Kamishna wa Polisi Mussa Ali Mussa akifafanua jambo katika Mkutano na Waandishi wa Habari akielezea juu ya Fujo na Ghasia zilizotokea katika Mkoa wa Mjini Magharibi na kupelekea kifo cha Askari Mmoja,Mkutano huo umefanyika hapo katika Makao Makuu ya Polisi Ziwani Mjini Zanzibar.
-Baadhi ya Waandishi wa Habari wakiwa katika Mkutano wa Jeshi la Polisi kuelezea juu ya Fujo na Ghasia zilizotokea katika Mkoa wa Mjini Magharibi na kupelekea kifo cha Askari Mmoja,Mkutano huo umefanyika hapo katika Makao Makuu ya Polisi Ziwani Mjini Zanzibar.
PICHA NA MAKAME MSHENGA-MAELEZO ZANZIBAR.
Na Ramadhan Ali na Mwanaisha Mohammed-Maelezo Zanzibar 18/10/2012
Askari mmoja wa Jeshi la Polisi F.2105 Coplo Said Abdulrahaman wa Kikosi cha FFU Mkoa Mjini Magharibi ameuliwa kinyama kwa kupigwa mapanga kichwani na mikononi wakati akirudi kazini majira ya saa 6.30 usiku katika eneo la Bububu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Ziwani, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa amesema mauaji hayo yamesababishwa na fujo za wafuasi wa Jumuiya ya UAMSHO baada ya kuenea uvumi wa kutekwa Msemaji Mkuu wa Jumuiya hiyo Sheikh Farid Hadi usiku wa kuamkia jana.
Kamishna Mussa amesema Jeshi la Polisi linaendelea na msako wa kuwatafuta watu waliofanya mauaji ya Coplo Saidi Abdulrahaman ili kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani kama sheria za nchi zinavyowaelekeza.
Amesema mpaka hivi sasa watu 10 wamekamatwa kwa tuhuma za makosa mbali mbali yaliyotokana na vurugu za jana na upelelezi wa kujua ukweli juu ya uvumi wa kutekwa Sheikh Farid unaendelea.
Ameongeza kuwa kutekwa kwa Sheikh Farid kunatia mashaka kutokana na mazingira ya kutoweka kwake kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mdogo wake Said Omar Said ambae alikuwa dereva wake katika hatua za mwisho maeneo ya Mazizini walipokwenda kununua umeme.
“Sheikh Farid alimuamuru Said amuache katika eneo hilo aende nyumbani kupeleka umeme na wakati huo akaendelea na mazungumzo na watu wengine walikuwemo ndani ya gari nyengine ndogo ya NOAH ambayo nambari zake hazijajulikana lakini aliporudi kumchukua hakumkuta” alisema Kamishana Mussa.
Amesema fujo hizo zilisababisha hasara kubwa kwa Serikali, Chama tawala na wananchi ikiwemo kuchoma na kuharibumiundo mbinu ya barabara, kuharibu maskani za CCM za Kisonge na Muembeladu kwa kuzichoma moto baadhi ya magari kuvunjwa vioo na kuvunja duka la pombe na kuiba mali iliyokuwemo ndani.
Hata hivyo amedai hali ya Mji wa Zanzibar kwa sasa ni shwari, wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vikosi vyengine vya ulinzi na usalama vitaendelea kuhakikisha amani inadumu muda wote.
Amewataka wananchi kuendelea kuwa wavumilivu na kudumisha amani na utulivu katika maeneo yao, na kutoa taarifa za watu waliohusika na vurugu pamoja na mauaji ya Coplo Said Abdulrahaman.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR
Huyu anasisitiza tu kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi ili kujua nani kahusika na mauaji ya Coplo Said na pia akawataka watu kutoa taarifa ya nani kahusika na mauaji ya Coplo Said, sawa watu wamefanya kosa kumuua Coplo Said.
ReplyDeleteLakini mbona huyu kamishna kwa haya mazungumzo yake haonekani kuguswa na tukio la kutoeka kwa Amir farid?.
Kama alivyosisitiza kwa mauaji ya Coplo Said hasema kwamba jeshi la polisi litahakikisha linafanya uchunguzi ili kujua ni nani anaehusika na kutoeka kwa Amir Farid?.
Mbona mm nakua na mashaka juu ya tukio hili? hapa inaonekana kama kuna mchezo umefanyika kwa sababu Polisi inaonekana kama kutojali juu ya suala hili.