Habari za Punde

Vurugu zaendelea Zanzibar mmoja apigwa risasi na kuuawa

Na Salma Said
 
VURUGU zimeendelea Zanzibar huku mtu mmoja akiuawa baada ya kupigwa risasi ya moto na askari wa Kikosi cha Valantia (KVZ) usiku wa kuamikia jana.

Habari za kuaminika zinasema mtu huyo, Salum Hassan Muhoja mwenye umri wa miaka 30 mkazi wa Regeza Mwendo nje kidogo ya mji wa Zanzibar alipigwa risasi karibu na Amaan mjini hapa.

Inaaminika kuwa mtu huyo alipigwa risasi wakati akipita karibu na baa na nyumba ya kualala wageni Mbawala Amaan ambayo ilivunjwa katika ghasia hizo.

Kijana huyo alitarajiwa kuzikwa jana jioni kijijini kwao Mwera Regeza Mwendo wilaya ya Magharibi Unguja.


Wakati kukiwa na habari hizo za mauaji vijana kadhaa wenye umri wa kati ya miaka 14 na 18 waliingia barabarani eneo la Darajani na kupambana na askari ambao walikuwa wametanda wakilinda doria.

Vijana hao huku wakiimba “tunamtaka amiri wetu , tunamtaka amiri wetu, tunamtaka amiri wertu” walitawanywa na askari hao huku wakirusha mawe kwa askari hao.

Hali hiyo iliwafanya polisi kupiga ovyo mabomu ya machozi katika mitaa ya Zanzibar huku wakifyatua risasi za moto na kuufanya mji kuhanikiza kwa vishindo vya mabomu na risasi na kuzifunga barabara kadhaa.

Baada ya sala ya Ijumaa katika misikiti mbalimbali hali ilonekana kuwa tulivu mjini hapa huku askari wakiwa wamejaa mitaani wakiwa kwenye magari na wengine wakitembea kwa mgguu wakiwa wameshikilia bunduki.

Katika baadhi ya misikiti wakati wa sala ya Ijumaa ilisomwa dua marufu ya Kunuti ikiwa ni sehemu ya kuiombea amani nchi kutokana na vurgu hizo.

Hali ilianza kuchafuka saa 8 mchana wakati kikundi cha vijana kilichokuwa kimejikusanya eneo la Uwanja wa Malindi kuingia barabarani huku wakipiga kelele za kumtaka amiri wao, Farid Hadi Ahmed ambaye alitoweka tangu Jumanne iliyopita.

Kupotea”kwa sheikh huyo ndiko kulikozua ghasia mjini hapa tangu Jumatano na kufanya mji usikalike huku biashara zote zikiwa zimefungwa na askari mmoja kuchinjwa Jumatano usiku.

Wafuasi wa Sheikh huyo wanaamini kwamba kiongozi wao amekamatwa na serikali kwa hiyo wanashinikiza ili aachiwe huru.

Barabara za mjini hapa zimejaa takakataka za kila aina kuanzia vifusi, mawe makubwa, matairi yaliyochomwa moto, matofali na vifuu vya madafu na kuharibu miundombinu kadhaa zikiwemo kukata waya.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Kamishna Msaidizi wa Polisi, Said Juma Hamis alisema kuwa hana taarifa za kuuawa kijana huyo zaidi ya zile za kuuawa kwa skari wao Bububu.
Alisema kwamba jeshi lake litafuatilia kwa karibu juu ya tukio hilo ili kujua ukweli wake,
Kamanda Hamis alisema kuwa hadi jana jumla ya watuhumiwa waliokamatwa kutokana na vurugu hizo ni 39 huku wanane walifikishwa mahakamani jana na wengine wanaendelea kuhojiwa na Polisi.
Kaimu Kamanda huyo pia alisema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na juhudi zake za kumtafuta kiongozi huyo wa Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislamu, Sheikh Farid ambae anadaiwa kutekwa.
Alisema kuwa katika kufanikisha juhudi hizo jana kulifanyika kikao cha wapelelezi kilichoongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi Zanzibar, ACP Yussuf Ilembo kujadili namna gani wanaweza kumpata au kujua yupo wapi Sheikh huyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.