1. Mheshimiwa Spika,
naomba kutoa hoja kwamba Baraza lako Tukufu likae kama Kamati kwa madhumuni ya
kupokea, kujadili na hatimae kuidhinisha makadirio ya mapato na matumizi ya
fedha ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (ORMBLM) kwa mwaka wa
fedha 2013/2014.
2. Mheshimiwa Spika,
naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha
kuwa wazima wa afya na hivyo kutekeleza majukumu yetu yakiwemo ya kustawisha
maisha ya jamii ya Wazanzibari.
3. Mheshimiwa Spika,
naomba pia kutumia nafasi hii kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa umahiri wake katika
kuiongoza nchi yetu. Chini ya uongozi wake, Serikali imeendelea kutekeleza
Mipango Mikuu ya Kitaifa ikiwemo MKUZA II na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
2010-2015, sambamba na ahadi alizozitoa
kwa wananchi katika nyakati tofauti na hasa wakati wa ziara zake Mikoani. Utekelezaji wa mipango hiyo, imesaidia
Serikali kutoa huduma muhimu kwa jamii na kuongeza imani ya wananchi kwa
Serikali yao.
4. Mheshimiwa Spika, nakupongeza
wewe binafsi na Naibu wako kwa kuendelea kuliongoza Baraza letu Tukufu kwa
mujibu wa kanuni na taratibu tulizojiwekea. Uvumilivu wako umekuwa ni mfano
katika kuimarisha demokrasia ndani ya Baraza hili. Hata hivyo, uvumilivu huo
haujawa kikwazo kwako katika kufikia maamuzi sahihi. Aidha, ninawapongeza Naibu
Spika na Waheshimiwa Wenyeviti wa Baraza ambao wanakusaidia kuliendesha Baraza
hili. Ninawashukuru pia Waheshimiwa Wawakilishi wote kwa ushirikiano mzuri
wanaonipa katika kutekeleza majukumu yangu ya kila siku. Hii ni Ofisi inayowajumuisha
na kuwaunganisha jamii na wananchi wote, hivyo mashirikiano makubwa kati yenu
Waheshimiwa Wawakilishi na Ofisi hii ni suala la msingi sana.
5. Mheshimiwa Spika, nampongeza
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia Ofisi za
Viongozi Wakuu, Mheshimiwa Hamza Hassan Juma, Mwakilishi wa kuchaguliwa wa wananchi
wa Jimbo la Kwamtipura ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wenyeviti. Nampongeza sana
Mheshimiwa Hamza kwa kuchaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Kamati hii. Naamini
umahiri wake katika kuiongoza Kamati hii katika kipindi kilichopita ndio kigezo
kikubwa kilichowafanya Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati anayoiongoza kumchagua
tena kwa kipindi cha pili mfululizo. Aidha, napenda kuchukua fursa hii
kuwapongeza Waheshimiwa Wajumbe wote walioteuliwa kuingia kwenye Kamati hii,
nawaahidi kwamba mimi binafsi pamoja na watendaji wenzangu wote tutaendelea
kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwao kwa kipindi chote cha utendaji wa
majukumu yetu.
6. Mheshimiwa Spika, kwa
namna ya kipekee naomba niwapongeze Wajumbe wote wa Kamati iliyopita kwa
ushirikiano waliouonesha na utekelezaji mzuri wa kazi zao. Mafanikio ya Ofisi
yangu yametokana zaidi na miongozo na ushauri wao waliokuwa wakitupatia mara
kwa mara. Naamini kwa wale Wajumbe ambao hawajarejea katika Kamati hii, kwa
kutumia uzoefu walioupata katika kipindi cha miaka miwili na nusu, wataendelea
kutoa mchango wao mkubwa katika kufanikisha ufanisi wa utendaji wa Ofisi ya
Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Nitakuwa sijatenda haki kama
sitompongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Hesabu za Serikali Mheshimiwa
Omar Ali Shehe Mwakilishi wa Jimbo la Chake Chake kwa kuchaguliwa tena
kuiongoza Kamati hiyo na pia nawapongeza Waheshimiwa Wajumbe wote wa Kamati
hii.
7. Mheshimiwa Spika,
siku za hivi karibuni kumejitokeza wimbi kubwa la baadhi ya wananchi nchini
mwetu kutotii Sheria za nchi. Watu wengine wamefikia kuhatarisha usalama na
amani ya nchi, kuwadhuru wengine na hata kufikia kuuwawa. Hali hii si ya
kawaida nchini mwetu na ni wajibu wetu sote kuvipiga vita vitendo vyote vya kihalifu.
Vile vile, ni wajibu wetu sote kulinda amani na usalama wa nchi yetu. Uzoefu wa
nchi nyingi umeonesha kwamba amani ikipotea si rahisi kuirejesha tena kwa
haraka lakini baya zaidi ni matokeo na hasara zinazoambatana na matokeo ya
mifarakano.
8. Mheshimiwa Spika,
kabla sijamaliza salamu zangu za pongezi naomba kuchukua fursa hii kumpongeza
kwa dhati Mwakilishi wa Jimbo la Bububu Mheshimiwa Hussein Ibrahim Makungu
(Bhaa) kwa kuchaguliwa na wananchi wa Jimbo hili kupitia Chama Cha Mapinduzi.
Kuchaguliwa kwake kunaonesha matumaini waliyonayo wananchi wa Jimbo hilo kwake
katika kuwaletea maendeleo.
B. SHABAHA YA OFISI
YA RAIS NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI
9. Mheshimiwa Spika, Shabaha
kuu ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ni:-
(i)
Kudumisha Amani, Ulinzi
na Usalama
(ii)
Kuwafanya vijana wawe
na maadili mema na mtazamo wa kujiajiri wenyewe
(iii)
Kustawisha haki za Wanafunzi
waliohalifu Sheria
(iv)
Kutoa Huduma bora kwa
Jamii
(v)
Kuimarika kwa Maendeleo
ya Zanzibar
C. MWELEKEO WA BAJETI
NA MALENGO YALIYOWEKWA KWA MWAKA WA FEDHA WA 2013/2014
10.
Mheshimiwa Spika, hotuba ya bajeti ya
Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mwaka wa fedha 2013/2014 inatoa muelekeo wa jumla wa utekelezaji wa mipango ya Idara
na Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
zikiwemo Mamlaka za Serikali za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na Idara
Maalum za SMZ. Katika hotuba hii, ili malengo na utekelezaji yaweze kuonekana vizuri
na Waheshimiwa Wajumbe nimeamua kwa makusudi kuweka viambatanisho vinavyoeleza
kwa ufasaha kwa njia ya vitabu mambo yafuatayo:-
(i)
Utekelezaji wa
Maagizo ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Yaliyotolewa Wakati wa Kuwasilisha
Bajeti ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Juni 2012,
(ii)
Utekelezaji wa Malengo
ya Bajeti ya Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2012/2013 na Malengo ya Bajeti
kwa mwaka wa fedha 2013/2014 na,
(iii)
Maelezo ya Bajeti
Inayotumia “Program Based Budget” (PBB) Kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014 Katika
Baraza la Wawakilishi.
11.
Mheshimiwa
Spika, kufuatia
uamuzi wa Serikali wa kutaka kubadilisha mfumo wa bajeti wa sasa wa “Line
Budget Item” kwenda “Program Based Budget” (PBB), Ofisi yangu imeanza
maandalizi hayo kwa kupanga shughuli zote za mwaka ujao katika programu nne.
Programu hizo ni:- Programu ya Ushirikiano wa Kikanda, Kimataifa na Wazanzibari
Wanaoishi nje ya nchi, Programu ya Uongozi na Utawala wa Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, Programu ya Mipango ya Ulinzi na Huduma za Urekebishaji na
Uwezeshaji Kiuchumi na Programu ya Usimamizi na Utawala Katika Ofisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Muundo wa PBB unaonekana katika Kiambatanisho Nambari
1.
12.
Mheshimiwa Spika, kutokana na Programu nilizozitaja hapo juu, Ofisi yangu
inaazimia kutekeleza malengo makuu matano ambayo ni kuimarisha Ulinzi na
Usalama, Kuwafanya vijana wawe na maadili mema na mtazamo wa kujiajiri wenyewe,
kuimarisha Utawala Bora na Haki za Binaadamu, kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa
mapato na ushirikishwaji wa Wazanzibari walioko nje katika maendeleo ya
Zanzibar. Kwa ufafanuzi zaidi angalia Kiambatanisho
Nambari 2.
13.
Mheshimiwa
Spika, ifikapo Januari mwakani, nchi yetu itaadhimisha Miaka 50 ya
Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ambayo yaliasisiwa na Jemedari Hayati Mzee Abeid
Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yakiwa na
lengo la kumkomboa Mzanzibari kutoka katika madhila ya Wakoloni. Mapinduzi hayo, yameiwezesha Zanzibar
kupiga hatua kubwa katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Katika kufanikisha maadhimisho hayo,
Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi imejipanga kutekeleza
shughuli mbali mbali kupitia Idara na Taasisi zake. Miongoni mwa mambo ambayo
Ofisi inatarajia kuyatekeleza ni kuandaa na kurusha hewani vipindi mbali mbali
vya TV na Redio vinavyoelezea mafanikio ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar na
kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbali mbali ya maendeleo ya
wananchi Mikoani.
14. Mheshimiwa Spika, Ofisi itafanya tathmini ya
vyanzo vya mapato vya Idara Maalum za SMZ ambayo itatoa mapendekezo ya
kuimarisha misingi ya ukusanyaji wa mapato na kuvitambua vyanzo vyote vya
mapato kwa usahihi. Aidha, Ofisi yangu inaendelea kuvifanyia
mapitio vyanzo vya mapato vya Serikali za Mitaa sambamba na kutayarisha upya
Sheria ya Serikali za Mitaa ambayo itaelekeza kwa uwazi utaratibu bora wa
ukusanyaji mapato katika Serikali za Mitaa pamoja na kuainisha vyanzo vya
mapato yake.
15. Mheshimiwa Spika,
kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais,
Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, tunakusudia kuharakisha mchakato wa
ukusanyaji wa Kodi ya Mali (Property Tax), kurasimisha kisheria ada
zinazokusanywa na Masheha na utozaji wa ada wa vitambulisho vya wageni. Kwa
hatua ya awali, Wataalamu wa Serikali za Mitaa wamefanya ziara ya kimafunzo Jijini
Dar es Salaam Wilaya ya Ilala kujifunza juu ya utaratibu bora wa ukusanyaji wa
Kodi ya Mali. Kimsingi, Halmashauri ya Wilaya ya Ilala imekubali kushirikiana
nasi na kubadilishana utaalamu katika kufanikisha zoezi hili.
16. Mheshimiwa Spika,
Serikali inaandaa utaratibu wa kuanzisha Shirika litakalosimamia Miradi ya
Idara Maalum. Aidha, Serikali inategemea kufanya marekebisho ya Sheria ya Idara
Maalum ya Kikosi cha Zimamoto na Uokozi ili kuweka ulazima kwa vyombo vya moto
vya biashara kuwa na vifaa vya kuzimia moto na kufanyiwa ukaguzi na Kikosi cha
Zimamoto na Uokozi. Azma hii
itakapoanza kutekelezwa, inakusudia kuongeza usalama wa kujikinga na majanga ya
moto.
17. Mheshimiwa Spika, Mikoa itatoa kipaumbele katika kutumia ulinzi
shirikishi ili kuhakikisha kuwa uhalifu unapungua katika mitaa na vijiji.
Aidha, Serikali inakusudia kuweka mfumo maalum wa kamera za ulinzi (CCTV) sambamba
na kuweka taa za kuongozea gari katika baadhi ya barabara. Kwa hatua za mwanzo,
maeneo ya Malindi, Mkunazini na Kwamchina Mwanzo yatashughulikiwa. Mpango huu
utakuwa chini ya Wizara ya Mawasiliano na Miundombinu kwa kushirikiana na Ofisi
ya Mkoa wa Mjini Magharibi.
18. Mheshimiwa Spika, Ofisi
ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi itaendesha utafiti unaokusudia kuangalia kwa umakini majukumu ya Sheha
katika mfumo wa mageuzi ya Serikali za Mitaa. Hii itasaidia katika zoezi la
kupanga majukumu ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa katika muundo mpya wa
Serikali ambao unalenga kupunguza baadhi ya madaraka kutoka Serikali Kuu kwenda
kwa wananchi (Decentralization by Devolution) ili kurahisisha utoaji wa huduma
kwa jamii.
19. Mheshimiwa Spika, utendaji
kazi katika ngazi za Mikoa na Wilaya nao utaimarishwa ili kuweza kutoa huduma
bora kwa jamii, azma hiyo inaenda sambamba na uwepo wa vitendea kazi katika
Taasisi hizo. Jumla ya gari kumi na moja zitanunuliwa katika mwaka wa fedha wa
2013/2014, gari hizo zitasaidia sana katika kazi za usimamizi na ufuatiliaji wa
shughuli mbali mbali zinazotekelezwa katika ngazi za Wilaya na Mikoa. Aidha,
Ofisi inaazimia kuwawekea mazingira bora ya makaazi Viongozi wa Mikoa na Wilaya
kwa kuanza ujenzi na kuzifanyia matengenezo makubwa nyumba wanazoishi. Jumla ya
TZS. 458.7 milioni zimetengwa kwa kazi hiyo ya ujenzi na matengenezo ya nyumba
za Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Ofisi zao.
20. Mheshimiwa Spika,
kwa muda mrefu sasa suala la kuwa na eneo la kudumu la kutupia taka limekuwa ni
tatizo kubwa. Napenda kuliarifu Baraza lako Tukufu kuwa hivi sasa Serikali imo
katika hatua za mwisho za kukabidhiwa eneo la kudumu la kutupia taka lilioko
Kibele Wilaya ya Kati ambalo lina ukubwa wa hekta 15. Hatua za kupimwa na
kupatiwa hatimiliki kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na
Nishati zinaendelea vizuri. Kupatikana eneo hilo kutatatuwa tatizo sugu la
kukosekana eneo la kudumu la kutupa taka zinazozalishwa katika Manispaa ya
Zanzibar na maeneo jirani.
21. Mheshimiwa Spika, Ofisi
ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi imekuwa ikiendelea na juhudi za kuimarisha usafi katika Manispaa
ya Zanzibar ambapo utaratibu maalum utaandaliwa wa kusafisha Mji wakati wa usiku ambao utatoa wasaa
mzuri wa wasafishaji kuweza kuusafisha Mji kwa urahisi na kwa utulivu mkubwa. Zoezi
hili litakuwa rahisi baada ya kupatikana kwa taa katika barabara zetu. Baraza
la Manispaa litaendelea na utaratibu wa kuwaondoa watu wanaofanya biashara kiholela
katika maeneo yasiyoruhusiwa, pia kutenga maeneo kwa ajili ya wafanyabiashara
wadogo wadogo.
22.
Mheshimiwa Spika, baada ya kuonesha mafanikio makubwa ya mradi wa majaribio wa uwekaji wa taa za barabarani wenye kutumia
nguvu za jua ambao ni ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na mazungumzo na Serikali ya Jamhuri
ya Watu ya China kwa kuanza awamu ya pili ya Mradi huu ambao utahusisha
barabara ya Kiembe Samaki hadi Mnazi Mmoja, Kiembe Samaki hadi Mwanakwerekwe,
Amani hadi Mtoni na Mtoni hadi Malindi. Aidha, barabara za Mji wa Chake Chake nazo
zimeingizwa katika mpango huu.
23. Mheshimiwa Spika, matayarisho
ya utekelezaji wa mradi wa Mpango wa Kuimarisha Huduma za Miji Zanzibar
(Zanzibar Urban Service Program – ZUSP), awamu ya kwanza (Hatua ya maandalizi) imefikia
asilimia 97. Katika awamu hiyo, jumla ya Washauri Elekezi wanane wametafutwa
ambao watashiriki katika utekelezaji wa kazi mbali mbali zilizopangwa kufanyika
katika maeneo ya Manispaa ya Mji wa Zanzibar na Mabaraza ya Miji ya Pemba (maelezo
ya kina yapo katika kiambatanisho nambari 14).
24. Mheshimiwa Spika, awamu ya pili ya
mradi wa ZUSP (Hatua ya utekelezaji) imefikia asilimia 30 inayojumuisha
shughuli za ujenzi na upatikanaji wa vifaa imeanza kutekelezwa kwa kuzingatia
sehemu kuu tatu ambazo ni kupatikana kwa Washauri Elekezi wa Mradi (Consultancy
Services), shughuli za ukarabati na ujenzi wa miundombinu (Physical Works) na
ununuzi wa vifaa. Miongoni mwa vifaa vilivyonunuliwa hadi sasa ni gari
tano aina ya ‘Double Cabin’ za Wakuu wa Idara za Baraza la Manispaa na gari nne
za Mabaraza ya Miji Pemba pamoja na Idara ya Uratibu Pemba, vespa 25, pikipiki
saba, magari matatu ya kuchukulia vikapu
vya taka kwa Mabaraza ya Miji Pemba, gari moja ya Idara ya Mipango Miji, gari
moja ya kuchukulia maji machafu ya Mabaraza ya Miji Pemba na vitendea kazi
vikiwemo kompyuta, samani, printer, projector na scanner. Jumla ya programu
tano zitaanza kutekelezwa katika mwaka unaokuja baada ya taratibu za mikataba
na upatikanaji wa Wakandarasi kukamilika.
