Habari za Punde

Kitengo cha viungo na vilema Mnazimmoja chaomba kutupiwa jicho na Serikali

 Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kijiji cha Bweleo akiwa pamoja na Viongozi wa Kamati ya Uongozi wa Msikiti wa Ijumaa wa Kijiji hicho Bwana Mataka Makame akimuelezea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi changamoto zinazowakabili Kijijini hapo mara baada ya sala ya Ijumaa.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Sweif Ali Iddi akikagua jingo litakalokuwa Ofisi Kuu ya Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar liliopo Mtaa wa Mombasa Wilaya ya Magharibi. Kushoto ya Balozi Seif ni Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Malik Abdulla Juma

Mkuu wa Kitengo cha Viungo na Vilema katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Dr. Adam Haji Makame akimpatia ufafanuzi wa kazi za Kitengo hicho Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipofanya ziara fupi ya kuangalia huduma katika Kitengo hicho.

Na Othman Khamis Ame , OMPR
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeombwa kufanya juhudi za ziada katika kukiimarisha kitengo cha Viungo na Vilema Kiliopo katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ili kiwe na uwezo wa kuhudumia wagonjwa kwa ufanisi zaidi.
Ombi hilo limetolewa na Wafanyakazi wa Kitengo hicho chini ya Usimamizi wa Mkuu wake Dr. Adam Haji Makame wakati Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara fupi ya kukagua shughuli za kazi za Kitengo hicho.
Wafanyakazi hao walimueleza Balozi Seif kwamba Kitengo hicho kimekuwa kikitoa huduma kwa kutumia vifaa vya zamani pamoja na Wafanyakazi hafifu kulingana na idadi kubwa ya Wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.
Walisema ipo haja kwa Serikali Kuu kufanya utaratibu wa haraka wa kuwasomesha Vijana waliomakini ambao watakuwa na moyo na uzalendo wa kusaidia Jamii yao.
“ Tumekuwa tukishuhudia Vijana wengi wanaosomea kada hii lakini cha kushangaza wamalizapo tuu mafunzo yao hata yale ya cheti huingia Mitini jambao ambalo linatuiwa vigumu sisi tunaohitaji kusaidia kazi hii”. Walisema wafanyakazi hao wa Kitengo cha Viungo na Vilema.
Walifahamisha kwamba Kitengo hicho kimekuwa kikipokea wagonjwa zaidi ya 1300 kwa mwezi wanaohitaji huduma za hapo lakini uwezo wa kuhudumia wagonjwa hao ni mdogo hasa ikizingatiwa uhaba wa Vifaa na Wafanyakazi.
Hata hivyo wafanyakazi hao pia wanalazimika wakati mwengine kuandaa ratiba ya kuwafuata wagonjwa wengine katika maeneo ya hapa Zanzibar kulingana na hali ya ulemavu wa baadhi ya wagonjwa ambao wako Vijijini.
Akitoa shukrani zake kwa Wafanyakazi hao wa kitengo cha Viungo na Vilema kutokana na kazi kubwa inayowakabili kila siku Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali itaangalia uwezekano wa kufanya mageuzi katika kitengo hicho.
Balozi Seif alifahamisha kwamba hatua hiyo inaweza kukifanya Kitengo hicho kufanya kazi zake kwa ufanisi na kitaalamu zaidi.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alilikaguwa Jengo la itakayokuwa Ofisi Kuu ya Bodi ya Chakula ,Dawa na Vipodozi liliopo Mtaa wa Mombasa.
Jengo hilo lililokuwa la Kiwanda cha Kampuni ya Uchapaji wa Al- Khayria linahitaji kufanyiwa matengenezo makubwa kufuatia baadhi ya Vifaa vyake likiwemo paa kuibiwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar Nd. Burhan Othman Said alisema kazi iliyopo hivi sasa ni kulifanyia matengenezo makubwa Jengo hilo licha ya uchafuzi wa mazingira kwa kuchimbwa mchanga unaofanywa na baadhi ya watu pembezoni mwa jengo hilo.
Akizungumza na Uongozi huo Balozi Seif ameiagiza Wizara ya Afya kufanya utaratibu wa kuliezeka kwa haraka jengo hilo ili kujaribu kusaidia kukabiliana na hali hiyo.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwapongeza Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na Wananchi wa Kijiji cha Bweleo kwa ari yao kubwa ya kujiletea Maendeleo.
Balozi Seif alitoa pongezi hizo mara baada ya Sala ya Ijumaa Katika Msikiti wa Kijiji hicho alipokuwa akisalimiana na Waumini hao wa Dini ya Kiislamu.
Alisema utaratibu wa Wananchi hao wa kujitatulia kero na matatizo yanayowakabili ni kitu kizuri kwani huleta faraja shauku ya kusaidia na wapenda maeneleo popote pale.
“Huu ni miongoni mwa Misikiti michache hapa Nchini ambayo imejengwa na Waumini wenyewe bila ya kutegemea nguvu za wafadhili”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Wananchi na Waumini hao kwamba ataangalia utaratibu wa kusaidia ujenzi wa vyoo na sehemu ya kutawadhia katika Msikiti huo wa ijumaa

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.