Habari za Punde

Takukuru inahitajia muda gani kuchunguza suala la kina Morris?

Na Salum Vuai
 
USEMI mashuhuri wa lugha ya Kiswahili ‘Kimya kingi kina mshindo mkuu’, hauna maana kwamba mshindo huo ni lazima utakuwa na neema au faraja kwa mtu anayesubiri kuvunjwa kwa ukimya huo.

Yumkini, baada ya kimya kirefu na kusubiri kulikovuka mpaka, mtu asubiriye akajikuta amewekwa katikati ya kitahanani na machungu yasiyoweza kuvumilika.
Ingawa wapo wanaosema kuwa subira ni ufunguo wa faraja, lakini dhana hiyo inakuwa kweli na tamu kwa wale tu ambao kusubiri kwao kumewasaidia kutimiza malengo yao, lakini kwa wenzangu mimi wenye bahati ‘nyeusi’ subira kwao ni tanuri la moto.

Dhamira yangu katika dibaji hiyo hapo juu, ni kujaribu kuizindua Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), ipekue majalada yake ili kuharakisha kazi iliyokabidhiwa na uongozi wa klabu ya soka ya Azam FC kuchunguza madai ya baadhi ya wachezaji wake kupokea rushwa.

Wasiwasi wangu ni kuwa huenda maofisa wa taasisi hiyo nyeti nchini, wamesahau kwamba walipewa kazi ya kuwachunguza wachezaji hao baada ya klabu yao kuwatilia wasiwasi kwamba wamekula rushwa.

Wachezaji hao wanne waliosimamishwa na Bodi ya klabu ya Azam FC tangu wiki ya kwanza ya mwezi Novemba mwaka uliopita, ni Said Morad, Erasto Nyoni, Deo Munishi na Aggrey Morris, wakidaiwa kupokea rushwa katika mchezo wa timu yao hiyo dhidi ya Simba kwenye ligi kuu msimu wa 2011/2012.

Katika mchezo huo, Azam FC ililala kwa mabao 3-1.
Wanandinga hao walisimamishwa kwa lengo la kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo, kazi iliyokabidhiwa TAKUKURU.

Huu ni mwezi wa tano sasa, wachezaji hao wamekuwa katika kitanzi bila kujua hatima yao na Azam itakuwaje huku msimu wa ligi ukikaribia kumalizika, na hakuna dalili kama TAKUKURU ina habari yoyote kuhusiana na kadhia hiyo.

Ingawa wawili kati ya wachezaji hao wameendelea kuitwa na kuichezea timu ya taifa ya Tanzania , ‘Taifa Stars’, bado wana haki ya kutaka kuharakishwa kwa uchunguzi wa kadhia hiyo, ili waelewe nini cha kufanya hasa katika kipindi hichi ambapo msimu wa ligi kuu unaelekea ukingoni.

Katika kufuatilia kwangu suala hili kwa uongozi wa Azam, nilipata kauli za kushangaza kwamba, hao ni wachezaji wao na hawafikirii kuwaacha licha ya tuhuma zinazowakabili.

Pamoja na kudai kuwa, wao pia wanashangazwa na ukimya wa TAKUKURU, lakini hata hivyo, wamesema hawawezi kuihimiza taasisi hiyo, wakisema ni ya serikali na inajua majukumu yake.

“TAKUKURU ni taasisi ya serikali kama ilivyo Polisi, hazifanyi kazi chini yetu”, aliniambia mmoja wa viongozi wa juu wa klabu hiyo.

Nilipomuuliza kiongozi huyo wa Azam kama haoni haja ya kuwasamehe tu wachezaji hao na kutangaza kuwaondoa katika timu yao ili wajue jinsi ya kujipanga, yeye alijibu kwa kuniuliza, kama nami pia ninatetea wala rushwa.

Jibu hilo lilinipa mshangao kwa kuwa lilidhihirisha kwamba tayari kwa upande wa Azam, wachezaji hao wametiwa hatiani hata kabla ya TAKUKURU kutoa ripoti ya uchunguzi iliotakiwa kuufanya.

Kwa ninavyofahamu mimi, na ninaamini na wengine pia, wachezaji hao bado ni watuhumiwa, na itakuwa dhambi kuwatia hatiani moja kwa moja.

Lakini suala linakuja, je, kwa nini TAKUKURU inachelewa kuweka mambo hadharani ili umma wa wapenda soka na hasa wapenzi wa Azam FC waelewe hatima ya wachezaji hao.

Kwa inavyoonekana, ni wazi kwamba hata hiyo TAKUKURU imejisahau, kwani sidhani kama suala hilo lingehitaji zaidi ya miezi miwili kulifanyia uchunguzi na kuukamilisha.