25. Mheshimiwa Spika, Programu zinazotarajiwa
kutekelezwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa msingi wa maji ya mvua katika
mitaa ya Sebleni na Ziwa la Kwa-Binti Hamrani ambao utekelezaji wake utaanza
mwezi Januari 2014. Programu ya uwekaji taa za barabarani katika maeneo ya
Shangani, Mkunazini, Kiponda na Amani – Kwabiziredi, utekelezaji wake utaanza
mwezi Oktoba 2013. Ukarabati wa jengo la Ofisi Kuu ya Baraza la Manispaa
Darajani na ukarabati wa Karakana ya Saateni, utekelezaji wake utaanza mwezi
Agosti 2013. Programu ya kuongeza uwezo wa Baraza la Manispaa itaanza mwezi
Agosti 2013. Aidha, Programu ya uendelezaji wa Mpango Mkuu wa Mji inatarajiwa
kukamilika katika miezi 18 ijayo.
26. Mheshimiwa
Spika, katika kuimarisha miundombinu
ya kuzima moto katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume, utaratibu
wa kupata eneo jengine kwa ajili ya shughuli za kituo cha Kikosi cha Zimamoto
umekamilika ambapo kwa sasa eneo jipya limeshapatikana na michoro ya jengo la
kituo hicho imeshatayarishwa. Aidha, katika kukabiliana na tatizo la uhaba na
uchakavu wa vifaa vya kuzimia moto, Kikosi cha Zimamoto na Uokozi kimetiliana
saini mkataba na Kampuni ya NN Engeneering ya nchini Uholanzi kwa ajili ya
ununuzi wa magari manne ya Zimamoto na vifaa mbali mbali vya uokozi vyenye
thamani ya EURO 2,054,852.
27.
Mheshimiwa Spika, mbali na juhudi zinazochukuliwa kuwahamasisha
Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi kuchangia maendeleo katika sekta za Kijamii
na Kiuchumi, bado juhudi hizi zinakabiliwa na changamoto mbali mbali. Miongoni
mwa Changamoto hizo ni: Kutokuwepo kwa muongozo wa uratibu wa shughuli za
maendeleo zinazofanywa na Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi, kutokuwepo kwa
mfumo maalum unaoratibu utumaji wa fedha kutoka nje na kutokuwepo kwa mfumo
unaoratibu utumiaji mzuri wa rasilimali walizonazo Wazanzibari wanaoishi nje ya
nchi ikiwemo fedha, elimu, utaalamu na teknolojia. Katika kutatua changamoto
zilizotajwa na nyengine, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi inaandaa
Sera ya Diaspora ambayo itatoa miongozo na
mikakati itakayowashajihisha Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi kushiriki katika
mipango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Zanzibar. Sera hiyo ya Diaspora
inatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha wa 2013/2014.
28.
Mheshimiwa
Spika, itakumbukwa kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar iliunda Kamati ya kuchunguza uendeshaji, usimamizi na
faida zinazopatikana kutoka katika Mradi wa Shamba la Mfano la Pamoja
linaloendeshwa kwa ubia kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali
ya Misri. Tayari ripoti ya uchunguzi imetolewa ambapo imeonesha changamoto
mbali mbali zilizopo katika mradi huo na imetoa mapendekezo juu ya namna ya
kukabiliana na changamoto hizo. Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi tayari imeshaanza kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti
hiyo ambayo yameoneshwa katika Kiambatanisho Nambari 3. Vile vile, Baraza lako Tukufu liliunda Kamati Teule ya Kuchunguza
Utendaji wa Baraza la Manispaa Zanzibar. Naomba kukujuilisha rasmi kwamba
Serikali imeipokea ripoti ya Kamati hiyo na inaendelea kuifanyia kazi na
itaiwasilisha rasmi taarifa ya utekelezaji katika kikao kijacho cha Baraza la
Wawakilishi.
29. Mheshimiwa
Spika, Ofisi
ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014, itatekeleza mradi
makhsusi wa Ukarabati
wa Ikulu Kuu Zanzibar. Jengo hili kwa sasa halipo katika hali ya kuridhisha
hasa ukitilia maanani ni jengo lenye umri wa miaka 108 lililojengwa katika
mwaka 1905. Kazi ya ujenzi wa kuzuia mmong’onyoko nyuma ya Ikulu ndogo ya
Mkoani nayo itafanyika sambamba na ujenzi na matengenezo ya nyumba za mapumziko
za Micheweni na Chwaka. Aidha, Ofisi itaendelea kutekeleza miradi saba ambayo
inatekelezwa katika mwaka huu wa 2012/2013. Pia, itatekeleza mradi wa Mpango wa
Kuimarisha Huduma za Miji Zanzibar na “Capacity
for Reform Implementation Management Program” ambayo kiutawala inasimamiwa na
Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo.
30.
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kupitia Halmashauri za Wilaya, Mabaraza ya Miji na Baraza
la Manispaa imejidhatiti katika suala zima la kuimarisha masoko yetu. Tayari soko la Mombasa limefunguliwa upya, halikadhalika na soko
la Qatar Chake Chake Pemba. Serikali inajitahidi sana kuongeza huduma za masoko
kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya soko kwa wananchi. Pia, Serikali
inazingatia kubadili mwenendo mzima wa uendeshaji wa masoko kwa kuongeza muda
wa kazi wa masoko yote baada ya kubainika kwamba sehemu kubwa ya wafanyakazi
wanafanya manunuzi ya mahitaji yao nyakati za jioni.
D. MAPITIO YA
UTEKELEZAJI WA MPANGO WA BAJETI 2012/2013 NA MALENGO KWA MWAKA 2013/2014
31. Mheshimiwa Spika, baada
ya utangulizi wa hapo juu, sasa naomba kueleza utekelezaji wa malengo ya bajeti
ya mwaka 2012/2013 pamoja na mwelekeo wa bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2014 kwa
Idara na Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi.
OFISI
YA FARAGHA YA RAIS
32. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Faragha ya Rais imeendelea kuratibu shughuli za kila siku za
Mheshimiwa Rais, kufuatilia ahadi na maagizo anayoyatoa kwa wananchi na Taasisi
mbali mbali, kusimamia upatikanaji wa huduma za kila siku za Mheshimiwa Rais,
pamoja na kuweka kumbukumbu za mazungumzo ya Mheshimiwa Rais na viongozi mbali
mbali wakiwemo Mabalozi. Kadhalika, Ofisi imeweza kuratibu safari za ndani na
nje za Mheshimiwa Rais na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi na vile vile kutekeleza jukumu lake la utunzaji na
ukarabati wa nyumba zote za Ikulu Unguja, Pemba, Dar es Salaam na Dodoma.
Nyumba zilizopo katika dhamana ya Ofisi hii ni Ikulu Kuu ya Mnazimmoja, Ikulu
ndogo iliyopo Kikwajuni, Ikulu ndogo iliyopo Migombani, Ikulu ndogo iliyopo
Kibweni na Ikulu ndogo iliyopo
Mkokotoni. Nyengine ni nyumba ya mapunziko ya Mazizini I, Mazizini II na
Bwefoum. Aidha, Ofisi hii ina dhamana ya
Ikulu ndogo iliopo Chake Chake na Mkoani pamoja na Nyumba ya Mapumziko ya
Micheweni. Nyengine ni Ikulu ndogo ya Laiboni Mjini Dar es Salaam, Ikulu ndogo
pamoja na nyumba ya Wageni Mjini Dodoma. Aidha, Ofisi hii imetekeleza
wajibu wake wa kuwasiliana na vyombo vya
habari na kutoa taarifa sahihi za Mheshimiwa Rais kwa wakati unaotakiwa kwa lengo la
kuwafikishia wananchi na wahusika wote. Vile vile, Ofisi hii inajukumu la
kuwaendeleza wafanyakazi wake kwa kuwapatia fursa za masomo katika vyuo na
Taasisi mbali mbali ndani na nje ya nchi.
33. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, Ofisi ya Faragha ilitengewa jumla ya TZS
1,908.3 milioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwemo mishahara na hadi
kufikia Machi 2013, Ofisi hii iliingiziwa TZS 1,265.0 milioni sawa na asilimia
66.3 ya makadirio.
34. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Faragha imetekeleza vizuri jukumu lake la kutoa huduma kwa Mheshimiwa Rais na wageni rasmi
mbali mbali. Katika kipindi hiki, Mheshimiwa Rais amekutana na kufanya
mazungumzo na mabalozi na viongozi kadhaa kutoka nchi mbali mbali kama
inavyoonekana katika Kiambatanisho Nambari 4. Mazungumzo hayo yalilenga
kuimarisha urafiki kati ya Zanzibar na nchi hizo, pia kuongeza juhudi za Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutafuta maendeleo ya haraka kwa wananchi wake
na kwa jumla yalijumuisha sekta zote za
uchumi, siasa na ustawi wa jamii. Wengi wa wageni hao, wamevutiwa sana na
jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukuza
uchumi na kuimarisha umoja, amani, utulivu na mshikamano. Kutokana na juhudi
hizo viongozi hao wamekuwa wakiunga mkono na kutoa ushirikiano wao katika juhudi za kuleta maendeleo kwa njia
mbali mbali ikiwemo kuhamasisha wawekezaji kutoka katika nchi zao kuja kuwekeza
Zanzibar.
35. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha unaomalizika, Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein,
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amefanya ziara mbili
katika nchi za Mashariki ya Mbali zenye mafanikio makubwa. Katika mwezi wa
Novemba, 2012 alitembelea Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam na hivi karibuni,
katika mwezi wa Mei, 2013 alitembelea
Jamhuri ya Watu wa China. Katika ziara yake ya Vietnam, Mheshimiwa Dk. Ali
Mohamed Shein alikutana na Mheshimiwa Truong Tan Sang, Rais wa Jamhuri ya
Kisoshalisti ya Vietnam, Mheshimiwa Bibi Nguyen Thi Doan, Makamu wa Rais wa
nchi hiyo na Mheshimiwa Nguyen Tan Dung,
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam pamoja na viongozi wa Taasisi
mbali mbali nchini humo. Ziara hiyo ilikuwa ni ya mafanikio kwani ujumbe wa
Zanzibar ulijifunza namna ambavyo nchi ya Vietnam imeweza kupiga hatua kubwa ya
kujiletea maendeleo katika muda mfupi ikiwemo kuzalisha mpunga kwa wingi. Vile
vile, Zanzibar ilifaidika kwa kuona na kufikia maelewano ya kushirikiana katika
shughuli mbali mbali za kiuchumi katika sekta ya kilimo hasa uimarishaji wa
ukulima wa mpunga kwa njia za kisasa na kukubaliana na Wizara ya Kilimo na
Maendeleo ya Vijijini ya Vietnam iwe na ushirikiano wa karibu na Wizara ya
Kilimo na Mali Asili ya Zanzibar. Aidha, wataalam wa kilimo na Uvuvi wa Vietnam
watembelee Zanzibar na kutoa ushauri wao wa kitaalamu. Maeneo mengine ambayo
Vietnam itashirikiana na Zanzibar ni katika sekta ya Uwezeshaji Wananchi
Kiuchumi ambapo wananchi watashajihishwa kufuga samaki na mazao ya baharini
kupitia vikundi vya ushirika pamoja na kunyanyua shughuli za akina mama
wajasiriamali. Ujumbe wa Zanzibar
ulitumia ziara hiyo kuitangaza Zanzibar kwa wawekezaji wa nchi hiyo.
36. Mheshimiwa Spika, katika ziara yake katika Jamhuri ya Watu wa China,
Mheshimiwa Rais alipata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Watu wa
China Mheshimiwa Xi Jinping kwa mara ya pili ndani ya mwaka huu, baada ya
kukutana nae mjini Dar es Salaam mnamo mwezi wa Machi, mwaka huu. Katika
mazungumzo yao yaliyotawaliwa na hisia
za kirafiki na kindugu, viongozi hao walizungumzia na kukubaliana juu ya uimarishaji wa uhusiano
wa kihistoria uliodumu tokea mwaka 1964, ulioanzishwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Marehemu
Mzee Abeid Amani Karume na Mwenyekiti Mao TseTung. Vile vile, Jamhuri ya Watu
wa China imesisitiza kuendeleza urafiki wake na Zanzibar pamoja na kukuza
ushirikiano katika nyanja za kiuchumi na kijamii zikiwemo sekta za kilimo, uvuvi,
afya, mafunzo mbali mbali, utafiti na utalii. Aidha, miradi kadhaa ya maendeleo
illizungumzwa. Vile vile, Mheshimiwa Rais alitumia fursa hiyo kuelezea kwamba
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliyo katika Muundo wa Serikali ya Umoja wa
Kitaifa ina dhamira ya kweli ya kuwahudumia na kuwaletea maendeleo wananchi
wake ambao wanaishi kwa amani na utulivu
37. Mheshimiwa Spika, Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais alikutana na kufanya mazungumzo na
Mheshimiwa Li Yuamchao Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China. Pia,
Mheshimiwa Rais, alipata heshima kubwa ya kuwa miongoni mwa viongozi wa nchi
nne, Singapore, Fiji, Sri Lanka na Zanzibar katika ufunguzi rasmi wa maonesho
ya kimataifa ya biashara na huduma mjini Beijing, wakiwa pamoja na Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa Li Keqiang. Viongozi wengine ambao
Mheshimiwa Rais alipata fursa ya kukutana na kuzungumza nao ni pamoja na Naibu
Waziri wa Biashara ambapo Wizara yake ilitia saini makubaliano ya ujenzi wa
kitengo cha wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Mnazi Mmoja na utoaji wa
mafunzo kwa maofisa wa habari pamoja na maofisa wa bajeti wa Zanzibar.
Makubaliano mengine yaliyotiwa saini ni ushirikiano katika Sayansi na Teknolojia
ya Baharini ikiwemo utafiti wa kisayansi katika bahari. Vile vile, alikutana na
Kiongozi wa Mji wa Nanjing katika jimbo la Jiangsu Mheshimiwa Li Xueyong pamoja
na madaktari waliowahi kufanya kazi Zanzibar kwa miaka tofauti ambapo suala la
kuwapeleka wagonjwa kutoka Zanzibar
katika hospitali ya Drum Tower lilizungumzwa. Katika mazungumzo yake na
Meya wa Mji wa Xiamen katika jimbo la
Fujian, Mheshimiwa Liu Keqing ilikubalika kwamba Jimbo hilo litaleta
Zanzibar ujumbe wa Viongozi wa Jimbo na makampuni mbali mbali hivi karibuni,
kwa ajili ya hatua za uwekezaji na mashirikiano katika maeneo mbali mbali.
Aidha, Mheshimiwa Rais alikutana na viongozi wa makampuni na Taasisi mbali
mbali yakiwemo Mashirika yanayojishughulisha na ujenzi, utalii na mahoteli,
usafiri wa baharini, uvuvi, teknolojia na viwanda ambapo wote wameonesha moyo
mkubwa wa kuwekeza na kushirikiana na Zanzibar. Ujumbe wa Rais kwa upande wake,
ulitoa taaluma kwa makampuni na wawekezaji mbali mbali wa China juu ya vivutio
vya uwekezaji na utalii vilivyopo Zanzibar. Aidha, Mheshimiwa Rais alitumia
fursa ya kuwepo kwake nchini China kuzungumza na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaoishi
nchini humo na kuwaeleza juu ya hali ya
maendeleo pamoja na amani na utulivu iliyopo nchini. Aliwataka wanafunzi
wanaochukua masomo mbali mbali nchini China kusoma kwa bidii na kurejea
nyumbani kuungana na wananchi wenzao katika shughuli za maendeleo mara tu
watakapomaliza masomo yao.
38. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa ziara za ndani, Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amekuwa akiendeleza
utaratibu wa kufanya ziara za Mikoa na Wilaya
zote za Zanzibar kila mwaka kwa
lengo la kukutana na wananchi katika maeneo yao na kuwaunga mkono katika juhudi
za kuleta maendeleo. Katika kipindi hiki, Mheshimiwa Rais alifanya ziara ya
Mikoa ya Unguja na Pemba tarehe 5 hadi 21 Machi 2013, ambapo alipokea taarifa
za Mikoa hiyo na kufanya majumuisho katika kila Mkoa baada ya kumaliza ziara ya
Mkoa husika. Katika ziara hizo ambapo Mheshimiwa Rais hufuatana na viongozi
mbali mbali, wananchi hupata fursa ya kuwasilisha ana kwa ana masuala muhimu
yanayowagusa katika maisha yao ya kila siku. Aidha, ziara hizo zimekuwa zikitoa
mchango mkubwa na kuhamasisha viongozi na wananchi kushiriki kikamilifu katika
harakati za maendeleo, kuwakurubisha viongozi kwa wananchi wanaowaongoza na
katika jitihada za kufufua ari ya utamaduni wa kujitolea katika kutekeleza
mipango muhimu ya maendeleo. Katika ziara za mwaka huu miradi mbali mbali ya
kilimo, afya, maji, elimu ilikaguliwa, kuwekewa mawe ya msingi na myengine
kuzinduliwa. Juhudi za wajasiriamali ziliungwa mkono na changamoto mbali mbali
kupatiwa ufumbuzi na baadhi yake kutolewa maelekezo.
