Na Mwantanga Ame
SERIKALI inajiandaa kuweka sera maalum itakayosimamia mahitaji ya watumishi wastaafu, ili kuondoa malalamiko kutoka kwa watumishi wa serikali.Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, aliyasema hayo wakati akizindua Jumuiya ya Wastaafu Pemba, hafla iliyofanyika ofisi ya Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC), Wawi.
Alisema serikali imeamua kuweka sera hiyo kwa dhamira ya kuendelea kuwathamini wastaafu kutokana na mchango walioutoa wa kujenga taifa hilo wakiwa watumishi serikalini.
Alisema sera hiyo kwa kiasi kikubwa itaonesha mambo yanayotakiwa wastaafu kufaidika nayo huku ikiangalia namna itakavyowezesha kuwashirikisha na wastaafu wa Muungano kwa baadhi ya mambo.
Alisema serikali imeamua kuweka sera hiyo, kwa kuzingatia mchango wa wastaafu bado ni mkubwa na uwezo walionao unahitaji kuendelezwa.
Alisema kitendo cha wastaafu kuamua kuunda umoja wao ni jambo la msingi kwani watajiendeleza kimaisha kupitia miradi watakayobuni.
Alisema jumuiya nyingi ziliopo nchini zinapata mafanikio na kuja kwa jumuiya hiyo, kutawezesha kuamsha ari ya kujituma kwa kuanzisha SACCOS yenye nguvu kimaendeleo.
Alisema serikali itahakikisha inawapatia misaada katika kukuza jumuiya hiyo kupitia Idara ya uwezeshaji ikiwa pamoja kuwasimamia kupata mikopo katika mabenki.
Aliwapongeza wanajumuiya hiyo na kuahidi kuendelea kushirikiana nao kwa kukubali kuendelea kuwa mlezi wa Jumuiya.
Nae Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba, Juma Kassim Tindwa, alisema upo uchelewaji wa malipo ya mafao ya uzeeni, tatizo linalochangiwa na maofisa utumishi kushindwa kuyapa kipaumbele madai ya wastaafu.
Hata hivyo, aliwapongeza wastaafu hao na kuwataka waendelee kushirikiana na serikali yao kwa kutoa mchango wao wa kuimarisha taifa.
Mapema wakisoma risala yao wastaafu hao 33, walisema bado serikali inastahiki kuyaangalia mahitaji yao.

No comments:
Post a Comment