Na Hassan Ali Ame
JAJI wa Mahakama Kuu Zanzibar, Abraham Mwampashi, amesema Mkurugenzi wa
Mashitaka (DPP) hana mamlaka ya kuiamuru mahakama nani apewe dhamana na nani
anyimwe.
Alisema hayo alipokuwa akitoa hukumu juu ya kesi ya viongozi 10 wa Jumuiya ya
Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu wanaomlalamikia kufungwa dhamana yao na
Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar Ibrahim Mzee Ibrahim.
“Mkurugenzi wa mashitaka hana mamlaka ya kusema nani apewe dhamana na nani
asipewe, ingawa anayo haki ya kumzuia ofisa yeyote wa polisi asitoe dhamana,”
alisema Jaji Mwampashi.
Alisema kwamba katika misingi ya utawala wa sheria na utawala bora, mahakama
ni muhimili unaojitegemea, suala la dhamana linaendelea kubaki kuwa la mahakama,
si kwa Mkurugenzi wa Mashitaka.
Kutokana na uamuzi huo Jaji Mwampashi aliwataka wadai kuwasilisha ombi jipya
la dhamana, lisikilizwe na kutolewa uamuzi na Mahakama Kuu, si Mrajis wa
mahakama kama ilivyokuwa hapo awali.
Pia, Jaji Mwampashi alisema DPP alipaswa kuweka wazi sababu za kukataa
dhamana kutolewa kwa walalamikaji ili mahakama iweze kupima uzito wake na
wahusika waweze kujitetea.
Kwa msingi huo alisema Mahakama Kuu imefuta maamuzi yote yaliyokuwa
yametolewa na Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar, Geroge Kazi, yakiwemo ya kufunga
dhamana ya watuhumiwa baada ya kuridhia hoja ya DPP ya kuzuia dhamana hiyo.
“Maamuzi ya Mrajis yote yanafutwa kwa sababu hakuwa na mamlaka kisheria
kupokea ombi la dhamana pamoja na kulitolea maamuzi, wakati kesi imefunguliwa
Mahakama Kuu,” alisema Jaji Mwampashi.
Katika mahakama hiyo ambapo kulikuwa na ulinzi mkali wa polisi wenye silaha
za moto, Jaji Mwampashi alihoji kuna haja gani kuwa na mahakama, kama mtu mmoja
anakuwa na haki ya kunyang’anya uhuru wa mtu mwingine?
Tangu kuanza kwa kesi hiyo Oktoba 25, mwaka jana, mawakili wa utetezi
wamekuwa wakipinga kitendo cha DPP kufunga dhamana.
Jaji Mwampashi alisema sheria iliyotumiwa na DPP kufunga dhamana ya
watuhumiwa ambayo ni Ibara ya 19(1)(2) inampa uwezo wa kumuagiza ofisa wa polisi
peke yake, si mahakama.
Alisema DPP alichotakiwa kueleza wakati wa kupinga dhamana ni sababu zipi za
kuishawishi mahakama isitoe dhamana kwa watuhumiwa.
Hata hivyo alisema hawezi kufuta kibali cha DPP cha kufunga dhamana kwa
sababu hakupewa nafasi ya kuja mahakamani kutetea hoja yake, lakini aliutaka
upande wa walalamikaji kuwasilisha upya ombi la dhamana Mahakama Kuu.
Viongozi hao wakuu wa Uamsho wanakabiliwa na mashitaka manne yanayohusiana na
kuharibu mali na kuhatarisha usalama wa taifa kinyume cha kifungu cha 3(d) cha
Sheria ya Usalama wa Taifa, Sura ya 47, ya mwaka 2002.
Washitakiwa hao ni masheikh Farid Hadi Ahmed, Mselem Ali Mselem, Mussa Juma
Issa, Azzan Khalid Hamdan, Suleiman Juma Suleiman, Khamis Ali Suleiman, Hassan
Bakari Suleiman, Gharib Ahmada Omar, Abdalla Said Ali na Fikirini Majaliwa
Fikirini.
Tangu kesi yao ilipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Oktoba 25, mwaka
jana, wamekuwa wakirudishwa rumande kwa sababu DPP ametoa kibali cha kufunga
dhamana kwa muda usiojulikana.
Watuhumiwa hao walifungua kesi Mahakama Kuu kutaka ifanye mapitio maamuzi ya
Mrajis na kuyatengua, pia ifute maamuzi ya DPP kufunga dhamana yao.
Watuhumiwa hao wanatetewa na mawakili wanne wakiongozwa na Salum Toufiq,
Abdalla Juma Mohamed, Rajab Abdalla Rajab pamoja na mwanasheria maarufu Suleiman
Salim.
Kutokana na uamuzi wa Jaji Mwampashi, kesi ya msingi itasubiri kupangiwa jaji
ili kujulikana siku ya kutajwa kwake.
Chanzo : Tanzania Daima
Ni aibu kwa DPP.
ReplyDeleteNi aibu kwa DPP na SMZ kuwanyima haki wananchi wake na kuwabambikizia hoja zisizo na msingi kuwanyima haki zao za kikatiba ndio maana wengi hawana imani na viongozi wa serikali. DPP alikuwa anaheshimika kwa kutetea haki za zanzibar na wananchi wa zanzibar lakini amejitia doa kwa utashi binafsi wa kisiasa. Zamani ukisikia DPP amepangiwa kuzungumza katika hafla fualani wengi wakiacha shughuli zao kumsikiliza wakiamini ni mtu mwema lakini hivi sasa amejitia aibu kweli na kuishusha hadhi yake kwa wazanzibari walio wengi. Anahitaji kujirekebisha na kuwaomba radhi wazanzibari ikiwa anataka kuendelea na hadhi yake ya awali kwa umma wa kizanzibari ambao unanyanyaswa kila siku.
ReplyDelete