39. Mheshimiwa Spika, Katika kuimarisha maendeleo ya jamii, Ofisi imewatembelea wananchi
mbali mbali Unguja na Pemba na kufanya tathmini
juu ya mahitaji yao ya msingi kwa lengo la kuwasaidia na kuwaunga mkono
katika juhudi zao za kuleta maendeleo.
40. Mheshimiwa Spika, Ofisi iliendelea kuimarisha Ikulu ya Mnazi Mmoja kwa kujenga na
kukamilisha jengo jipya linalojumuisha Stoo na Ofisi. Kadhalika, Ofisi
imefanikisha ufungaji wa mashine tatu za kufulia katika Ikulu ya Migombani,
mashine tatu za vipoza hewa katika ukumbi wa Baraza la Mapinduzi na kupaka
rangi jengo la Ikulu. Kwa upande wa Ofisi ya Ikulu ndogo ya Laibon ilioko Dar
es Salaam, Ofisi imefunga mashine ya kipoza hewa, kufanya matengenezo ya vyoo
na kufanya malipo ya huduma za umeme na maji. Aidha, Ofisi imeendelea
kuimarisha huduma katika Ikulu ndogo ya Dodoma kwa kuvifanyia matengenezo
makubwa vyoo vitano pamoja na sehemu ya kufulia.
41. Mheshimiwa Spika, pamoja na utekelezaji wa mambo yaliyoainishwa, Ofisi ya Faragha ya
Rais, vile vile imetekeleza majukumu yake mengine kama ifuatavyo:-
(i)
Ofisi imeendelea kuwaendeleza
wafanyakazi wake katika kada mbali mbali. Kati ya wafanyakazi watano waliokuwa
masomoni katika mwaka wa fedha uliopita, wafanyakazi wawili wamemaliza mafunzo
yao kwa ufanisi katika ngazi ya Stashahada kwenye masomo ya Uongozi katika
Utoaji Huduma katika Chuo cha Maendeleo ya Utalii Maruhubi. Wafanyakazi wengine
wawili wanaendelea na mafunzo kama hayo katika ngazi ya Shahada na mwengine
mmoja anaendelea na mafunzo ya Stashada katika fani ya Rasilimali Watu katika
Chuo cha Utawala wa Umma, Tunguu. Aidha, Ofisi ya Faragha imewapatia nafasi za
mafunzo ya Uongozi katika Utoaji Huduma, katika ngazi ya Stashada, wafanyakazi
wengine wawili katika Chuo cha Maendeleo ya Utalii Maruhubi katika mwaka huu wa
fedha. Jumla ya madereva wawili wamemaliza mafunzo ya muda mfupi ya kuendesha
gari za viongozi na Ofisa mmoja ameshiriki katika mafunzo mafupi ya Sheria.
Vile vile, Ofisa mmoja ameshiriki mafunzo ya muda mfupi ya Uchumi na Maendeleo
ya Jamii katika Jamhuri ya Watu wa China yaliyofadhiliwa na Serikali ya nchi
hiyo.
(ii)
Matengenezo makubwa ya maktaba ya Mheshimiwa Rais yamekamilika. Hatua
inayofuata ni ununuzi wa samani pamoja na kuongeza vitabu kwa ajili ya maktaba
hiyo.
(iii) Ofisi imeendelea kuchapisha vitabu vya Hotuba
mbali mbali za Mheshimiwa Rais, pamoja na kuweka kumbukumbu za hotuba na ziara
mbali mbali za Rais katika DVD na CDs.
(iv) Ofisi imetoa huduma zinazohitajika kwa wageni
rasmi pamoja na kufanikisha sherehe mbali mbali zinazohusiana na Ofisi ya
Faragha.
42. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, Ofisi ya Faragha ya Rais
inatarajia kutekeleza malengo yafuatayo:-
(i) Kuimarisha huduma za Mheshimiwa Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
(ii) Kuimarisha
mazingira ya kazi;
(iii) Kuendelea na matengenezo madogo madogo ya majengo
ya Ikulu za Zanzibar; na
(iv) Kujenga uwezo kwa wafanyakazi sita katika ngazi ya
Stashahada na watatu ngazi ya Cheti.
43. Mheshimiwa Spika, ili Ofisi ya Faragha iweze kutekeleza malengo yake kwa ufanisi, kwa
mwaka wa fedha 2013/2014, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS. 2,197.2
milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida.
OFISI
YA BARAZA LA MAPINDUZI
44. Mheshimiwa Spika, Baraza
la Mapinduzi ndio chombo kikuu cha kumsaidia na kumshauri Mheshimiwa Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika masuala mbali mbali ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Shughuli za Baraza la Mapinduzi zinaratibiwa
na kusimamiwa na Ofisi ya Baraza la Mapinduzi chini ya Katibu wa Baraza la
Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi. Ofisi hii pia inajukumu la kuratibu na
kusimamia vikao vya Kamati mbali mbali za Baraza la Mapinduzi ikiwa ni pamoja
na Kamati ya Kitaalamu ya Makatibu Wakuu (Inter-Ministerial Technical Committee).
Aidha, Baraza la Mapinduzi limeunda Kamati mbili kutoka kwenye Wajumbe wake, Kamati
hizi zinaitwa Kamati ya Maendeleo ya Jamii na Kamati ya Fedha na Uchumi.
45. Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka wa fedha 2012/2013, Ofisi ya Baraza la Mapinduzi ilitengewa TZS. 1,362.0 milioni kwa matumizi ya kawaida na hadi
kufikia Machi 2013, Ofisi hii iliingiziwa TZS. 848.0 milioni sawa na asilimia 62.3
ya makadirio.
46. Mheshimiwa Spika, Ofisi
imeandaa semina mbili, moja kwa Masheha na Madiwani wote katika Kisiwa cha Pemba
na nyengine kwa Viongozi Wakuu wa Serikali. Semina hizo zilikuwa na lengo la
kutathmini utendaji kazi wa Serikali na kuwajuilisha Viongozi hasa katika
Mikoa, Wilaya na Shehia juu ya dhamana zao, majukumu yao ya kila siku na nini
hawapaswi kufanya. Jumla ya vikao 22 vya Baraza la Mapinduzi na 30 vya
Kamati ya Makatibu Wakuu vimefanyika. Aidha, Ofisi ya Baraza la Mapinduzi
imeratibu mikutano 35 ya pamoja kati ya Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Viongozi na watendaji wa Wizara mbali
mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kupitia vikao na mikutano hiyo
masuala mbali mbali yaliweza kujadiliwa na ushauri kutolewa.
47. Mheshimiwa Spika, Ofisi
ya Baraza la Mapinduzi pia imefanya matengenezo ya jengo la Ofisi ikiwa ni
pamoja na kukamilisha kazi ya kuezeka paa la Ofisi, matengenezo ya varanda
(corridor), vyumba vinne na kuweka samani (shelves na viti) katika ukumbi wa
mkutano unaotumika kwa mikutano ya Kamati ya Makatibu Wakuu.
48. Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka wa fedha 2013/2014, Ofisi ya Baraza la Mapinduzi, imepanga kutekeleza malengo
yafuatayo:-
(i)
Kuendelea kuandaa vikao vya kujadili Rasimu za
Sera, Sheria na Nyaraka mbali mbali zinazowasilishwa katika vikao vya Baraza la
Mapinduzi na Kamati zake;
(ii)
Kuimarisha na kuendeleza ustawi wa Ofisi na kuimarisha mazingira ya
kazi;
(iii) Kuwajengea uwezo watumishi ili waweze kutekeleza
majukumu yao ipasavyo; na
(iv) Kutunza na kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu muhimu
za Ofisi.
49. Mheshimiwa Spika, ili
Ofisi ya Baraza la Mapinduzi iweze kutekeleza malengo yake kwa ufanisi, naliomba
Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS. 1,379.0 milioni kwa ajili ya matumizi ya
kazi za kawaida.
IDARA YA MIPANGO,
SERA NA UTAFITI
50. Mheshimiwa Spika, Idara
ya Mipango, Sera na Utafiti imeendelea na jukumu lake la kuratibu na kusimamia
uandaaji wa Sera, Sheria na Mipango ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi. Aidha, Idara imeendelea na utekelezaji wa jukumu la kufanya tafiti
mbali mbali pamoja na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo.
51. Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka wa fedha 2012/2013, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti, ilitengewa TZS. 466.9
milioni kwa ajili ya utekelezaji wa kazi za kawaida na TZS. 906.0 milioni kwa
ajili ya miradi minne ya maendeleo. Hadi kufikia Machi 2013, Idara ya Mipango,
Sera na Utafiti imeingiziwa TZS. 188.0 milioni sawa na asilimia 40.3 ya
makadirio ya matumizi ya kazi za kawaida na TZS. 372.9 milioni kwa kazi za
maendeleo sawa na asilimia 41.2.
52. Mheshimiwa Spika, Idara
ya Mipango, Sera na Utafiti imeratibu mikutano mitatu ya robo mwaka kwa ajili
ya kufanya tathmini ya utekelezaji wa malengo ya bajeti, utekelezaji wa Ilani
ya Uchaguzi na uandaaji wa ripoti. Aidha, Idara imefanya mapitio ya Muongozo wa
Mpango wa Muda wa Kati wa Bajeti (MTEF) na Mipango Kazi ya Taasisi zote za Ofisi
ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Unguja na Pemba.
53. Mheshimiwa Spika, Idara
imewawezesha watumishi watatu kuhudhuria mafunzo ya muda mrefu katika Shahada
ya kwanza ya mipango ya maendeleo, Stashahada ya Teknologia ya Habari na
Mawasiliano na Shahada ya pili ya Sheria. Aidha, wafanyakazi watano wamepatiwa
mafunzo ya muda mfupi katika fani za Uchambuzi wa Bajeti na Uchumi, Sera na Udereva.
Vile vile, Idara imetoa mafunzo ya siku mbili kuhusu Usimamizi
na Tathmini ya Miradi ya Maendeleo kwa Maofisa Mipango 25 wa Taasisi za Ofisi
ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
54. Mheshimiwa Spika, Idara
imeratibu utafiti kuhusu maoni ya wananchi juu ya taarifa zinazotolewa na Idara
ya Mawasiliano - Ikulu ili kubaini mafanikio na changamoto ziliopo. Sambamba na
hilo katika kuimarisha mfumo wa takwimu wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Idara imekamilisha mchakato wa kumpata Mshauri Elekezi wa
kufanya utafiti juu ya mahitaji ya takwimu katika Ofisi ya Rais na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi. Hatua hii ya kuelewa mahitaji ya takwimu itaiwezesha
Ofisi kujua mahitaji sahihi ya takwimu zake na namna ya kukusanya na kuzitumia
takwimu hizo. Aidha, Idara imeendesha semina kwa
Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhusu Sera mpya ya Serikali za
Mitaa ya Zanzibar.
55. Mheshimiwa Spika, Idara
pia imeandaa taarifa jumuishi za utekelezaji wa malengo ya bajeti ya Ofisi ya
Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mwaka wa fedha 2012/2013 za robo
mwaka ya kwanza, ya pili na ya tatu za Taasisi zote za Ofisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Taarifa imeonesha kuwa utekelezaji kwa
ujumla ni asilimia 70. Aidha, katika kipindi hiki Idara imekiimarisha kitengo
cha kutunzia nyaraka kwa kukipatia vitendea kazi vikiwemo samani.
56. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti
imekusudia kutekeleza malengo yafuatayo:-
(i)
Kuimarisha uwezo wa Idara katika Mipango, kuandaa na kuchambua Sera,
kufanya Utafiti na shughuli za uratibu;
(ii)
Kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini;
(iii)
Kuimarisha uwezo wa watendaji wa Idara na wa Ofisi
ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
(iv)
Kuimarisha huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano; na
(v)
Kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi ili kutoa huduma bora.
57. Mheshimiwa Spika,
ili Idara ya Mipango, Sera na Utafiti iweze kutekeleza malengo yake ipasavyo,
kwa mwaka wa fedha 2013/2014, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS.
522.4 milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida na TZS. 1,250.0 milioni kwa
matumizi ya kazi za maendeleo.
IDARA YA UTUMISHI NA UENDESHAJI
58. Mheshimiwa Spika, Idara
ya Utumishi na Uendeshaji ina jukumu la kusimamia shughuli za Utawala na
Utumishi za siku hadi siku zikiwemo kusimamia Sheria na Kanuni za Utumishi kwa
watendaji pamoja na kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi, kuratibu na kusimamia
utekelezaji wa Sheria ya Manunuzi na Ugavi, kuwaendeleza wafanyakazi kielimu
pamoja na kusimamia maslahi yao.
59. Mheshimiwa Spika,
Idara ya Utumishi na Uendeshaji, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, iliidhinishiwa
TZS. 1,247.3 milioni kwa kazi za kawaida. Hadi kufikia Machi 2013, Idara hii
iliingiziwa TZS. 680.0 milioni
sawa na asilimia 54.5 ya makadirio ya matumizi ya kawaida.
60. Mheshimiwa Spika,
Idara imelipa stahili mbali mbali za wafanyakazi zikiwemo mishahara, michango
ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, likizo kwa wafanyakazi, posho la kujikimu,
gharama za safari za ndani na sare kwa wafanyakazi. Aidha, Idara imenunua vifaa
mbali mbali vya kuandikia na vifaa vya usafi. Vile vile, Idara imesimamia utekelezaji
kivitendo wa Sheria ya Manunuzi na Ugavi kwa kuendesha vikao vinane vya Bodi ya
Zabuni pamoja na vikao vya Kamati ya Ukaguzi wa Ndani.
61. Mheshimiwa Spika,
wafanyakazi wamejengewa uwezo kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu wafanyakazi
watatu katika ngazi ya Shahada ya Uzamili na wafanyakazi watano Stashahada.
Vile vile, Idara imewapatia mafunzo ya muda mfupi wafanyakazi watatu katika
fani ya Udereva, Uongozi wa Rasilimali Watu na Lugha za Alama pamoja na
kuwapatia semina wafanyakazi 80 juu ya maadili ya kazi na utunzaji wa siri za Ofisi
na Uimarishaji wa masjala za Ofisi. Sambamba na hayo, Idara imeratibu mafunzo
ya muda mrefu na mfupi kwa Wafanyakazi 207 wa Idara na Taasisi zilizo chini ya
Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Kiambatanisho Nambari 5
kinatoa ufafanuzi zaidi.
62. Mheshimiwa Spika,
katika kuyapatia hati miliki majengo ya Ikulu na nyumba za Serikali, gharama za
upimaji wa maeneo ya majengo zimelipwa kwa lengo la kuyatafutia hati miliki. Jengo
la Ikulu ya Mnazi Mmoja limeshapatiwa hati miliki na majengo yaliyobakia hati
zake zimeshafanyiwa uhakiki na zitapatikana hivi karibuni. Sambamba na hayo, Idara
imeandaa Makisio ya mishahara na Mipango ya Matumizi ya Rasilimali Watu (Norminall
Roll) pamoja na kufanya mapitio na marekebisho ya Miundo ya Utumishi (Scheme of
Service) na kuwasilishwa Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa
hatua ya kufanyiwa kazi.
63. Mheshimiwa Spika,
Idara inaendelea na kazi ya uhakiki wa mahitaji na kuandaa Mpango wa Mafunzo wa
Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambapo kazi hiyo inategemewa
kukamilika katika mwaka wa fedha 2013/2014.
64. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Idara ya Utumishi na Uendeshaji inakusudia
kutekeleza malengo yafuatayo:-
(i)
Kuongeza ufanisi wa kazi kwa kuimarisha mazingira ya utendaji kazi na
maslahi ya wafanyakazi;
(ii)
Kutekeleza Sheria ya Manunuzi kwa kuendesha vikao 12 vya Bodi ya Zabuni na
vikao vinne vya Kamati ya Ukaguzi wa ndani;
(iii)
Kuwajengea uwezo wafanyakazi kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu na mfupi
ndani na nje ya nchi;
(iv)
Kuendeleza uhusiano
wa kimichezo kwa wafanyakazi;
(v)
Kuratibu masuala mtambuka
pamoja na kupima afya za wafanyakazi ili kubaini mienendo ya hali zao na
kupatiwa ushauri wa kinga na matibabu kwa wakati;
(vi)
Kuandaa makisio ya mishahara
na kupanga matumizi ya Rasilimali Watu ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi; na
(vii) Kusimamia
utendaji na uwajibikaji wa wafanyakazi.
65. Mheshimiwa Spika, ili Idara ya Utumishi na Uendeshaji iweze kutekeleza
majukumu yake kwa ufanisi, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, naliomba Baraza lako
Tukufu liidhinishe TZS. 1,274.6 milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida.
IDARA YA MAWASILIANO
- IKULU
66. Mheshimiwa Spika, Idara ya Mawasiliano - Ikulu imeendelea na utekelezaji wa majukumu yake
ya msingi ya kupokea na kutoa taarifa za
Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuhusu
utekelezaji wa Sera na Mipango ya Serikali. Aidha, Idara ya Mawasiliano – Ikulu
imepewa jukumu la kuhakikisha kuwa taarifa za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi zinazotolewa kwa wananchi ni sahihi na katika wakati
muafaka.
67. Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka wa fedha 2012/2013, Idara ya Mawasiliano – Ikulu ilitengewa jumla ya TZS.
174.9 milioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na hadi kufikia Machi 2013, iliingiziwa TZS. 132.0 milioni sawa na
asilimia 75.5 ya makadirio ya matumizi.
