Ramani halisi itakavyokuwa Hoteli ya Daraja la Saba ya Kampuni ya Kimataifa ya ASB Holding’s inayojengwa katika eneo la ilipokuwa Starehe Club Pembezoni mwa Fukwe ya Forodha Mchanga.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar Nd. Issa Sarboko Makarani akimuonyesha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ramani ya ujenzi wa Hoteli ya Daraja la Saba hapo Forodha Mchanga inayojengwa na Kampuni ya Kimataifa ya ASB Holding’s.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, makazi, Maji, Nishati na Madini Nd. Al -Khalil Mirza akimsisitiza Mwakilishi wa Kampuni ya ASB Holding’s Bwana Ali Al-Bwardy kuzingatia kufuatwa kwa taratibu za hifadhi ya Mji Mkongwe kwenye ujenzi wa Hoteli yao iliyopo eneo la Forodha Mchanga mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif.
Pembeni yao ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar Nd. Issa Sarboko Makarani.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akisalimiana na Wafanyakazi wa Ujenzi wa Hoteli ya Daraja la Saba iliyopo maeneo ya Forodha Mchanga hawapo Pichani wakati alipofanya ziara fupi kukagua ujenzi huo.
Pembeni yake ni Mwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa itayoendesha Hoteli hiyo ya ASB Holding’s Bwana Ali Al- Bwardy.
Jengo la Hoteli ya Kimataifa ya Daraja la Saba la Kampuni ya ASB Holding’s linalojengwa na Kampuni ya Kimataifa ya CRJ ya China liliopo katika eneo la Forodha Mchnga.
Picha na Hassan Issa wa -OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Hoteli Mpya ya Daraja la Saba { Grand Hyatt } inayomilikiwa na Kampuni ya Kimataifa ya ASB Holding’s ambayo inajengwa katika eneo lililokuwa Starehe Club ndani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar inatarajiwa kufunguliwa rasmi katika sherehe za Maadhimisho ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar za mwaka 2014.
Ujenzi wa Hoteli hiyo unaofanywa na Kampuni ya Kimataifa ya CRJ kutoka Nchini china unatazamiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka huu ambapo zaidi ya ajira za wazalendo kati ya 60 na 100 zitatolewa wakati itakapoanza kazi zake rasmi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifanya ziara fupi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hoteli hiyo ili kupata sura halisi ya Ujenzi huo kufuatia kupokea malalamiko mengi kutoka kwa baadhi ya watu na taasisi dhidi ya ujenzi huo kwa dhana ya kukiukwa kwa matakwa ya hifadhi ya Mji Mkongwe.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar Nd. Issa Sarboko Makarani alimueleza Balozi Seif kwamba Jengo la Hoteli hiyo litakalokuwa na ghorofa tatu linazingatia kubakisha sura ile ile ya haiba ya nyumba zilizomo ndani ya Mji mkongwe.
Nd. Sarboko alisema Uongozi wa Kampuni ya ASB utapaswa pia kuzingatia ujenzi wa ukuta maalum wa mita tatu kama yalivyo majengo mengine ya Mji mkongwe yaliyo pembezoni mwa bahari ili kusaidia kunusuru athari yoyote ya maji, Mazingira au matukio ya dhoruba yanapotokea wakati wowote.
Alisema hatua zote hizo zinachukuliwa sambamba na matakwa ya Umoja wa Mataifa kupitia Shirika lake la Elimu sayansi na Utamaduni { UNECSO } juu ya hifadhi ya Mji mkongwe wa Zanzibar ambao umo katika makubaliano ya Hifadhi ya Kimataifa.
Naye Mwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa ya ASB Holding’s Bwana Ali Al-Bwardy alifahamisha kwamba Uongozi wa Hoteli hiyo utazingatia matumizi bora na sahihi ya fukwe iliyopo pembezoni mwa Hoteli hiyo bila ya kuathiri matumizi ya Wananchi kwa utaratibu maalum utakaoandaliwa.
Bwana Ali Al – Bwardy alisema uongozi wa Kampuni yake ya ASB unaelewa kwamba eneo la fukwe ni la Serikali ambalo Jamii inafursa ya kulitumia wakati wowote wanapolihitaji kwa shughuli zao za kila siku ikiwemo michezo au hata mapumziko.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa nasaha zake mara baada ya kuangalia harakati hizo za ujenzi alieleza kuridhika kwake na taratibu za ujenzi zinazochukuliwa na Kampuni hiyo ya ASB Holding’s.
Balozi Seif alisema kwamba amechukuwa hatua hiyo ya kukagua ujenzi huo kufuatia malalamiko aliyokuwa akiyapokea kutoka kwa baadhi ya Watu na Taasisi tofauti yakiishutumu Kampuni hiyo kukiuka taratibu za ujenzi ndani ya eneo la hifadhi ya Mji Mkongwe.
“ Nimeridhika na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Kampuni yenu ya ASB Holding’s katika ujenzi huu wa Hoteli kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe. Sina shaka nao na mnaweza kuendelea na Ujenzi kama kawaida. Sasa kama kuna asiyeridhika mnaweza kumuelekeza kuja kwangu “.Alisisitiza Balozi Seif.
No comments:
Post a Comment