Joseph Ngilisho,Arusha
NAIBU Waziri wa Nishati na Madini ,George Simbachawene amewataka wanasheria kuweka maslahi ya taifa mbele wakati wanaposaini mikataba ya uchimbaji wa mafuta na gesi ili nchi pamoja na Watanzania waweze kunufaika na rasilimali hizo.
Hayo yalisema mwishoni mwa wiki jijini Arusha , wakati akifunga
mafunzo ya siku tano yaliyoshirikisha wanasheria pamoja na wataalam wa mafuta
na gesi juu ya kuangalia mikataba inayoingiwa na watafutaji na wachimbaji
mafuta na gesi baharini.
Alisema uchimbaji mafuta ni suala la muda mrefu lakini kwa
bahati nzuri gesi ndiyo imeweza kuleta neema zaidi kuliko mafuta ingawa bado
watafutaji wa gesi na mafuta wanaendelea kuangalia kama kuna uwezekano wa
kupata mafuta pia.
Alisema kutokana na uchimbaji huo wanasheria ni lazima wakaweka maslahi ya kitaifa mbele
ili nchi iweze kunufaika badala ya kujali maslahi yao binafsi ambayo hayaleti
tija.
“Wanasheria angalieni maslahi ya Taifa kwanza katika kusaini
mikataba msitangulize maslahi yeni binafsi tunataka gesi ikivumbuliwa au mafuta
basi nchi inufaike pamoja na wananchi kwa ujumla,” alisema.
Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye ni Kaimu
Mkurugenzi wa Utafutaji,Uzalishaji na Huduma za Kiufundi wa Shirika la Petroli
Tanzania (TPDC), Elias Kilembo alisema hivi sasa Tanzania imepiga hatua katika
ugunduzi wa gesi na mafuta kimataifa hivyo kutokana na takwimu wanazotoa
kampuni zinazotafuta mafuta ni lazima zitoe taarifa kwa wataalam ili nao waweze
kuzipitia na kuhakikisha katika masuala ya mikataba nchi inafaidika kwa asilimia
kubwa.
Alisema katika masuala ya mikataba kuna sheria zake na ni lazima
kumvuta mwekezaji na kulinda mapato kwa nchi na mwekezaji hivyo ni muhimu
wataalam kuangalia suala hilo kwa makini ili kuondokana na mikataba mibovu
inayolalamikiwa na watu.
No comments:
Post a Comment