68.
Mheshimiwa
Spika, Idara ya Mawasiliano – Ikulu
imeendelea kuimarisha mawasiliano baina ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Taasisi za Serikali na wananchi na imeandaa na kurusha
hewani vipindi 44 vya Televisheni katika Shirika la Utangazaji la Zanzibar
(ZBC). Vipindi hivyo vilihusu ziara za Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ndani na nje ya nchi na hotuba za Mheshimiwa
Rais. Aidha, Idara imeandaa na kurusha hewani vipindi 17 vya Redio kupitia
Shirika la Utangazaji la Zanzibar, vipindi ambavyo vilizungumzia masuala ya
utalii kwa wote, uwezeshaji wananchi kiuchumi na uwajibikaji kwa wafanyakazi. Orodha
ya vipindi vilivyorushwa hewani inaoneshwa katika Viambatanisho Nambari 6 na 7.
69. Mheshimiwa Spika, Idara
pia, imeandaa na kuchapisha nakala 3,000 za kalenda zenye kuonyesha shughuli
zinazotekelezwa na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi katika nyanja za kijamii, kiuchumi na kidiplomasia. Vile vile, Idara
iliandaa na kuchapisha matoleo matatu ya Jarida la ‘IKULU’ lenye kuonyesha
shughuli mbali mbali za maendeleo pamoja na utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Rais
alizozitoa kwa wananchi katika nyakati tofauti.
70. Mheshimiwa Spika,
Idara imeendelea kuwajengea uwezo wa kiutendaji watumishi wake ili kuimarisha
ueledi katika fani ya mawasiliano. Katika kufanikisha azma hii, Idara imelipia
gharama za mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa watumishi watatu katika fani za Ukatibu
Muhtasi, Matumizi ya Kompyuta na namna ya kuandaa majarida.
71. Mheshimiwa Spika,
kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Idara ya Mawasiliano – Ikulu imepanga kutekeleza
malengo yafuatayo:-
(i) Kuendeleza taswira nzuri ya Mheshimiwa Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
(ii) Kuimarisha
mazingira ya kazi katika Idara ili iweze kutoa huduma nzuri; na
(iii) Kuwajengea
uwezo wafanyakazi wa Idara ya Mawasiliano.
72. Mheshimiwa Spika,
ili Idara ya Mawasiliano – Ikulu iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo, kwa
mwaka wa fedha 2013/2014, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS. 242.7
milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida.
IDARA YA
USHIRIKIANO WA KIMATAIFA NA URATIBU WA WAZANZIBARI WANAOISHI NJE YA NCHI
73. Mheshimiwa Spika,
Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Wazanzibari Wanaoishi Nje ya
Nchi imeendelea na majukumu yake ya kuratibu ushiriki wa Zanzibar katika
mikutano mbali mbali ya Kikanda na Kimataifa na kuhakikisha kwamba Zanzibar
inafaidika na ushiriki huo na fursa zinazotokana na mikutano hiyo. Aidha, Idara
ina jukumu la kuwatafuta, kuwatambua na kuwashajihisha Wazanzibari wanaoishi
nje ya nchi (Diaspora) ili kuchangia katika kujenga uchumi mzuri na kuleta maendeleo
ya kiuchumi na kijamii Zanzibar.
74. Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka wa fedha 2012/2013, Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa
Wazanzibari Wanaoishi Nje ya Nchi, ilitengewa TZS. 884.0 milioni kwa ajili ya matumizi
ya kazi za kawaida na hadi kufikia Machi 2013, iliingiziwa TZS. 364.8 milioni
sawa na asilimia 41.3 ya makadirio ya matumizi.
75.
Mheshimiwa
Spika, Zanzibar imeshiriki kikamilifu katika
mikutano ya Kikanda ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika
(SADC) na Mkutano wa Nchi Zinazozungukwa na Bahari ya Hindi (IOR). Idara kwa
kushirikiana na Wizara za SMZ inafuatilia maamuzi ya vikao hivyo kwa manufaa ya
Zanzibar. Wizara ya Mifugo na Uvuvi tayari inafuatilia miradi ya uvuvi
inayotokana na makubaliano ya mkutano uliofanyika India mwezi Novemba 2012. Aidha,
Ofisi inaendelea kufuatilia hatua za mwisho za kuanzisha Taasisi ya Kiswahili
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wamesharidhia
kuanzishwa kwa Taasisi hiyo hapa Zanzibar na kazi iliyobaki sasa ni
utayarishaji wa makubaliano na Makao Makuu ya Jumuiya.
76. Mheshimiwa Spika,
Idara pia, ilishiriki katika mkutano wa Diaspora uliofanyika nchini Oman
kufuatia ziara ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.
Jakaya Mrisho Kikwete. Katika mkutano huo ajenda kuu ilikua ni kujadili namna
ambavyo Wazanzibari wanaoishi Oman na nchi za Mashariki ya Kati wanavyoweza
kushiriki na kuchangia maendeleo ya Zanzibar. Matokeo ya mikutano hiyo
imepelekea Benki ya Watu wa Zanzibar kuingia mkataba na Benki ya Muscat
kufungua akaunti maalum ambayo itawezesha Diaspora hao kutuma fedha zao
Zanzibar bila ya usumbufu kupitia akaunti hiyo.
77.
Mheshimiwa
Spika, matayarisho ya Sera ya Diaspora
yameanza baada ya kupatikana Mshauri Elekezi, pamoja na hatua hiyo muhimu,
Shirika la Uhamiaji la Kimataifa (IOM) limeahidi kuipitia Rasimu ya Sera hiyo
kila baada ya hatua na kutoa ushauri wa kitaalamu. Kazi hiyo inatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha
2013/2014.
78. Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, Idara imeendelea kuwajengea uwezo
wa kiutendaji watumishi wawili, mmoja katika ngazi ya Shahada ya Uzamili
(Uhasibu) na mwengine katika Stashahada (Utawala wa Umma).
79. Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka wa fedha 2013/2014, Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa
Wazanzibari Wanaoishi Nje ya Nchi imepanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
(i) Kuhakikisha kuwa Zanzibar inashiriki kikamilifu katika
mikutano mbali mbali ya Kikanda na Kimataifa;
(ii) Kuwashajihisha Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi kuchangia
katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii;
(iii) Kuwajengea uwezo Wazanzibari katika sekta mbali mbali
kupitia wataalamu wa Kizanzibari wanaoishi nje ya nchi (Diaspora);
(iv) Kuitangaza
dhana ya Diaspora ndani na nje ya nchi;
(v) Kuandaa
Programu maalum itakayorahisisha upatikanaji wa taarifa kwa Diaspora kuhusu
maendeleo yanayopatikana katika nchi yao;
(vi) Kuandaa
programu maalum ya mafunzo ya kuongeza uwezo wa wataalamu wa Serikali katika
majadiliano ya Kikanda; na
(vii) Kuwaongezea
uwezo wafanyakazi kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na mrefu.
80. Mheshimiwa Spika, ili
Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Wazanzibari Wanaoishi Nje ya
Nchi iweze kutekeleza malengo yake kwa ufanisi, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, naliomba
Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS. 873.0 milioni kwa matumizi ya kawaida.
KITENGO CHA USALAMA
WA SERIKALI (GSO) ZANZIBAR
81. Mheshimiwa Spika, Kitengo
cha Usalama wa Serikali kimeendelea kufanya kazi zake kama kilivyopangiwa kwa
mujibu wa Sheria. Kwa mwaka wa fedha 2012/2013, Kitengo cha Usalama wa Serikali
kilitengewa TZS. 54.9 milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida na hadi kufikia
mwezi Machi 2013, kiliingiziwa TZS. 29.0 milioni sawa na asilimia 52.8 ya
makadirio ya matumizi.
82.
Mheshimiwa
Spika, kazi kubwa za kitengo hiki ni za
kufanya upekuzi endelevu kwa wafanyakazi wanaotaka kuajiriwa. Katika mwaka wa
fedha 2012/2013, Kitengo cha Usalama wa Serikali (GSO) kimefanya ukaguzi katika
Taasisi tisa za Serikali. Taasisi hizo ni Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Wizara
ya Biashara Viwanda na Masoko – Unguja na Pemba, Kituo cha Matrekta Macho Mane
– Pemba, Wizara ya Kilimo na Mali Asili – Pemba, Shirika la Bima – Unguja na
Pemba, Chuo cha Kilimo Kizimbani – Unguja, Viwanja vya Ndege – Unguja na
Pemba, Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa
Bahari Kuu – Unguja na Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati. Aidha, katika
kipindi hiki Kitengo kilifanya upekuzi wa kiusalama kwa wafanyakazi 168 wa Taasisi
mbali mbali za Serikali na kutoa ushauri wa kiusalama kwa Taasisi hizo. Taasisi
zilizokaguliwa zimeoneshwa kwenye Kiambatanisho Nambari
8.
83. Mheshimiwa Spika, Kitengo
kimeendesha mafunzo ya utunzaji wa nyaraka na siri za Serikali kwa watumishi wa
Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko. Mafunzo hayo yalihusu udhibiti wa siri
za Serikali na kuelimisha watumishi juu ya umuhimu wa nyaraka na kumbukumbu za
Serikali. Aidha, Kitengo kimeendesha mafunzo kama hayo katika Chuo cha Kilimo
Kizimbani, Wahudumu, Madereva, Maafisa masjala wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi, Makatibu Muhtasi wa Mawaziri na Makatibu Wakuu wa
Wizara zote za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
84. Mheshimiwa Spika,
kwa mwaka wa fedha 2013/214, Kitengo cha Usalama wa Serikali kimepanga
kutekeleza malengo yafuatayo:-
(i)
Kuimarisha shughuli za upekuzi kwa watumishi
kabla na baada ya kuajiriwa;
(ii)
Kuimarisha ukaguzi wa majengo, miundombinu
na mali za Serikali;
(iii)
Kuwajengea uwezo watumishi juu ya utunzaji
na udhibiti wa siri za Serikali;
(iv)
Kufanya tathmini ya utekelezaji wa maelekezo
yanayotolewa kwa Wizara/Taasisi wakati wa ukaguzi; na
(v)
Kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi
85. Mheshimiwa Spika, ili
Kitengo cha Usalama wa Serikali (GSO) kiweze kutekeleza malengo yake kwa
ufanisi, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS.
61.6 milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida.
OFISI YA USAJILI NA
KADI ZA UTAMBULISHO
86. Mheshimiwa Spika,
Ofisi ya Usajili na Kadi za Utambulisho imefanya kazi zake kwa ufanisi kwa
mujibu wa Sheria. Kwa mwaka wa fedha 2012/2013, Ofisi ya Usajili na Kadi za Utambulisho
iliidhinishiwa TZS. 1,593.0 milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida na hadi mwezi
Machi 2013, iliingiziwa TZS. 1,086.9 milioni
sawa na asilimia 68.2 ya makadirio.
87. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Usajili na Kadi za Utambulisho imefanya usajili wa Wazanzibari
wakaazi 26,594 waliotimiza masharti ya usajili ikiwa ni ongezeko la asilimia 151
ukilinganisha na idadi ya Wazanzibari Wakaazi 10,578 waliosajiliwa katika mwaka
2011/2012. Aidha, Ofisi imetengeneza vitambulisho vipya 18,532 vilivyomaliza
muda wake wa matumizi na imetengeneza vitambulisho 5,178 kwa wananchi
waliopoteza na walioomba kufanya marekebesho halali ya taarifa zao binafsi.
88. Mheshimiwa Spika,
Ofisi imeendelea kutengeneza vitambulisho vya wafanyakazi wa Serikali na
Taasisi zake ambapo jumla ya vitambulisho 2,410 vimetengenezwa. Aidha, jumla ya
vitambulisho 1,347 vya Mashirika ya Serikali na 2,188 vya Idara Maalum za
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar vimetengenezwa.
89. Mheshimiwa Spika, naomba
kutoa taarifa kuwa Sheria Namba 7/2005 imefanyiwa marekebisho kuwa Sheria Namba
14/2012 ili kuruhusu kutoa vitambulisho maalumu kwa wageni wanaoishi Zanzibar.
Utaratibu wa kutoa vitambulisho umekamilika na Serikali inategemea kuanzisha
rasmi utoaji wa vitambulisho hivyo katika mwaka ujao wa fedha wa 2013/2014.
90. Mheshimiwa Spika, katika
kuongeza uelewa wa wananchi juu ya umuhimu wa matumizi bora ya Kitambulisho cha
Mzanzibari, Ofisi ya Usajili na Kadi za Utambulisho imeandaa na kurusha hewani
jumla ya vipindi 18 kupitia Shirika la Utangazaji la Zanzibar. Aidha, Ofisi
imeendelea kuwajengea uwezo wa kitaaluma wafanyakazi wake katika ngazi za Cheti,
Stashahada na Shahada.
91. Mheshimiwa Spika,
Ofisi imefanyiwa ukaguzi na Shirika la Viwango vya Kimataifa (I Q Net) juu ya
mfumo na viwango. Taarifa ya ukaguzi huo imethibitisha kuwa mfumo na taratibu
zinazotumika ziko katika kiwango kinachokubalika Kimataifa. Sambamba na hilo,
Ofisi imenunua seti 15 za mashine za kisasa za usajili. Mashine hizo
zinategemewa kusaidia shughuli za usajili katika Ofisi za Wilaya.
92. Mheshimiwa Spika,
kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Ofisi ya Usajili na Kadi za Utambulisho
inakusudia kutekeleza malengo yafuatayo:-
(i)
Kuwasajili Wazanzibari Wakaazi waliotimiza
masharti kwa mujibu wa Sheria na kuwapatia vitambulisho;
(ii)
Kutunza taarifa za waliosajiliwa katika
database maalum;
(iii)
Kuwasajili na kutoa vitambulisho maalum kwa
wageni wanaoishi Zanzibar kwa ruhusa maalum;
(iv)
Kuzishajihisha Taasisi za Serikali kutumia
taarifa zilizowekwa katika “Database” ya Ofisi ya Usajili na Kadi za Utambulisho
kwa usalama na kiuchumi;
(v)
Kuratibu masuala mtambuka pamoja na kutoa
elimu ya kujikinga na maambukizi mapya ya UKIMWI kwa wafanyakazi;
(vi)
Kuendelea kuwajengea uwezo kielimu
wafanyakazi wa Ofisi; na
(vii) Kuongeza ufanisi kazini
ikiwa ni pamoja na kuwapatia wafanyakazi stahili zao.
93. Mheshimiwa Spika,
ili Ofisi ya Usajili na Kadi za Utambulisho iweze kutekeleza malengo yake kwa
ufanisi, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS.
2,055.0 milioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
OFISI YA OFISA
MDHAMINI – PEMBA
94. Mheshimiwa Spika,
Ofisi ya Ofisa Mdhamini – Pemba ina jukumu la kuratibu na kusimamia shughuli za
utawala na huduma za Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Pemba.
Aidha, Ofisi ya Ofisa Mdhamini inawajibu wa kuratibu na kusimamia ziara za
Viongozi Wakuu wa Kitaifa na Kimataifa Kisiwani
Pemba.
95. Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka wa fedha 2012/2013, Ofisi ya Ofisa Mdhamini – Pemba iliidhinishiwa jumla
ya TZS. 462.4 milioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na hadi kufikia Machi
2013, iliingiziwa TZS. 385.2 milioni sawa na asilimia 83.3 ya makadirio ya
matumizi.
96. Mheshimiwa Spika, Ofisi
ya Ofisa Mdhamini Pemba imeendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji wa
shughuli za Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Pemba kwa
kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo
inayotekelezwa na Taasisi za Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Pemba. Aidha, Ofisi imeratibu
na kuwawezesha maofisa kushiriki katika mikutano na vikao mbali mbali vilivyofanyika
Unguja vikiwemo vikao vya Bodi ya Zabuni, Bajeti, na Uwasilishaji wa Ripoti za
Utekelezaji.
97. Mheshimiwa Spika, Ofisi
imewawezesha wafanyakazi watatu kupata mafunzo ya Stashahada katika fani ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano na Vyakula na Vinywaji. Vile vile, mfanyakazi mmoja
amepatiwa mafunzo ya muda mfupi juu ya zabuni za majengo na ukandarasi. Aidha, Ofisi
iliandaa mafunzo ya siku moja kwa wafanyakazi 50 wa Taasisi za Ofisi ya Rais na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi - Pemba juu ya utunzaji wa siri za Serikali,
maadili, Sheria na Kanuni za kazi.
98. Mheshimiwa Spika,
katika kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU katika
sehemu za kazi, Ofisi imetoa mafunzo kwa wafanyakazi 50 juu ya kujikinga na
maambukizi mapya ya VVU. Katika mafunzo hayo wafanyakazi hao wameazimia kuweka
siku maalum kwa ajili ya kuendesha zoezi la kupata ushauri nasaha na kupima
afya zao kwa hiari.
99. Mheshimiwa Spika, Ofisi
imesimamia kazi ya kufanya matengenezo katika majengo ya Ikulu ya Mkoani. Kazi
nyengine zilizofanyika ni pamoja na kupaka rangi katika jengo la Ofisi ya Ofisa
Mdhamini, uwekaji wa mtandao mpya wa maji Ofisi Kuu na Ikulu ya Chake Chake ili
kupata huduma hiyo kwa urahisi.
100. Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka wa fedha 2013/2014, Ofisi ya Ofisa Mdhamini – Pemba imepanga kutekeleza
malengo yafuatayo:-
(i)
Kuwajengea uwezo
wafanyakazi sita katika mafunzo ya muda mfupi na mrefu;
(ii)
Kuimarisha uwezo wa Ofisi katika kuratibu
Mipango, Sera na Utafiti;
(iii)
Kuimarisha mazingira bora ya kufanyia kazi,
stahili na kutoa huduma bora;
(iv)
Kuimarisha uwezo wa utendaji wa Serikali za
Mitaa – Pemba; na
(v)
Kuhamasisha wafanyakazi juu ya uwelewa wa masuala
mtambuka ikiwemo UKIMWI, Jinsia na Mazingira.
101. Mheshimiwa
Spika, ili Ofisi ya Ofisa Mdhamini
– Pemba iweze kutekeleza malengo yake kwa ufanisi, kwa mwaka wa fedha
2013/2014, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS. 645.8 milioni kwa ajili
ya matumizi ya kazi za kawaida.
IDARA YA URATIBU WA
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
102.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka
wa fedha 2012/2013, Idara ya Uratibu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
ilitengewa TZS. 701.4 milioni kwa ajili ya matumizi ya kazi za kawaida na TZS. 1,291.0
milioni ikiwa ni Ruzuku kwa Baraza la Manispaa. Hadi Machi 2013, iliingiziwa TZS.
399.0 milioni sawa na asilimia 56.9 kwa matumizi ya kazi za kawaida na TZS. 990.0
milioni sawa na asilimia 76.7 ambazo ni Ruzuku ya Baraza la Manispaa.
103.
Mheshimiwa
Spika, Idara kupitia Tume ya Kurekebisha
Sheria, imeanza mchakato wa kuandaa Sheria mpya ya Vileo kufuatia kupitwa na
wakati Sheria ya zamani (Cap Na. 163/1928). Kwa kuwa Sheria hiyo inaigusa
Jamii, mchakato wake wa kuiandaa uliwashirikisha wadau na wananchi katika
maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba. Mswada wa Sheria hiyo unatarajiwa kuwasilishwa
katika Baraza la Wawakilishi katika mwaka ujao wa fedha 2013/2014.
104.
Mheshimiwa
Spika, Idara imeratibu mkutano mmoja wa
mashirikiano ya pamoja baina ya Viongozi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi na Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) uliofanyika Pemba
kuanzia tarehe 12 hadi 14 Desemba, 2012. Lengo la mkutano huo ni kubadilishana
mawazo, uzoefu na utaalamu miongoni mwa Viongozi na watendaji wa pande zote
mbili katika kuratibu na kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya
Serikali za Mikoa na Serikali za Mitaa.
105.
Mheshimiwa
Spika, mkutano
huo wa mashirikiano uliazimia mambo muhimu yakiwemo kuunda kikosi kazi kwa
pande zote mbili kitakachoangalia uwepo wa Sheria ndogo ndogo za Serikali za
Mitaa na utekelezaji wake katika usimamizi wa usafi wa mazingira pamoja na
ziara za kubadilishana uzoefu. Maazimio hayo ni muhimu kwa maendeleo ya Serikali
za Mikoa na Serikali za Mitaa. Hivyo basi, Ofisi yangu imeanza kuyafanyia kazi
maazimio hayo hatua kwa hatua ikiwemo ziara ya mafunzo kwa Watendaji na
Viongozi wa Serikali za Mitaa katika Jiji la Mwanza ya kujifunza na
kubadilishana uzoefu juu ya usafi wa Mji na mazingira.
106.
Mheshimiwa
Spika, Idara imetoa mafunzo kuhusu utawala
bora katika usimamizi wa majukumu ya Serikali za Mitaa kwa Waheshimiwa Madiwani
wa Kamati za Fedha, Sheria na Afya katika Halmashauri tano. Aidha, Idara
imefuatilia utekelezaji wa miradi ya Halmashauri zote Unguja na Pemba. Matokeo
ya jumla yanaonesha kuwa kiwango cha utekelezaji wa shughuli zilizopangwa kinaridhisha.
107.
Mheshimiwa
Spika, Idara iliendelea kuwawezesha watumishi
wake kuhudhuria mafunzo ya muda mfupi na mrefu. Watumishi watatu walipatiwa
mafunzo ya muda mfupi katika fani za Utawala na Uongozi wa Serikali za Mitaa na
wawili mafunzo ya muda mrefu katika fani za Utunzaji wa Kumbukumbu na Usimamizi
wa Rasilimali Watu.
108. Mheshimiwa Spika,
kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Idara ya Uratibu wa Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa imekusudia kutekeleza malengo yafuatayo:-
(i)
Kuimarisha mazingira bora kazini na utoaji
wa huduma;
(ii)
Kujenga uwezo wa watumishi;
(iii)
Kuimarisha uratibu wa Taasisi za Mikoa, Wilaya,
Serikali za Mitaa na Wadau wa maendeleo; na
(iv)
Kuimarisha ushirikishwaji wa wananchi katika
utawala wa kidemokrasia.
109. Mheshimiwa Spika, ili
Idara ya Uratibu wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa iweze kutekeleza malengo
yake kwa ufanisi, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, naliomba Baraza lako Tukufu
liidhinishe TZS. 643.6 milioni kwa matumizi
ya kazi za kawaida na TZS. 1,200.0 milioni ikiwa ni Ruzuku kwa Baraza la
Manispaa.
MAMLAKA ZA SERIKALI
ZA MIKOA
110. Mheshimiwa Spika, Mamlaka
za Serikali za Mikoa zimepewa jukumu la kuratibu na kusimamia utekelezaji wa maagizo
ya Serikali katika maeneo yao ya utawala. Aidha, iliratibu kwa ufanisi mkubwa
shughuli za kupata maoni ya wananchi katika Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania. Pia, Mikoa na Wilaya ilisimamia kikamilifu zoezi la Sensa ya Watu
na Makaazi ya mwaka 2012 kupitia Kamati za Sensa za Wilaya na Mikoa kwa
kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali. Pamoja na hayo, naomba kutoa maelezo kuhusu utekelezaji
wa malengo ya Mamlaka za Serikali za Mikoa kwa mwaka 2012/2013 na utekelezaji
wa malengo yaliyopangwa kwa mwaka 2013/2014.
MKOA WA MJINI
MAGHARIBI
111.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/2013 Mkoa wa
Mjini Magharibi uliidhinishiwa TZS. 1,099.0 milioni kwa kazi za kawaida na hadi
kufikia mwezi wa Machi 2013, Mkoa huu umeingiziwa TZS. 709.4 milioni sawa na
asilimia 64.5 ya makadirio ya matumizi.
112.
Mheshimiwa
Spika, hali ya ulinzi na usalama katika Mkoa
wa Mjini Magharibi imeendelea kuwa nzuri ingawa kumejitokeza matukio ya uhalifu
ambayo yaliishitua jamii. Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa imekutana katika
vikao vyake mbali mbali kupanga mikakati ili kuhakikisha kuwa vitendo hivyo vya
uhalifu vinadhibitiwa. Mkoa umeendelea kushajihisha uimarishaji wa ulinzi
shirikishi katika Shehia zote za Mkoa. Hata hivyo, mkazo zaidi umewekwa katika
Shehia za Kianga, Sharifumsa, Kwaalinatu na Amani. Kutokana na hatua hiyo, matokeo
yanaonesha kuwa uhalifu umepunguwa na hasa utumiaji wa madawa ya kulevya katika
Shehia hizo.
113.
Mheshimiwa
Spika, Operesheni maalum ya kuwaondosha
wanyama wanaozurura ovyo Mjini pamoja na wafanyabiashara wanaofanya biashara kiholela
tena sehemu zisizoruhusiwa katika Masoko imefanyika. Operesheni hii
inayosimamiwa na Mkoa kupitia Baraza la Manispaa na Halmashauri ya Wilaya ya
Magharibi imeweza kudhibiti uzururaji wa wanyama na zaidi ya wanyama 190
wamekamatwa na kupelekwa katika maeneo maalum yaliyotengwa. Kwa wale wanyama
waliogombolewa huwa wanarejeshewa wenyewe kwa masharti maalum yakiwemo wanyama
hao kupelekwa nje ya Mji na gharama za upelekaji huo hulipwa na mmiliki wa
mnyama husika. Aidha, wanyama wote waliogombolewa huwekwa rangi maalum na
pindipo akikamatwa tena hatua za kisheria huchukuliwa dhidi ya mmiliki.
114.
Mheshimiwa
Spika, Katika kuimarisha ufanisi na utendaji
kazi, Mkoa umefanikiwa kulipa Stahili za wafanyakazi, kununua vifaa vya
kutendea kazi, kuanza matengenezo madogo na makubwa ya Ofisi. Aidha, mafunzo ya
Sheria Namba 2/2011 ya Usimamizi wa Utumishi wa Umma Zanzibar yametolewa kwa
wafanyakazi. Wafanyakazi 13 wamesomeshwa katika ngazi ya Stashahada ya Uzamili,
Stashahada na Cheti kwa fani za Uhasibu, Uandishi wa Habari, Utunzaji wa Kumbukumbu,
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Rasilimali Watu, Ukatibu Muhtasi na Utawala
wa Umma. Mchanganuo wa watendaji waliopatiwa mafunzo unaonekana katika
Kiambatanisho Nambari 9.
115.
Mheshimiwa
Spika, mafunzo juu ya kupambana na UKIMWI na
kupiga vita unyanyasaji wa kijinsia yametolewa kwa wafanyakazi 91, Masheha 45,
na makundi matatu ya kijamii yakiwemo watu wenye ulemavu, watu wenye kuishi na
VVU na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi. Kamati za mazingira za Wilaya
zimeundwa na kuendesha vikao, ufuatiliaji na uhamasishaji wananchi juu ya
uhifadhi wa mazingira, usafishaji wa misingi ya maji machafu pamoja na upandaji
wa miti.
116.
Mheshimiwa
Spika, Mkoa umeratibu na kusimamia miradi
mbali mbali iliyoanzishwa na wananchi. Utekelezaji wa miradi hiyo kwa hatua
mbali mbali unaonekana katika Kiambatanisho Nambari 10. Aidha, jumla ya vikundi
51 vya SACCOS na Ushirika vimetembelewa na kupatiwa ushauri wa kuviendeleza
vikundi vyao.
117.
Mheshimiwa
Spika, kazi nyengine zilizotekelezwa na Mkoa
ni pamoja na:-
(i)
Kukutana na Wakurugenzi
Mipango, Sera na Utafiti wa Wizara 16 za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa
azma ya kuimarisha na kusaidia utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika Mkoa;
(ii)
Utatuzi wa migogoro kumi
na moja ya ardhi kati ya 34 iliyoripotiwa pamoja na kutoa mafunzo juu ya matumizi
bora ya ardhi kwa jamii;
(iii) Kufuatilia
na kutoa mafunzo ya uwekaji wa kumbukumbu katika Shehia 27 kati ya 84;
(iv) Kufuatilia
kesi saba za udhalilishaji wa wanawake na watoto;
(v)
Kusimamia uandikishaji
wa watoto 13,321 waliofikia umri wa kuanza darasa la kwanza;
(vi) Kuhamasisha
ukulima wa kilimo cha mpunga ambapo jumla ya ekari 1,912 zimelimwa kati ya
ekari 1,800 zilizolengwa awali na ekari 1,042 kati ya ekari 917 za mazao ya
chakula na ekari 237 za mboga mboga;
(vii) Wananchi
63 wamepatiwa misaada ya kijamii na kiuchumi; na
(viii) Utoaji
wa mafunzo juu ya Uibuaji Miradi, Upangaji wa Mipango na Usimamizi wa Fedha kwa
Wajumbe wa Kamati za Maendeleo za Shehia 25 na kuwashirikisha Wenyeviti na Makatibu
pamoja na washika fedha wa Kamati hizo.
118. Mheshimiwa Spika,
kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Mkoa wa Mjini Magharibi unatarajia kutekeleza malengo
yafuatayo:-
(i) Kuimarisha kiwango cha utendaji kwa wafanyakazi wa Mkoa wa Mjini Magharibi
na Sekta ziliopo;
(ii) Kuimarisha hali ya ulinzi na usalama ndani ya Mkoa;
(iii) Kuhakikisha jamii yenye afya njema; na
(iv) Kuhakikisha maendeleo endelevu kwa jamii.
119. Mheshimiwa Spika,
ili Mkoa wa Mjini Magharibi uweze kutekeleza malengo iliyojipangia kwa ufanisi,
kwa mwaka wa fedha 2013/2014, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS. 1,455.0
milioni kwa ajili ya matumizi ya kazi za kawaida.
MKOA WA KUSINI UNGUJA
120.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, Mkoa
uliidhinishiwa TZS. 1,064.0 milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida na hadi
mwezi Machi 2013, uliingiziwa TZS. 680.4 milioni sawa na asilimia 63.9 ya fedha
zilizoombwa.
121.
Mheshimiwa
Spika, kwa ujumla hali ya ulinzi na usalama
katika Mkoa imezidi kuimarika. Kamati ya Ulinzi na usalama ilifanya vikao tisa
kutathmini hali hiyo ndani ya Mkoa. Aidha, kikao kimoja cha Kamati ya Maendeleo
ya Mkoa (RDC) kimefanyika na vikao vitatu kujadili utekelezaji na uratibu wa
Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010.
122.
Mheshimiwa
Spika, Mkoa umefanya ukaguzi katika vituo 17
vya mitihani vya Wilaya zote mbili kati ya vituo 29 viliomo katika Mkoa. Aidha,
Mkoa uliratibu kikao kimoja kilichojadili mbinu za kukabiliana na utoro
maskulini. Mikakati iliobuniwa na kutekelezwa katika Mkoa imesaidia kupunguza
tatizo la utoro ambapo katika hatua ya awali wanafunzi 18 wa Skuli ya Charawe
wamerejeshwa Skuli na kuendelea tena na masomo.
123.
Mheshimiwa
Spika, Mkoa umefuatilia hali ya usambazaji wa
maji safi na salama. Miradi ya maji safi na salama ndani ya Mkoa inaendelea
vizuri ikiwemo ujenzi wa matangi ya maji yaliopo Machui, Jumbi na Pongwe.
Aidha, ulazaji wa mabomba ya maji safi katika Shehia za Chwaka na Miwani
umekamilika na huduma imeanza kupatikana.
124.
Mheshimiwa
Spika, sambamba na hayo, Mkoa umesimamia
kikamilifu kilimo cha mpunga ambapo jumla ya ekari 1,444.5 za mpunga katika
Wilaya ya Kati na ekari 119.0 katika Wilaya ya Kusini zimechimbwa na kuburugwa.
Hatua hii inafanya jumla ya ekari zilizochimbwa, kuburugwa na kupandwa katika
Mkoa wa Kusini Unguja kufikia 1,563.5.
125.
Mheshimiwa
Spika, Mkoa umeratibu mchakato wa kuwatambua
watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Katika utambuzi huo
jumla ya watoto 35 wametambuliwa na kupatiwa msaada wa sare za skuli, viatu na
vifaa vya kusomea. Aidha, katika kuufanya utaratibu huu uwe endelevu, Mkoa umetenga
fedha kwa ajili ya kuwasaidia watoto hao.
126.
Mheshimiwa
Spika, kazi nyengine zilizotekelezwa na Mkoa
ni pamoja na:-
(i)
Kuanza ujenzi wa
Ofisi ya Wilaya ya Kati hadi kufikia hatua ya kuinua msingi;
(ii)
Kusimamia matengenezo
ya vyombo vya usafiri pamoja na ununuzi wa samani na vifaa vya Ofisi;
(iii) Kuwajengea
uwezo wa kiutendaji wafanyakazi wake ambapo wafanyakazi saba wamepatiwa mafunzo
ya muda mfupi na mrefu katika fani za Upangaji na Usimamizi wa Miradi, Uhasibu
na Udereva; na
(iv) Kutoa
taaluma kwa wafanyakazi wake juu ya namna ya kujikinga na maambukizi mapya ya
VVU. Jumla ya wananchi 85 nao waliweza kupatiwa ushauri nasaha na kupima VVU
kwa hiari wakati wa Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani.
127.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Mkoa
wa Kusini Unguja umekusudia kutekeleza malengo yafuatayo:-
(i)
Kusimamia shughuli za
ulinzi na usalama;
(ii)
Kuratibu, kusimamia,
kufuatilia na kusaidia utekelezaji wa shughuli za sekta mbali mbali;
(iii) Kuwajengea
uwezo wafanyakazi kwa kuwapatia mafunzo ya muda mfupi na mrefu ili kuongeza
ufanisi kazini;
(iv) Kusimamia
na kuzitumia ipasavyo rasilimali watu na vitu katika kuleta maendeleo ya
kiuchumi na kijamii;
(v)
Kuendeleza jengo la
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Wilaya na matengenezo madogo madogo; na
(vi) Kuratibu
shughuli Mtambuka zikiwemo za UKIMWI, mazingira na masuala ya watu wenye
ulemavu.
128. Mheshimiwa Spika, ili
Mkoa wa Kusini Unguja uweze kutekeleza malengo yake kwa ufanisi, kwa mwaka wa
fedha 2013/2014, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS. 1,147.0 milioni
kwa matumizi ya kazi za kawaida.