Kama nilivyotangulia kusema awali, kwamba kimya hicho kirefu, kinawapa wakati mgumu wachezaji hao, kwani kwa sasa wanalazimika kufanya mazoezi na timu za mchangani ili kujiweka fiti, hasa kwa Morris na Nyoni ambao ni miongoni mwa wanandinga wa Taifa Stars.

Kufanya mazoezi na timu za mchangani hasa kwa wachezaji wanaotegemewa sana na kocha mkuu katika timu ya Taifa, si vizuri kwani viwango na ushindani wanaopata huko hauwiani na ule wa timu hiyo ya Taifa.

Hivi karibuni, Nyoni alikaririwa na blogi moja hapa nchini akisema, kufanya mazoezi kwa muda mrefu na timu za mitaani au maarufu ‘mchangani’, kumechangia kupunguza makali yake na hivyo kutokucheza kwa kiwango kilichotarajiwa katika mechi dhidi ya Morocco hivi karibuni.

Hata hivyo, napenda nimpongeze kocha mkuu wa Taifa Stars Kim Poulsen, kwa kuwa muwazi na kusema kwamba, wanasoka hao ni muhimu na hawezi kuwapoteza.

Hapa sina maana ya kuwasapoti kama watakuwa kweli wamehusika na kupokea rushwa ili waihujumu klabu yao , Simba.

Lakini dhamira yangu ni kuizindua TAKUKURU, ili kama itakuwa imesahau kuwa ilipewa kazi ya kuchunguza iIi kubaini kama kweli wachezaji hao wamekula mrungura, iamke sasa na itoe haraka matokeo ya uchunguzi wao ili mbivu na mbichi ijulikane mapema.

Kama kweli itathibitika kuwa walihusika na makosa hayo, sitakuwa na pingamizi ya kuadhibiwa na klabu yao , lakini la kuuliza hapa, ni hadi lini tuendelee kusubiri jambo ambalo nina shaka kuwa pengine hata uchunguzi wake haujaanza?

Kama TAKUKURU ingekuwa makini, na nia ya dhati kushughulikia kadhia hiyo, ninaamini ingekwishafanya hivyo zamani, na hatima ya wanasoka hao ingeshajulikana.

Mimi si mtaaalamu wa mambo ya sheria, lakini pia sidhani kama kesi ya akina Morris inahitaji muda wote huo kuthibitisha ukweli wake.

Ligi kuu ya soka Tanzania Bara iko ukingoni na karibuni hivi itafikia tamati.
Bila shaka baada ya hapo, klabu zitakuwa katika harakati kubwa za usajili, huku zikiwa na orodha ya wachezaji wapya zitakaotaka kuwavuta kutoka timu nyengine, na wale wa kuwaacha.

Katika hili, bila shaka wachezaji hao wanne waliosimamishwa na Azam FC, watapaswa kufahamu kauli na matakwa ya klabu hiyo juu yao, kama itapenda kuendelea kuwa nao au itataka kuwafungulia mlango ili watafute timu nyengine.

Ili hilo liwezekane, na kwa vile walisimamishwa kwa tuhuma nzito, ni lazima TAKUKURU imalize uchunguzi wake na kuweka bayana mazingira yaliyozunguka kadhia nzima ya wachezaji hao.

Kuendelea kukaa kimya huku ligi kuu ikielekea mfundani, ni wazi kunawaweka wachezaji hao njia panda na pengine kuwavuruga kisaikolojia kwani hawajui nini kitakachowatokea.

Aidha, wakati wachezaji hao wakiendelea kuishi katika jinamizi la kutokufahamu hatima yao na Azam, uongozi wa timu hiyo nao unapata kigugumizi kuiuliza TAKUKURU sababu ya kuchelewa kutoa taarifa ya uchunguzi wake, (kama kweli imeufanya).

Yawezekana zipo klabu zinazowamezea mate wanasoka hao, hata kama watabainika wamekubali kurubuniwa ili kuifungisha Azam, na hilo watakuwa na tahadhari nalo mbele.

Lakini je, watawapata vipi bila kwanza kuzungumza na Azam ambayo haifichi ukweli kwamba nyota hao ni muhimu pia kwa klabu hiyo, licha ya kuwatia komeo na kuwapa kisogo ili kusubiri ripoti ya TAKUKURU, ambayo imekuwa bubu?
    
Cha muhimu katika sakata hili, ni kwa TAKUKURU kuharakisha uchunguzi wake, ili Azam ipate pa kuanzia katika kuwashughulikia wachezaji hao, pamoja nao kupumua kutokana na tuhuma zinazowakabili.

Kuendelea kuchelewesha ripoti, kunachangia kuwashusha kiwango, na kuwafungia milango ya riziki hasa ikizingatiwa kuwa soka ndio ajira waliyochagua kuwaendeshea maisha yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.