RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali
Mohamed Shein leo ameongoza hitma ya kumuombea dua Rais wa kwanza wa Zanzibar
Marehemu mzee Abeid Amani Karume, iliyofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui
mjini Zanzibar.
Hitma
hiyo pia, ilihudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk.
Jakaya Mrisho kikwete, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.
Mohammed Kharib Bilal, Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Ali
Hassan Mwinyi pamoja na Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif
Hamad.
Viongozi
wengine ambao walihudhuria katika hitma hiyo ni Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Idd na Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
Mhe. Amani Abeid Karume, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabhi, Kadhi
Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Sheikh Mussa Salum kutoka Mkoa wa
Dar-es-Salaam nae pia, alihudhuria.
Wengine
ni viongozi wa serikali zote mbili na viongozi wastaafu, viongozi wa vyama vya
siasa, Masheikh kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, Wabunge na Wawakilishi,
wananchui kutoka sehemu mbali mbali pamoja na Mabalozi wadogo waliopo hapa
Zanzibar.
Hitma
hiyo ilitanguliwa na Qur-an tukufu, iliyosomwa na Ustadh Sharif Muhidin na
kuongozwa na Sheikh Yussuf Mohammed Khamis.
Mara
baada ya hitma hiyo, Sheikh Mkoa wa Dar-es-Salaam, Sheikh Mussa Salum alitoa
mawaidha na kumuelezea marehemu mzee Abeid Amani Karume kuwa ni kiongozi
aliyepigania maendeleo ya wananchi wa Zanzibar na kumuombea MwenyeziMungu ampe
makaazi mema Peponi.
Akieleza
kuhuhu umauti, Sheikh Mussa alisema kuwa umauti ni jambo ambalo litafika kwa
kila kiumbe alichokiumba MwenyeziMungu na kusisitiza kuwa ni vizuri mwanaadamu
akakumbuka asili yake na hatma yake.
Baada ya
kisomo hicho cha hitma ambacho hufanyika kila mwaka inapofika tarehe 7, Aprili,
viongozi hao na wananchi waliohudhuria katika hitma hiyo walimuombea dua,
marehemu mzee Abeid Karume katika kaburi lake lililopo pembezoni mwa afisi hiyo
ya CCM Kisiwandui dua iliyoongozwa na viongozi wa dini tofauti akiwemo Mufti
Mkuu wa Zanzibar Sheikh Omar Kabhi, Askofu Michael Hafidh kutoka Kanisa la
Anglikana Zanzibar.
Viongozi
na wanafamilia waliweka mashada ya maua katika kaburi la marehemu mzee Abeid
Amani Karume akiwemo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk.
Jakaya Mrisho Kikwete, Waziri Kiongozi Mstaafu wa Zanzibar Mhe. Ramadhan Haji
Faki aliyeweka shada la maua akiwakilisha wazee walioshiriki Mpinduzi ya
Januari 12, 1964.
Mwakilishi
wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania Meja Jenerali Hassan Vuai
Chema, Balozi Ali Karume aliyewakilisha watoto wa Marehemu Karume na Balozi
mdogo wa Misri anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Balozi Walid Mohamed Ismail
aliyewawakilisha Mabalozi wenzake wa hapa nchini na Ahmed Amani Karume
aliyewakilisha wajukuu.
Aidha
mjane wa marehemu mzee Abeid Karume, Mama Fatma Karume, alishiriki katika hitma
hiyo akiongozana na Mama Salma Kikwete, Mama Asha Balozi na Mama Pili Balozi,
Mama Shadya Karume na viongozi wengine wanawake wa kitaifa wakiwemo Mawaziri,
Wabunge, Wawakilishini na wananchi kutoka sehemu mbali mbali ya Zanzibar na
Tanzania Bara.
April 7,
1972 ndiyo siku aliyouawa Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehemu Mzee Abeid Amani
Karume na wapinga maendeleo nchini ambapo hivi leo imetimia miaka 41 tokea
utokee msiba huo.
No comments:
Post a Comment