Habari za Punde

Balozi Seif kuzinduwa kampeni za CCM uchaguzi mdogo Chambani

Na Othman Khamis Ame, OMPR
 
 
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi kesho anatarajiwa kuzindua rasmi Kampeni za Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Chambani Mkoa wa Kusini Pemba kupitia Chama hicho kwa nafasi ya Kiti cha Ubunge.
 
Uchaguzi huo mdogo wa Jimbo la Chambani umekuja kufuatia aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Marehemu Salim Hemed Khamis kufariki dunia kutokana na maradhi ya moyo mnamo Tarehe 26 Machi Mwaka huu.
 
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar atahutubia Wanachama wa CCM, Wapenzi na Wananchi wa Jimbo hilo katika Mkutano wa hadhara utakaofanyikia katika uwanja wa Michezo wa Ukutini Sokoni kwenye Kijiji cha Ukutini.
 
Kampeni hizo za uchaguzi zitakazochukua takriban siku kumi na Tatu zinamalizika tarehe 15 ambapo uchaguzi huo mdogo unatarajiwa kufanyika tarehe 16 Juni Mwaka huu.
 
Vyama Vinne vimethibitisha kusimamisha wagombea wake kwenye Uchaguzi huo ambao ni Ndugu Mattar Sarhan Said wa Chama cha Mapinduzi { CCM }, Ndugu Yussuf Salim Hussein wa Chama cha Wananchi { CUF }, Ndugu Said Miraji wa Chama cha ADC na Bibi Siti Ussi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo { Chadema }.
 
Chama cha Mapinduzi kimemteua Balozi Seif Ali Iddi kuzindua Kampeni hizo wakati ufungaji wa Kampeni hizo kwa chama cha Mapinduzi utafanywa na Rais mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.