MKOA WA KASKAZINI
UNGUJA
129.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, Mkoa wa
Kaskazini Unguja ulitengewa TZS. 1,083.0 milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida
na hadi Machi 2013, uliingiziwa TZS. 735.0 milioni sawa na asilimia 67.9 ya makadirio
ya matumizi ya kawaida.
130.
Mheshimiwa
Spika, Mkoa umeratibu vikao sita vya Kamati
ya Ulinzi na Usalama ambavyo vilijadili masuala mbali mbali na kupitia taarifa
za hali ya ulinzi na usalama katika Mkoa. Hali ya usalama katika Mkoa
imeendelea kuimarika kufuatia hali ya udhibiti wa vitendo vinavyoashiria
uvunjifu wa amani.
131.
Mheshimiwa
Spika, Mkoa umeendesha mikutano mitano ya
kuhamasisha wananchi juu ya umuhimu wa kushiriki katika utekelezaji wa Miradi ya
maendeleo pamoja na kufanya mikutano miwili ya Kamati ya Maendeleo ya Mkoa na
mikutano sita ya Kamati za Maendeleo ya Wilaya. Mkoa ulisimamia utekelezaji wa
miradi mbali mbali ya wananchi ikiwemo ujenzi wa mabanda matatu ya Skuli ya
Matetema, ujenzi wa Skuli ya Kidagoni,
ujenzi wa mabanda mawili ya Skuli ya Pangeni, ujenzi wa ukumbi wa
kufanyia mitihani, ujenzi wa maktaba Tumbatu Jongowe na ujenzi wa kituo cha
Afya Bumbwini Kiongwe. Aidha, Mkoa ulikuwa na jumla ya migogoro ya ardhi 20
ambayo imeripotiwa. Katika jitihada zake za kutatua migogoro hiyo, minane
iliyopo katika maeneo ya Matemwe, Kiwengwa, Pwani Mchangani na Nungwi
imetatuliwa, migogoro minne imepelekwa mahakamani kutokana na utata wake. Jumla
ya migogoro minane imo katika hatua ya kupatiwa ufumbuzi.
132.
Mheshimiwa
Spika, wafanyakazi wa Mkoa wameendelea
kujengewa uwezo kwa kuwapatia mafunzo ya
muda mrefu na mfupi katika ngazi ya Stashahada ya juu na Shahada ya pili ya
Maendeleo Vijijini, Shahada ya kwanza ya Uhasibu, Stashahada ya Ukatibu
Muhutasi na Stashahada ya Manunuzi na Ugavi. Aidha, wafanyakazi 21 wamepatiwa
mafunzo ya siku mbili juu ya Utawala bora. Jumla ya mikutano 12 imefanyika juu
ya uhamasishaji wa kujikinga na maambukizi mapya ya VVU kwa wafanyakazi na wananchi
kwa ujumla.
133.
Mheshimiwa
Spika, kazi nyengine zilizofanywa na Mkoa ni
pamoja na kufuatilia utekelezaji wa shughuli za mashamba darasa 12, vituo vya
kilimo viwili na mabonde ya mpunga sita. Mkoa pia ulifuatilia shughuli za
mifugo na uvuvi ambapo vituo sita vya mifugo, wafugaji 75 wa ng’ombe na 53 wa
kuku pamoja na Skuli 36 za mafunzo ya mifugo na madiko sita ya uvuvi. Aidha, Skuli
41, vituo 31 vya elimu ya watu wazima, Maktaba mbili pamoja na madarasa 38
mapya vimefuatiliwa sambamba na shughuli nyengine za sekta za afya, mazingira
na utalii.
134.
Mheshimiwa
Spika, Ujenzi wa jengo jipya la Ofisi ya Mkuu
wa Mkoa umekamilika kwa kiwango cha kuweza kuhamiwa. Aidha, ukarabati wa jengo
la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kaskazini “A” umefanyika.
135.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Mkoa wa
Kaskazini Unguja unakusudia kutekeleza malengo yafuatayo:-
(i) Kuimarisha
hali ya ulinzi na usalama katika Mkoa;
(ii) Kuimarisha
ushiriki wa wananchi katika utawala wa kidemokrasia;
(iii) Kuongeza
uelewa wa wafanyakazi katika masuala mtambuka (UKIMWI na Mazingira);
(iv) Kuandaa
mazingira mazuri katika uendeshaji wa shughuli za Ofisi; na
(v) Kuwajengea
uwezo wafanyakazi.
136. Mheshimiwa Spika,
ili Mkoa wa Kaskazini Unguja uweze kutekeleza malengo yake kwa ufanisi, kwa
mwaka wa fedha 2013/2014, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS. 1,247.0
milioni kwa ajili ya matumizi ya kazi za kawaida.
MKOA WA KUSINI PEMBA
137.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, Mkoa
uliidhinishiwa jumla ya TZS. 1,741.0 milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida, kati
ya hizo TZS. 1,169.0 milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida za Mkoa, TZS.
363.0 milioni Ruzuku kwa Baraza la Mji Chake Chake na TZS. 209.0 milioni kwa
ajili ya Ruzuku Baraza la Mji Mkoani. Hadi kufikia mwezi Machi 2013, Mkoa
uliingiziwa TZS. 683.3 milioni sawa na asilimia 58.5 ya fedha zilizoidhinishwa
kwa kazi za kawaida, TZS. 258.0 milioni sawa na asilimia 71.1 ya Ruzuku kwa Baraza la Mji Chake Chake
na TZS. 151.7 milioni sawa na asilimia 72.6 ya Ruzuku kwa Baraza la Mji Mkoani.
138.
Mheshimiwa
Spika, Mkoa umefanya vikao vinne vya Kamati
ya Ulinzi na Usalama. Aidha, vikao vitatu vya Kamati ya Ukaguzi wa Hesabu na
vikao viwili vya Bodi ya Zabuni vimefanyika. Mkoa pia umeratibu utekelezaji wa
miradi ya sekta mbali mbali zikiwemo za kilimo, elimu, afya, miundombinu,
utawala bora na maendeleo ya vijana.
139.
Mheshimiwa
Spika, kiwanja kinachokusudiwa kujengwa nyumba
ya Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa tayari kimepatikana pamoja na hati miliki ya kiwanja
hicho. Mtaalamu wa kutayarisha michoro amepatikana na hatua za ujenzi zinatarajiwa
kuanza mara baada ya kukamilisha kazi yake.
140.
Mheshimiwa
Spika, Mkoa umesimamia Miradi mbali mbali ya
maendeleo ya wananchi katika Wilaya zake zote mbili, maelezo ya kina ya
utekelezaji ya miradi hiyo yamewekwa katika Kiambatanisho Nambari 15. Aidha,
mfanyakazi mmoja amepatiwa mafunzo ya muda mrefu katika ngazi ya cheti Chuo cha
Utumishi wa Umma Unguja. Mkoa pia umetayarisha semina kwa wafanyakazi 76 juu ya
Jinsia na namna ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI.
141.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Mkoa wa
Kusini Pemba unakusudia kutekeleza malengo yafuatayo:-
(i) Kuimarisha
ulinzi na usalama kwa raia na mali zao;
(ii) Kuimarisha
uratibu, usimamiaji na ufuatiliaji wa kazi za maendeleo ya Mkoa;
(iii) Kuimarisha
kiwango cha taaluma kwa wafanyakazi saba kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu na
mfupi;
(iv) Kuwajengea
uwezo wafanyakazi juu ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI; na
(v) Kuimarisha
mazingira bora ya kazi ili kuleta ufanisi, umakini na uwajibikaji.
142.
Mheshimiwa
Spika, ili Mkoa wa Kusini Pemba uweze
kutekeleza malengo yake kwa ufanisi, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, naliomba
Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya TZS 1,871.0 milioni kwa matumizi ya
kawaida. Kati ya hizo, TZS. 1,290.0 milioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, TZS. 370.0 milioni ni Ruzuku kwa Baraza la Mji Chake
Chake na TZS. 211.0 milioni ni Ruzuku kwa Baraza la Mji Mkoani.
MKOA WA KASKAZINI
PEMBA
143.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, Mkoa wa
Kaskazini Pemba uliidhinishiwa jumla ya TZS. 1,384.0 milioni kwa matumizi ya
kazi za kawaida, kati ya hizo TZS. 275.0 milioni ni Ruzuku kwa Baraza la Mji
Wete. Hadi mwezi Machi 2013, Mkoa uliingiziwa TZS. 709.6 milioni sawa na
aslimia 64.0 ya fedha zilizoidhinishwa na TZS. 176.0 milioni sawa na asilimia
64.0 ya fedha za Ruzuku kwa Baraza la Mji Wete.
144.
Mheshimiwa
Spika, Mkoa umefanya vikao 15 vya Kamati ya Ulinzi
na Usalama ambavyo vimepelekea hali ya usalama na amani katika Mkoa huu
kuimarika. Aidha, umeratibu na kusimamia utekelezaji wa Miradi
ya maendeleo ya sekta mbali mbali ikiwemo elimu, afya, maji safi, miundombinu
ya barabara, kilimo, mifugo, uvuvi, ustawi wa jamii na maendeleo ya wanawake,
vijana na watoto. Mkoa pia, umefuatilia utekelezaji wa Miradi ya maendeleo iliyoanzishwa
na wananchi ikiwemo ya vituo vya afya vya Bwagamoyo na Kifundi, ujenzi wa
madarasa ya Skuli ya Kiuyu Kipangani pamoja na uendelezaji wa ujenzi wa
barabara zinazojengwa na Kampuni ya MECCO na H. Young. Barabara hizo ni za
Mtambwe, Pandani, Konde, Gando, Kangagani na Likoni.
145.
Mheshimiwa
Spika, Mkoa umefanya ukarabati mdogo katika
Ofisi ya Ofisa Tawala Mkoa kwa kukata vyumba (partition) pamoja na kufanya
marekebisho ya mfumo wa umeme na kuvuta laini mpya ya maji na baadhi ya matengenezo
ya nyumba za Wakuu wa Wilaya ya Wete na Micheweni. Aidha, katika kuimarisha
taaluma ya wafanyakazi kiutendaji, Mkoa umewapatia wafanyakazi saba mafunzo ya muda mfupi na mrefu katika fani ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Utunzaji wa kumbukumbu, Uhasibu, Ununuzi
na Ugavi, Rasilimali Watu na Sayansi ya Jamii.
146.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Mkoa wa
Kaskazini Pemba unakusudia kutekeleza malengo yafuatayo:-
(i) Kuimarisha
mazingira bora ya kazi na kuona wafanyakazi wanawajibika ipasavyo;
(ii) Kuimarisha
ulinzi na usalama wa raia na mali zao;
(iii) Kusimamia,
kuratibu na kufuatilia shughuli mbali
mbali za kisekta na maendeleo ya Mkoa;
(iv) Kuwajengea
uwezo wa kielimu wafanyakazi saba kwa kuwapatia mafunzo ya muda mrefu na mfupi; na
(v) Kuwajengea
uwezo wafanyakazi juu ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI.
147. Mheshimiwa Spika, ili
Mkoa wa Kaskazini Pemba uweze kutekeleza malengo yake kwa ufanisi, kwa mwaka wa
fedha 2013/2014, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya TZS. 1,558.0
milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida. Kati ya hizo TZS. 280.0 milioni kwa
ajili ya Ruzuku ya Baraza la Mji Wete.
IDARA YA URATIBU WA
IDARA MAALUM ZA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR
148.
Mheshimiwa
Spika, Idara hii ina wajibu wa kusimamia na
kuratibu kazi za Idara Maalum za SMZ zikiwemo za kusimamia utekelezaji wa Sera,
Sheria na Kanuni za Idara Maalum, kusimamia vikao vya Tume ya Utumishi pamoja
na Mahkama ya Rufaa za Idara Maalum za SMZ. Aidha, Idara ina majukumu ya kisera
ya kuoanisha miundo ya kiutumishi, maslahi ya maafisa na wapiganaji, kuwajengea
uwezo wa kiutendaji na kuratibu masuala ya michezo na utamaduni ndani ya Idara
Maalum za SMZ.
149.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, Idara
ilitengewa TZS 200.0 milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida
na hadi mwezi Machi 2013, Idara ilikuwa tayari imeingiziwa TZS 105.0 milioni
sawa na asilimia 52.5 ya fedha zilizoidhinishwa.
150.
Mheshimiwa
Spika, Idara ya
Uratibu wa Idara Maalum za SMZ imeandaa Miundo ya Utumishi (Scheme of Services)
ya Idara Maalum za SMZ ili kuimarisha maslahi na majukumu ya watumishi wa Idara
hizo. Miundo hiyo tayari imewasilishwa Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na
Utawala Bora kwa ajili ya kupata maamuzi. Miundo ya Utumishi ya Idara hizo inatarajiwa
kuanza kutumika katika mwaka ujao wa fedha wa 2013/2014.
151.
Mheshimiwa
Spika, vikao vitatu vya Tume ya Utumishi ya Idara Maalum na
Kamati ya Ajira ya Idara Maalum za SMZ vimefanyika kupitia utaratibu wa ajira
katika Idara hizo. Sambamba na hilo, Tume ya Utumishi ya Idara Maalum
ilizingatia maombi ya kupandishwa vyeo kwa Wapiganaji na Maofisa pamoja na
kusikiliza malalamiko kutoka kwa watumishi wa Idara Maalum za SMZ. Aidha, vikao
vitatu vya Mahkama ya Rufaa ya Idara Maalum za SMZ vimefanyika ambapo jumla ya
rufaa nne zilijadiliwa na kutolewa maamuzi.
152.
Mheshimiwa
Spika, katika
kuwaendeleza watumishi kitaaluma, wafanyakazi wake wawili wamepatiwa mafunzo ya
muda mrefu na mfupi katika fani za Mipango ya Maendeleo na Habari na
Mawasiliano. Vilevile, Idara imeendelea kuweka mazingira mazuri ya kazi ili
kuongeza ufanisi kwa kununua vitendea kazi vikiwemo samani za Ofisi.
153.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Idara ya
Uratibu wa Idara Maalum za SMZ ina mpango wa kutekeleza malengo yafuatayo:-
(i) Kuweka
mazingira mazuri ya kufanya kazi ili Idara iweze kutoa huduma nzuri;
(ii) Kuimarisha
uratibu na ufuatiliaji wa shughuli za Idara Maalum za SMZ Unguja na Pemba;
(iii) Kuwajengea
uwezo wa kiutendaji watumishi wa Idara kwa kuwapeleka mafunzoni ndani na nje ya
Zanzibar; na
(iv) Kuandaa
vikao vya rufaa vya Idara Maalum za SMZ.
154.
Mheshimiwa
Spika, ili Idara ya Uratibu wa Idara Maalum
za SMZ iweze kutekeleza malengo yake kwa ufanisi, kwa mwaka wa fedha 2013/2014,
naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS 144.8 milioni kwa ajili ya matumizi
ya kazi za kawaida.
TUME YA UTUMISHI YA
IDARA MAALUM ZA SMZ
155.
Mheshimiwa
Spika, kuanzia mwaka ujao wa fedha wa
2013/2014, Tume ya Utumishi ya Idara Maalum za SMZ itakuwa na kasma yake ndogo
na hivyo kuiondoa kutoka katika kasma ya Idara ya Uratibu ya Idara Maalum.
Hatua hii imechukuliwa ili kuifanya Tume hiyo iweze kusimamia vizuri kazi zake.
156.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Tume ya
Utumishi ya Idara Maalum inakusudia kutekeleza malengo yafuatayo:-
(i) Kuimarisha mazingira bora ya
Utumishi wa Idara Maalum;
(ii) Kutoa
elimu kwa Maafisa na Wajumbe wa Tume ya Utumishi ya Idara Maalum za SMZ;
(iii) Kuhakikisha
kazi za Tume zinafanyika ipasavyo; na
(iv) Kufuatilia
ajira na maslahi ya Watumishi wa Idara Maalum za SMZ kwa kushirikiana na Tume
ya Utumishi Serikalini.
157. Mheshimiwa Spika, ili
Tume ya Utumishi ya Idara Maalum za SMZ iweze kutekeleza malengo yake kwa
ufanisi, katika mwaka wa fedha 2013/2014, naliomba Baraza lako Tukufu
liidhinishe TZS. 53.2 milioni
kwa matumizi ya kazi za kawaida.
KIKOSI MAALUM CHA
KUZUIA MAGENDO (KMKM)
158.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, Kikosi Maalum
cha Kuzuia Magendo (KMKM) kilitengewa TZS 9,660.0 milioni kwa ajili ya matumizi
ya kazi za kawaida na TZS. 200.0 milioni kwa kazi za maendeleo. Hadi kufikia
Machi 2013, Kikosi kiliingiziwa TZS. 6,188.3 milioni sawa na asilimia 64.1 ya
bajeti iliyoombwa kwa kazi za kawaida. Kwa upande wa kazi za maendeleo, fedha
zilizoingizwa ni TZS. 115.0 milioni sawa na asilimia 57.5 ya fedha za maendeleo.
159.
