Habari za Punde

Kisassi ataka wanachama CCM wapewe nguvu.


MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Thuwaybah Edington Kisassi, amesema umefikia wakati kwa chama hicho, kupendekeza ndani ya katiba mambo yatakayowapa nguvu wanachama kuwaondoa viongozi wanaokisaliti chama.

Hayo aliyasema jana wakati akifungua mkutano mkuu wa uchaguzi wa CCM Mkoa wa Kaskazini, uliofanyika hoteli ya Kiwengwa Strend, wilaya ya kaskazini ‘B’ Unguja.

Alisema ni lazima chama kifikirie suala hilo kutokana na mtindo ulioanza kwa baadhi ya viongozi kuanzisha vitendo vinavyoenda kinyume na sera ya CCM huku wakitambua fika kwamba hata wakifanya wataendelea kubakia maadarakani.

“Lazima chama kifikirie kuwa na utaratibu wa kuwavua uongozi kabla ya muda wao, viongozi ambao wanaenda kinyume na taratibu za chama," alisema.

Alisema hilo litawafanya wanachama kujenga imani na chama chao.

Alisema baadhi ya viongozi wamekuwa wakisahau viapo walivyoapa kwa kuacha kusimamia misimamo ya chama na kuanza kufuata sera ambazo hazikubaliani na chama.

Alisema mfumo wa vyama vingi upo lakini bado kila chama kinaendelea kubakia na sera zake na haitakuwa vyema kwa wanachama wa CCM kwenda kinyume misimamo ya chama chao.

“Mtu utamsikia anasema kura hazimtoshi na baadae kuamua kwenda upande wa pili, huyu tayari alikuwa na mipango hiyo tangu awali sasa ndani ya CCM msitafute sababu ya kudai wanaitwa uamsho anaejiona hawezi kukifanyia kazi kwa sera zake basi aondoke kwa amani na kubwa wakubali kurejesha kadi ya CCM,” alisema.

Aidha alisema inasikitisha kuona hivi sasa baadhi ya watu wameanza kujenga tabia ya kuitumia vibaya siku tukufu ya Ijumaa kwa kuanzisha mikutano inayochochea uvunjifu wa amani.

Aliwataaka wanaCCM wasikubali kurudi nyuma kwa kushiriki vitendo vya uvunjifu wa amani kwani si lengo la CCM, kuona nchi inarudi ilipotoka.

Alisema demokarasia yoyote haitaki mabavu na ni vyema kwa waCCM wakazingatia hilo ili kuona amani na utulivu inabakia.

Akitoa shukrani kwa wajumbe hao,mjumbe wa kamati ya siasa mkoa wa kaskazini, Ali Ameir Mohammed, alisema ipo haja serikali ikadhibiti vitendo vya uvunjifu wa amani kutokana na baadhi ya makundi ya watu kuanza kutukana viongozi wa nchi.

Alisema hali hiyo inaashiria vitendo vibaya amabavyo vinaweza kuingiza nchi katika uvunjifu wa amani amabao hivi sasa hauhitajiki.

Hata hivyo, alisema ni vyema CCM kuacha kuwafumbia macho viongozi wanaofanya vitendo vya kukihujumu chama.

“Mimi nilipoona ipo haja ya kukaa upande nilifanya hiyo lakini bado nitabaki kuwa mwanasiasa nilichoacha ni uongozi lazima tufikie mahali kuambizana ukweli tusiwe wazee wanafiki,” alisema Ameir.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.