Habari za Punde

NBC : Kuanzishwa huduma za benki za kiislamu ni kukidhi mahitaji ya wateja

Na Said Ameir. Ikulu

Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Taifa ya Biashara-NBC Dk. Mussa Assad amesema lengo la kuanzishwa kwa huduma za benki ya kiislamu katika benki hiyo ni kukidhi mahitaji ya wateja wao ambayo kwao ni ibada.

Dk. Assad ameeleza hayo jana wakati akizungumza kwenye hafla ya futari ambayo iliandaliwa na benki hiyo kwa wateja wao wa Zanzibar.

Mgeni Rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye hoteli ya Zanzibar Beach Resort mjini Unguja alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

Wengine waliohudhuria ni pamoja na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho, Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Mufti Mkuu wa Zanzibar pamoja na viongozi wengine.

“Tumefungua huduma za benki ya kiislamu kwa kusikiliza mahitaji ya wateja wetu. Tunafahamu kuwa huduma hii ni ibadi kwa wateja wetu waumini wa dini ya kiislamu”alisema Dk. Assad na kusisitiza kuwa daima benki hiyo imekuwa sikivu kwa wateja wake.

Aliongeza kuwa muda si mrefu benki hiyo itaanzisha huduma nyingine mpya ambazo lengo lake kuu ni kukidhi mahitaji mbalimbali ya wateja wake.

“tunaelewa wateja wetu mna mahitaji mbalimbali na ninawaomba msisite kutueleza shida zenu na sisi tutawasikiliza na kuzuitafutia ufumbuzi ” alieleza.

Awali akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Bi. Mizinga Melu alisema kuwa kuwepo kwa benki hiyo humu nchini hakutakuwa na maana kama benki haitaweza kuwasaidia wateja wake kukidhi mahitaji yao.

Amesema kwa kutambua hilo ndio maana pamoja na kuanzisha huduma za benki ya kiislamu imeongeza pia huduma kwa wateja wanaotaka kufanya safari za Hija.

“miaka mitatu iliyopita tulianzisha huduma za benki ya kiislamu na mwitikio umekuwa mkubwa pasi na matarajio yetu na hivyo tumefurahi kwa kuwa tumeweza kukidhi mahitaji ya wateja wetu kwani hiyo ndio azma yetu” alisema Bi Melu.

Aliongeza kuwa mpango wa benki yake sasa ni kuongeza huduma zaidi ili wateja waweze kupata kila huduma ya kifedha wanazohitaji.

Mkurugenzi Mtendaji huyo aliwaeleza wageni waalikwa na viongozi walihudhuria hafla hiyo kuwa benki yake inaunga mkono jitihada za Serikali za kuwatelea wananchi maendeleo. 

Aliwashukuru wateja wa benki hiyo Zanzibar kwa ushirikiano wao na kueleza kuwa madhudhurio mazuri katika hafla hiyo ni kielelezo cha ushirikiano thabiti kati ya benki na wateja wake.

Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ameupongeza uongozi wa Benki ya Taifa ya Biashara wa kuandaa futari na kuwakutanisha wateja wa benki hiyo.

Akitoa shukrani hizo kwa niaba ya Rais, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Maghribi Abdalla Mwinyi amesema kitendo cha benki hiyo kuwakutanisha wateja wake katika hafla kama hiyo ni cha kiungwana na kinazidisha upendo baina ya benki na wateja.

“Kitendo chenu cha kutufutarisha kwa vyakula vya kila aina vyenye ladha asili ya visiwa vyetu imemvutia kila aliyefika hapa akiwemo Mheshimiwa Rais na viongozi wengine”alieleza Mkuu huyo wa Mkoa na kusisitiza kuwa huo ni ukarimu mkubwa wa kushukuriwa.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.