Mheshimiwa
Spika, Kikosi cha KMKM kimeendelea kutoa
huduma ya chakula kwa Makamanda na Wapiganaji wake katika muda wote wanapokuwa
kazini na mafunzoni. Vile vile kimeimarisha nguvu za ulinzi wa doria na
kufanikiwa kukamata vyombo 14 na mali walizokuwa wakizitorosha na kuleta nchini
kimagendo (Kiambatanisho Nambari 16). Vyombo na mali zinazokamatwa huwa
vinakabidhiwa Mamlaka husika kwa hatua zao za kisheria. Aidha, vyombo vyake
vikubwa vimefanyiwa matengenezo pamoja na kuvipeleka chelezoni na kufanya
ununuzi wa vifaa vya mawasiliano.
160.
Mheshimiwa
Spika, kitengo cha uzamiaji (Diving Section)
nacho kimeimarishwa kwa kukinunulia vifaa pamoja na kuendesha mafunzo maalum ya
uzamiaji ili kuweza kukabiliana na majanga. Hivi karibuni, Maofisa wanne
wamekwenda Uingereza kwa ajili ya mafunzo zaidi ya uzamiaji kivitendo chini ya
mwaliko wa kampuni ya “L&W UK and Indeep Diving and Marine Service” ya nchini
humo.
161.
Mheshimiwa
Spika, Kikosi kimekamilisha malipo ya sare
za Maafisa na Wapiganaji wake 500. Matengenezo ya Ofisi ya mipango na kitengo
cha manunuzi pamoja na kununua samani za Ofisi navyo vimefanyika.
162.
Mheshimiwa
Spika, Kikosi kimefanya ukarabati na ujenzi
katika majengo mbali mbali ikiwemo Ofisi ya Idara ya Mipango. Kitengo cha
Manunuzi, banda jipya la kulala askari katika Kambi ya Msuka, hanga moja la
kulala askari katika Kambi mpya ya KMKM Tumbatu ambalo limefikia hatua ya uezekaji
pamoja na ujenzi wa mnara wa Bendera katika Kisiwa cha Tumbatu.
163.
Mheshimiwa
Spika, Hospitali ya KMKM Kibweni imeendelea
kutoa huduma za afya kwa Makamanda na Wapiganaji pamoja na wananchi wanaoishi
maeneo jirani. Takwimu zinaonesha upo muitiko mkubwa wa wananchi kupatiwa
huduma katika hospitali hiyo jambo ambalo limesaidia kupunguza msongamano wa
wagonjwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja. Jumla ya wananchi 16,865 wakiwemo
Makamanda na Wapiganaji walifika hospitalini hapo na kupatiwa huduma, kati yao
wanawake ni 8,645 na wanaume ni 8,220.
164.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Kikosi
Maalum cha Kuzuia Magendo kimepanga kutekeleza malengo yafuatayo:
(i)
Kuwapatia chakula
bora askari wanapokuwa kazini na mafunzoni;
(ii)
Kuimarisha hali ya ulinzi wa doria;
(iii)
Kuimarisha sehemu ya uzamiaji kikosini;
(iv)
Kuhakikisha kuwa Maofisa na Wapiganaji
wanawajibika ipasavyo kwa kupatiwa stahiki zao;
(v) Kuwapatia sare Maofisa na
wapiganaji wote;
(vi) Kuendeleza kuwapatia
elimu ndani na nje ya Kikosi; na
(vii) Kuendeleza ukarabati wa majengo
mbali mbali ya Kikosi Unguja na Pemba.
165. Mheshimiwa Spika, ili
Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo kiweze kutekeleza malengo iliojipangia kwa
ufanisi, katika mwaka wa fedha 2013/2014, naliomba Baraza lako Tukufu
liidhinishe TZS. 9,452.0 milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida.
JESHI LA KUJENGA
UCHUMI (JKU)
166.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/2013 Kikosi
cha JKU kilidhinishiwa TZS. 7,504.0 milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida na
TZS. 300.0 milioni kwa miradi ya maendeleo na hadi Machi 2013, Jeshi la Kujenga
Uchumi limeingiziwa TZS. 5,196.0 milioni sawa na asilimia 69.2 ya fedha.
167.
Mheshimiwa
Spika, Jeshi la Kujenga Uchumi limeendelea
kujenga mazingira mazuri ya kiutendaji kwa kuwapatia watumishi wake fursa za
masomo ya muda mfupi na mrefu. Jumla ya wafanyakazi 10 wanaendelea na masomo
katika ngazi za Shahada ya Uzamili, Shahada ya Kwanza, Stashahada na Cheti.
168.
Mheshimiwa
Spika, Jeshi la Kujenga Uchumi limeendelea kuimarisha
mradi wa ufugaji wa kuku na ng’ombe wa maziwa kwa kununua vifaranga 2,000
(1,000 vya nyama na 1,000 vya mayai) pamoja ng’ombe wawili wa maziwa. JKU pia
imesimamia kilimo cha mazao ya nafaka na miti ya matunda kwa kulima ekari 130
za mpunga, ekari 10 za mahindi, ekari 5 za mtama, ekari 140 za muhogo, ekari 20
za kunde na ekari 5 za miti ya kudumu.
169.
Mheshimiwa
Spika, katika kuimarisha Skuli za Ufundi na
Sekondari, Jeshi la Kujenga Uchumi limeanzisha fani
tatu za mafunzo ya ufundi ambazo ni ufundi wa ushoni, ufundi bomba na useremala
katika Skuli ya Ufundi Chokocho na vifaa kwa ajili ya mafunzo hayo vimenunuliwa.
Aidha, ununuzi wa vifaa vya maabara ya Skuli ya Sekondari ya JKU Mtoni
vimenunuliwa.
170.
Mheshimiwa
Spika, Kikosi cha JKU kimeendelea kutoa
huduma za afya kwa watumishi wake na wananchi wa maeneo jirani. Katika kipindi cha
mwaka 2012/2013 jumla ya wananchi 23,653 wamepatiwa huduma za afya katika vituo
mbali mbali vya JKU. Aidha, elimu ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU imetolewa
kwa wananchi wa maeneo jirani na watumishi waliopo katika kambi mbali mbali
Unguja na Pemba.
171.
Mheshimiwa
Spika, JKU imeendelea kuweka
mazingira mazuri ya kuendeshea mafunzo kwa vijana, jumla ya vijana 400 wa
kujitolea wamesajiliwa na wanaendelea kupatiwa mafunzo. Katika kuimarisha
michezo Kikosi cha JKU kimenunua vifaa vya michezo mbali mbali pamoja na kugharamia
ushiriki wa timu zake katika mashindano ndani na nje ya Zanzibar sambamba na Tamasha
la Michezo lililofanyika Zanzibar.
172.
Mheshimiwa
Spika, kwa ajili ya kuweka
mazingira bora ya utendaji kazi kwa askari wake, JKU imenunua samani za Ofisi,
jokofu, vitanda na magodoro 300, sare za askari 200 pamoja na kufunga mtambo wa
simu.
173.
Mheshimiwa
Spika, katika kuimarisha mashirikiano baina
ya vikosi vya JKU na JKT, Jeshi la Kujenga Uchumi, limeratibu vikao viwili vya mashirikiano baina ya Viongozi Wakuu wa vikosi
hivyo ambapo masuala mbali mbali yanayohusu mafunzo kwa vijana yalijadiliwa
pamoja na kubadilishana uzoefu katika nyanja mbali mbali.
174.
Mheshimiwa
Spika, pamoja na kutekeleza majukumu na
malengo yaliopangwa, Jeshi la
Kujenga Uchumi kwa kutumia vyanzo vyake vya ndani limefanikiwa kuezeka nyumba
ya Mkuu wa Kanda (Zone) Pemba, nyumba ya kuishi askari katika kambi ya Mwambe,
kufanya ukarabati wa Ofisi ya JKU Upenja, kufanya ukarabati mkubwa wa mabweni
ya kuishi askari wa kambi ya Kama na uanzishaji wa duka la dawa liliopo Makao
Makuu.
175.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Jeshi la
Kujenga Uchumi linakusudia kutekeleza malengo yafuatayo:-
(i) Kutoa mafunzo kwa vijana
wanaojiunga na JKU katika nyanja za kilimo, mifugo, ufundi, kazi za amali na
ulinzi wa Taifa ili waweze kujitegemea na kuijenga Nchi yao;
(ii) Kuwapatia wapiganaji sare
na vifaa;
(iii) Kutoa mafunzo kwa
watumishi ili kuongeza ufanisi wa kazi;
(iv) Kuimarisha mashirikiano
na Taasisi mbali mbali ndani na nje ya Zanzibar; na
(v) Kuimarisha utoaji wa
huduma kwa wana JKU na jamii kwa ujumla.
176. Mheshimiwa Spika, ili
Jeshi la Kujenga Uchumi liweze kutekeleza malengo yake kwa ufanisi, kwa mwaka wa
fedha 2013/2014, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS. 7,457.0 milioni
kwa matumizi ya kazi za kawaida na TZS. 250.0 milioni kwa kazi za maendeleo.
IDARA YA CHUO CHA
MAFUNZO (MF)
177.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, Idara ya
Chuo cha Mafunzo iliidhinishiwa TZS. 5,890.0 milioni kwa matumizi ya kazi za
kawaida na TZS. 400.0 milioni kwa mradi wa maendeleo. Hadi Machi 2013, Idara iliingiziwa
TZS 4,007.0 milioni sawa na asilimia 68.0 ya fedha zilizoidhinishwa kwa kazi za
kawaida na TZS. 145 milioni sawa na asilimia 36.3 kwa ajili ya mradi wa
maendeleo.
178.
Mheshimiwa
Spika, katika kuimarisha makaazi ya
wanafunzi wa Vyuo vya Mafunzo, matengenezo ya Chuo cha Kinumoshi yamefanyika.
Pia, Idara ya Chuo cha Mafunzo kwa Kanda za Mashamba inayotarajiwa kujengwa
Langoni imefanyiwa makisio ya ujenzi na michoro yake imekamilika. Sambamba na
hayo, vyoo katika mabweni mawili ya kulala wanafunzi katika Chuo cha Mafunzo
Langoni tayari vimeshawekwa. Aidha, upimaji wa mashamba ya Kinumoshi na Ubago
umekamilika na gharama za hatimiliki zimeshalipwa. Taratibu za kupatiwa
hatimiliki hizo zinaendelea.
179.
Mheshimiwa
Spika, katika kuweka mazingira mazuri ya
kazi, Idara imenunua gari moja aina ya Toyota Vitara, samani za ukumbi wa
mkutano wa Makao Makuu na magodoro 80 kwa matumizi ya wanafunzi. Idara pia imenunua
dawa kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi na askari.
Aidha, Idara imeendelea kuwajengea uwezo watumishi wake kwa kugharamia masomo ya muda mrefu na mfupi kwa watumishi watano wa Idara
katika fani za Uhasibu, Katibu muhutasi na Ustawi wa Jamii.
180.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014,
Idara ya Chuo cha Mafunzo imekusudia kutekeleza malengo yafuatayo:-
(i) Kuimarisha huduma bora za
urekebishaji tabia kwa wanafunzi, kuwaendeleza na kuwajengea uwezo wanaporudi
katika jamii;
(ii) Kuhakikisha haki za binadamu
zinatolewa kwa wanafunzi na wale walioko rumande kwa mujibu wa Sheria za nchi,
kikanda na makubaliano ya Kimataifa;
(iii) Kuweka mazingira mazuri
ya kazi, maendeleo na ustawi wa maafisa na wapiganaji pamoja na usimamizi mzuri
wa fedha; na
(iv) Kuendelea na ujenzi wa
Chuo kipya cha Mafunzo Hanyegwa Mchana.
181. Mheshimiwa Spika,
ili Idara ya Chuo cha Mafunzo iweze kutekeleza malengo yake kwa ufanisi, kwa
mwaka wa fedha wa 2013/2014, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS. 6,099.0
milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida na TZS. 300.0 milioni kwa mradi wa
maendeleo.
KIKOSI CHA ZIMAMOTO
NA UOKOZI ZANZIBAR (KZU)
182.
Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013,
Kikosi cha Zimamoto na Uokozi kiliidhinishiwa TZS. 3,099.0 milioni kwa matumizi
ya kazi za kawaida na hadi mwezi Machi,
2013 Kikosi kimeingiziwa TZS. 2,126.0 milioni sawa na asilimia 68.6 ya makadirio
ya matumizi.
183.
Mheshimiwa
Spika, jitihada zinaendelea za
kujenga vituo vya zimamoto katika kila Wilaya. Jumla ya vituo vitatu vimeanzishwa
na kutoa huduma. Vituo hivyo ni Mwanakwerekwe Wilaya ya Magharibi Unguja, eneo
la Bandarini Unguja na eneo la Bandarini Mkoani Pemba. Kituo cha bandari ya
Mkoani kwa sasa kitakuwa kikitoa huduma za zimamoto na uokozi katika Wilaya ya
Mkoani na maeneo jirani. Hatua za ujenzi wa Kituo cha Marumbi Wilaya ya Kati
zimeanza. Aidha, hatua zitachukuliwa za kupatikana eneo katika Wilaya za
Micheweni na Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba pamoja na Wilaya ambazo huduma hizi
hazijafika.
184.
Mheshimiwa Spika, Idara
imewapatia sare Maafisa wake, vyakula kwa askari wanaolala kambini na waliopo
mafunzoni na dawa kwa matumizi ya Maafisa na Wapiganaji wa Kikosi. Aidha, wapiganaji
na maofisa 77 wamepatiwa mafunzo ndani na nje ya nchi. Mafunzo hayo ni katika
fani za Uongozi Mkubwa, Uongozi Mdogo, Uzimaji moto, Matumizi ya Kompyuta,
Masjala, Sheria na Fedha.
185.
Mheshimiwa
Spika, Kikosi kimeendelea kufanya matengenezo
ya mara kwa mara ya magari yaliopo pamoja na kununua vipuri na vitendea kazi
vikiwemo; “Foam compound”, “Carbon Dioxide”, “Delivery
Horse 35 na B.A”. Aidha, Kikosi kimenunua jumla ya gari tatu za kuzimia moto na
gari moja ya kuchukulia wagonjwa. Malipo ya asilimia 75 ya gharama za ununuzi wa
gari hizo yameshafanywa.
186.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka
wa fedha 2013/2014, Kikosi cha Zimamoto na Uokozi kimelenga kutekeleza malengo yafuatayo:-
(i) Kupunguza muda wa kuwahi
kufika katika tukio la moto na majanga mengine bila ya kuzidi dakika 15;
(ii) Kuboresha ujenzi wa vituo
na kupatikana vifaa vya kazi vituoni ili kuleta ufanisi wa huduma zinazotolewa;
(iii) Kuwapa motisha
wafanyakazi ili kukuza ufanisi na tija kwa aina ya huduma zinazotolewa nchini;
(iv) Kuboresha Rasilimali Watu
kwa kuwapatia Maafisa na Maaskari elimu za aina mbali mbali;
(v) Kuendelea kutoa elimu ya
tahadhari za moto; na
(vi) Kuongeza uhusiano na
mashirikiano ya namna ya kukabiliana na majanga mbalimbali Kitaifa na Kimataifa.
187. Mheshimiwa
Spika, ili Kikosi cha Zimamoto na
Uokozi kiweze kutekeleza malengo yake kwa ufanisi, kwa mwaka wa fedha
2013/2014, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS. 3,113.0 milioni kwa
matumizi ya kazi za kawaida.
KIKOSI CHA VALANTIA
ZANZIBAR (KVZ)
188.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka
wa fedha 2012/2013, Kikosi cha Valantia kilitengewa TZS. 3,784.0 milioni kwa matumizi ya kazi za kawaida na TZS. 100.0
milioni kwa matumizi ya kazi za maendeleo. Hadi mwezi Machi 2013, Kikosi cha
Valantia kimeingiziwa TZS. 2,224.0 milioni sawa na asilimia 58.8 ya fedha
zilizoidhinishwa kwa matumizi ya kawaida na TZS. 40.0 milioni sawa na asilimia
40.0 kwa matumizi ya mradi wa maendeleo.
189.
Mheshimiwa Spika, Kikosi
cha Valantia kimeendelea kuimarisha nguvu za ulinzi na usalama kwa kuwapatia
chakula cha kutosha askari wanaokaa zamu katika kambi zote za Kikosi. Aidha,
Kikosi kimeendelea kusimamia masuala ya usafiri ili kuimarisha shughuli za
ulinzi na utawala.
190.
Mheshimiwa Spika, Kikosi
kimeendelea kuwajengea uwezo wa kiutendaji Maafisa na Wapiganaji wake ndani na nje
ya Kikosi. Katika kipindi hiki Kikosi kimedhamini mafunzo kwa askari sita
katika ngazi ya Stashahada na Shahada. Aidha, dawa kwa ajili huduma za afya kwa
askari na raia zimenunuliwa pamoja na ununuzi wa gari mbili aina ya Land Rover.
Kikosi kimekamilisha malipo ya gharama
za uungaji wa umeme katika kambi ya Ndugukitu ilioko Pemba. Pia, Kikosi kimenunua
sare seti 127 kwa ajili ya matumizi ya maafisa na askari wake.
191.
Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka wa fedha 2013/2014, Kikosi cha Valantia kina mpango wa kutekeleza malengo
yafuatayo:-
(i) Kuimarisha nguvu za
ulinzi na usalama;
(ii) Kuwaongezea uwezo wa
kiutendaji wapiganaji wa kikosi cha Valantia;
(iii) Kuandaa mazingira mazuri
ya utendaji kazi kwa wapiganaji wa kikosi cha Valantia;
(iv) Kuendeleza ujenzi pamoja
na kuyapatia hatimiliki maeneo ya Kikosi ya Unguja na Pemba; na
(v) Kuhakikisha wafanyakazi
wanawajibika ipasavyo.
