmoja yalifunguliwa
mapema mwezi Septemba mwaka huu na kufungwa wiki iliyopita yakishirikisha jumla ya askari 47 wa sajeni meja,
stafu sajenti 275 na sajenti 618.
No comments:
Post a Comment