192.
Mheshimiwa Spika, ili
Kikosi cha Valantia kiweze kutekeleza malengo yake kwa ufanisi, kwa mwaka wa
fedha 2013/214, naliomba Baraza lako Tukufu liidhinishe TZS. 3,258.0 milioni kwa
matumizi ya kazi za kawaida na TZS. 70 milioni kwa matumizi ya mradi wa
maendeleo.
MIRADI YA MAENDELEO YA
OFISI YA RAIS NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI
193. Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha
2012/13, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ilipanga kutekeleza
Miradi minane ya maendeleo na fedha zilizotengwa kwa Miradi hiyo ni TZS. 1,906.0
milioni. Miradi yenyewe ni kama ifuatavyo:-
i)
Mradi wa Uimarishaji Nyumba za Viongozi na Nyumba za Serikali
194.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa
Uimarishaji Nyumba za Viongozi na Nyumba za Serikali uliidhinishiwa TZS. 400.0
milioni na hadi kufikia Machi 2013, Mradi huu uliingiziwa TZS. 306.9 milioni
ambazo ni sawa na asilimia 76.7 ya makadirio ya matumizi na kutekeleza kazi
zifuatazo:-
(i) Matengenezo ya Ikulu ya
Mkoani yapo katika hatua za mwisho kukamilika;
(ii) Ujenzi wa ghala katika
Ikulu Kuu ya Mnazi mmoja nao umekamilika;
(iii) Ikulu ndogo ya Laibon Dar
es Salaam imefanyiwa matengenezo kwa kuwekewa malighafi maalumu ya kuziba paa
la zege ili kuzuia kuvuja; na
(iv) Ikulu ya Dodoma
imefanyiwa matengenezo makubwa ya vyoo.
195.
Mheshimiwa Spika, kwa
mwaka wa fedha 2013/2014, Mradi wa Uimarishaji Nyumba za Viongozi na Nyumba za
Serikali umetengewa TZS. 600.0 milioni na umepanga kutekeleza kazi zifuatazo:-
(i)
Kuanza ujenzi wa nyumba
za walinzi katika Ikulu ya Laibon Dar es
Salaam;
(ii)
Kufanya ukarabati wa
Ikulu ya Chake Chake;
(iii)
Kufanya matengenezo
katika Ikulu Kuu ya Mnazi Mmoja yakiwemo kubadilisha madirisha ya zamani;
(iv)
Kujenga ukuta wa
nyumba zilizokuwa za Posta katika Ikulu ya Migombani;
(v)
Kujenga ukuta wa
kuzuia mmong’onyoko katika Ikulu ya Mkoani;
(vi)
Kujenga ukuta wa
Ikulu ndogo Mkokotoni; na
(vii) Kuendeleza
ujenzi wa nyumba ya mapumziko ya Micheweni.
ii)
Mradi wa Kuimarisha Mawasiliano - Ikulu
196. Mheshimiwa
Spika, Mradi wa Kuimarisha
Mawasiliano – Ikulu uliidhinishiwa TZS. 100.0 milioni na hadi kufikia Machi
2013, Mradi huu uliingiziwa TZS. 13.3 milioni ambazo ni sawa na asilimia 13.3
ya makadirio ya matumizi na kutekeleza kazi zifuatazo:-
(i)
Hatua za awali za ukarabati wa chumba cha kutayarishia vipindi katika Ofisi ya Rais na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi zimeanza.
197.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka
wa fedha 2013/2014, Mradi wa Kuimarisha Mawasiliano – Ikulu umetengewa TZS. 150
milioni na utatekeleza kazi zifuatazo:-
(i) Ununuzi
wa Gari la matangazo kwa ajili ya huduma za Rais Pemba; na
(ii) Ununuzi
wa vifaa vya matangazo.
iii)
Mradi wa Uimarishaji wa Serikali za Mitaa
198.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa
Uimarishaji wa Serikali za Mitaa uliidhinishiwa TZS. 150.0 milioni na hadi
kufikia Machi 2013, Mradi huu uliingiziwa TZS. 46.9 milioni ambazo ni sawa na
asilimia 31.3 ya makadirio ya matumizi na kutekeleza kazi zifuatazo:-
(i) Utayarishaji
wa Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Sera;
(ii) Utayarishaji
wa muongozo na Rasimu ya Sheria ya Serikali za Mitaa;
(iii) Kufanya
mapitio ya vyanzo vya mapato vya Serikali za Mitaa; na
(iv) Semina
za Wadau kujadili utekelezaji wa Sera ya Serikali za Mitaa ikiwemo Semina kwa
Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
199.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka
wa fedha 2013/2014, Mradi wa Uimarishaji wa Serikali za Mitaa umetengewa TZS.
150 milioni na utatekeleza kazi zifuatazo:-
(i) Kuandaa
Kanuni za Sheria ya Serikali za Mitaa;
(ii) Kufanya
tathmini ya mahitaji ya watumishi katika Serikali za Mitaa;
(iii) Kuhakiki
mipaka ya Mamlaka ya Mikoa na Serikali za Mitaa; na
(iv) Kufanya
tathmini na kuandaa mfumo, utaratibu na miongozo ya fedha.
iv)
Mradi wa Kiwanda cha Ushoni (Zanzibar Quality Tailoring LTD)
200. Mheshimiwa
Spika, Mradi wa “Zanzibar Quality
Tailoring Ltd” uliidhinishiwa TZS. 256.0 milioni na hadi kufikia Machi 2013,
Mradi huu uliingiziwa TZS. 5.8 milioni ambazo ni sawa na asilimia 2.3 ya
makadirio ya matumizi na kutekeleza yafuatayo:-
(i)
Kugharamia shughuli za uendeshaji wa kiwanda zikiwemo ununuzi wa vifaa
vidogo vidogo kama mikasi na nyuzi za kushonea.
201.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka
wa fedha 2013/2014, Mradi wa Kuimarisha Kiwanda cha Ushoni umetengewa TZS. 350.0
milioni na utatekeleza kazi zifuatazo:-
(i) Ununuzi
wa vifaa pamoja na kutafuta malighafi za uzalishaji; na
(ii) Kujenga
uwezo wa watendaji na kiwanda.
v)
Mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya KMKM
202.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa
Ujenzi wa Hospitali ya KMKM uliidhinishiwa TZS. 200.0 milioni na hadi kufikia
Machi 2013, Mradi huu uliingiziwa TZS. 115.0 milioni ambazo ni sawa na asilimia
57.5 ya makadirio ya matumizi na kutekeleza yafuatayo:-
(i) Ujenzi
umeendelea kwa hatua za kumalizia ambapo kazi zilizofanyika ni upigaji plasta,
uwekaji wa dari na ununuzi wa vigae; na
(ii) Uezekaji
wa jengo litakalotumika kwa ajili ya kufulia nguo.
203. Mheshimiwa
Spika, kwa mwaka wa fedha wa
2013/2014, Mradi wa Ujenzi wa
Hospitali ya KMKM utakuwa umekamilika.
vi)
Mradi wa Ujenzi wa Chuo cha Mafunzo
204.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa
Ujenzi wa Chuo cha mafunzo uliidhinishiwa TZS. 400.0 milioni na hadi kufikia
Machi 2013, Mradi huu uliingiziwa TZS. 145.0 milioni ambazo ni sawa na asilimia
36.3 ya makadirio ya matumizi na kutekeleza yafuatayo:-
(i) Malipo
ya Mshauri Elekezi na msimamizi wa ujenzi; na
(ii) Ujenzi
wa msingi unaozunguka eneo la Chuo Kipya cha Mafunzo, nguzo za ukuta mkubwa na
uzio.
205.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Mradi
wa Ujenzi wa Chuo kipya cha Mafunzo Hanyegwa Mchana
umetengewa TZS. 300.0 milioni na utatekeleza kazi zifuatazo:-
(i) Kujenga ukuta wa urefu wa mita 600 wenye kimo cha mita 1.5;
(ii) Kujenga msingi jengo la watoto;
(iii) Kufanya malipo ya Mshauri Elekezi; na
(iv)
Kufanya
malipo ya mafuta na matengenezo ya zana
vii)
Mradi wa Ujenzi wa Makao Makuu ya Valantia
206. Mheshimiwa
Spika, Mradi wa Ujenzi wa Makao
Makuu ya Valantia uliidhinishiwa TZS. 100.0 milioni na hadi kufikia Machi 2013,
Mradi huu uliingiziwa TZS. 40.0 milioni ambazo ni sawa na asilimia 40.0 ya
makadirio ya matumizi na kutekeleza yafuatayo:-
(i)
Ujenzi wa mesi na
ukumbi wa mikutano umefikia hatua ya juu na unasubiri kuezekwa.
207.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Mradi
wa Ujenzi
wa Makao Makuu ya Valantia umetengewa TZS. 70.0 milioni na utatekeleza kazi
zifuatazo:-
(i) Kuanza ukarabati Mkubwa wa nyumba Namba 1900; na
(ii) Kumaliza Ujenzi wa Ukumbi wa Mikutano.
viii)
Mradi wa Shamba la Mfano la Pamoja - Bambi
208.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Shamba la Mfano
la Pamoja - Bambi ambao unatekelezwa kwa pamoja baina ya Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar na Serikali ya Misri. Utekelezaji wake haukufanyika kutokana na kutoingiziwa
fedha.
209.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka
wa fedha 2013/2014, Mradi wa Shamba la Mfano la Pamoja - Bambi umetengewa
TZS. 250.0 milioni na utatekeleza kazi zifuatazo:-
(i) Kukamilisha ujenzi wa nyumba moja;
(ii) Kuendeleza Shamba la Bambi;
(iii) Kufanya ukarabati wa nyumba ya Wataalamu; na
(iv) Kujenga ghala jipya la kisasa.
MAMLAKA YA SERIKALI
ZA MITAA
210. Mheshimiwa
Spika, Serikali za Mitaa ndio mhimili mkubwa
wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali katika lengo zima la kuhakikisha
yanakuwepo maendeleo endelevu katika nchi yetu. Katika kufanisha azma hiyo,
Serikali kupitia Mpango wa Mageuzi ya Serikali za Mitaa imedhamiria kuziwezesha
Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoa huduma bora kwa wananchi. Hata hivyo, jukumu
hilo haliwezi kutekelezeka iwapo Serikali hizi hazitokuwa na wataalamu, pia
hazitaweza kuongeza mapato na kuwa na nidhamu katika matumizi. Hivyo, mkazo
uliwekwa katika kuimarisha mfumo wa
ukusanyaji mapato. Kwa mfano, kwa mwaka wa fedha 2012/2013, Baraza la Manispaa
limeendesha zoezi la kutathmini viwango vya leseni na thamani za nyumba ili
kuwa na takwimu sahihi za walipa kodi (tax payers).
211. Mheshimiwa
Spika, kutokana na
hali hiyo, Serikali itaimarisha usimamizi wa mapato na matumizi katika Serikali
za Mitaa. Hivyo, Taasisi hizo zinawajibu wa kuhakikisha kuwa Sheria, Kanuni na
Taratibu za Fedha zinazingatiwa. Aidha, Ofisi yangu itahakikisha Serikali za
Mitaa zinaongeza uwazi katika mapato na matumizi ili kuwawezesha wananchi
kushiriki katika kupanga, kufuatilia na kutathmini Mipango na utekelezaji
kulingana na vipaumbele vyao.
212. Mheshimiwa
Spika, Serikali imeendeleza
juhudi za kuimarisha usafi katika Manisapaa ya Zanzibar. Katika kufanikisha
hilo, Baraza la Manispaa limefanya malipo kwa Taasisi saba za kijamii na Polisi
Jamii ambazo imeingia nazo mkataba wa kutoa huduma za kufanya usafi katika
maeneo ya masoko, barabara, misingi ya maji machafu na maji ya mvua kwa kutumia
utaratibu wa ‘Out Sourcing’. Utaratibu huu shirikishi umesaidia sana kuimarisha
huduma za uzoaji taka katika maeneo mbali mbali ya Manispaa.
213. Mheshimiwa
Spika, maelezo ya
kina ya utekelezaji wa malengo ya Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2012/2013,
ukusanyaji wa mapato na malengo yatakayotekelezwa kwa mwaka wa fedha 2013/2014
yameainishwa katika kitabu cha “Majadweli ya
Utekelezaji wa Malengo ya Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013 na
Malengo ya Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2013/2014”
JUMLA YA MAPATO NA MATUMIZI
YA OFISI YA RAIS NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI
214.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka
wa fedha 2012/2013, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi ilipangiwa kukusanya jumla ya TZS.
66.5 milioni. Kati ya fedha hizo, TZS. 25.5 milioni zilipangwa kukusanywa na
Kikosi cha Jeshi la Kujenga Uchumi, hadi kufikia Machi 2013, JKU ilikusanya TZS.
8.0 milioni sawa na asilimia 31.4. Chuo cha Mafunzo, kilipangiwa kukusanya TZS.
41.0 milioni, hadi Machi 2013, ilikusanya TZS 10.0 milioni sawa na asilimia 24.4.
215.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka
wa fedha 2012/2013, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi ilikadiriwa kutumia jumla ya TZS.
48,560.1 milioni. Kati ya hizo, TZS. 44,516.1 milioni kwa kazi za kawaida, TZS.
1,906.0 milioni kwa kazi za maendeleo na TZS. 2,138.0 milioni kwa ajili ya Ruzuku
za Baraza la Manispaa na Mabaraza ya Miji ya Mkoani, Chake Chake na Wete. Hadi
kufikia Machi 2013, Ofisi ilikuwa imeshaingiziwa TZS. 28,741.9 milioni sawa na
asilimia 64.6 kwa kazi za kawaida, TZS. 672.9 milioni sawa na asilimia 35.3 kwa
kazi za maendeleo na TZS. 1,575.7 milioni sawa na asilimia 73.7 kwa ajili ya Ruzuku
(Kiambatanisho Nambari 11, 12 na 13).
216.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2013/2014, Ofisi
ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi inatarajia kukusanya jumla ya TZS. 121.3 milioni,
kati ya fedha hizo, TZS. 25 milioni
zitakusanywa na Kikosi cha Jeshi la Kujenga Uchumi, TZS. 41 milioni
zitakusanywa na Chuo cha Mafunzo, TZS. 15.8 milioni zitakusanywa na Kikosi
Maalum cha Kuzuia Magendo, TZS. 10 milioni zitakusanywa na Kikosi cha Zimamoto
na Uokozi na TZS. 7 milioni zitakusanywa na Kikosi cha Valantia. Fedha zitakazokusanywa na Ofisi ya
Usajili na Kadi za Utambulisho
ni
22.5 milioni.
217. Mheshimiwa
Spika, ili Ofisi
ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi iweze
kutekeleza majukumu na malengo yake ya mwaka wa fedha 2013/2014, naomba sasa
Baraza lako Tukufu liidhinishe jumla ya TZS. 49,819.9 milioni. Kati ya hizo, fedha za matumizi ya kazi za kawaida ni TZS.
45,888.9 milioni sawa na asilimia 92.1, TZS. 1,870.0 milioni kwa ajili ya
matumizi ya maendeleo sawa na asilimi 3.8 na TZS. 2,061.0 milioni sawa na
asilimia 4.1 kwa ajili ya Ruzuku kwa Baraza la Manispaa na Mabaraza ya Miji ya
Chake Chake, Mkoani na Wete (Kiambatanisho Nambari 11, 12 na 13).
HITIMISHO
218.
Mheshimiwa Spika, kwa mara
nyengine tena nachukua fursa hii kuwashukuru wote Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza
la Wawakilishi kwa mashirikiano yenu makubwa mnayoendelea kutupatia wakati
wote. Kama nilivyosema mwanzoni, mafanikio
ya utekelezaji wa majukumu na malengo ya Ofisi ya Rais
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi yamewezekana
kutokana na ushirikiano wenu. Shukurani zangu za pekee ziende kwa Viongozi na
Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambao wamekuwa wakinipa msaada mkubwa katika kutekeleza
majukumu ya kila siku ya Ofisi hii.
219.
Mheshimiwa Spika, kwa dhati
kabisa naomba nitumie fursa hii tena kuwashukuru washirika wetu wote wa maendeleo
ambao wametuunga mkono wakati wote wa kutekeleza majukumu ya Ofisi yetu. Shukurani
hizi ziwaendee washirika wetu wote wa maendeleo nikitarajia kuwa wataendelea na
moyo huo huo. Sio rahisi kuwataja wote lakini nitaje wachache ambao ni Serikali
ya Jamhuri ya Watu wa China, Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Korea, India, Mashirika
ya Kimataifa yakiwemo Benki ya Dunia (WB), Shirika la Mpango wa Maendeleo la
Umoja wa Mataifa (UNDP) na Shirika la Uhamiaji la Kimataifa (OIM).
220.
Mheshimiwa Spika, napenda
nitoe tena shukurani zangu za dhati kwako binafsi na kwa Waheshimiwa Wajumbe
wote wa Baraza lako Tukufu kwa kunisikiliza.
221. Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja.
(Dkt. Mwinyihaji Makame)
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Zanzibar
No comments:
Post a Comment