Na Mariam Kamgisha, MOROGORO
KAMATI ya maafa ya kijiji cha Magole
wameilalamikia kamati ya maafa ya wilaya ya Kilosa kwa kushindwa kuwafikishia
misaada wanayopewa waathirika wa mafuriko.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi
aliyetembelea kambi ya waathirika wa mafuriko iliyopo skuli ya sekondari Magole baadhi yaa wajumbe
na waatrhirika hao walidai pamoja na kushuhudia misaada ikitolewa,bado
hawapatiwi chakula cha kutosha na kwa wakati.
Walidai chakula wanachopewa ni kidogo na
kisichotosheleza mahitaji, huku kingine wakishuhudia kikiondoka bila kuelezwa
wala kujua ni wapi kinapopelekwa.
Mwenyekiti wa kamati ya maafa wa kijiji cha
Magole, Ally Ngulungu, alisema mpaka sasa waathirika wanaishi katika hema moja
watu wanane ukiondoa watoto.
Alisema waathirika wanaokaa kambini pekee ndio
wanaopatiwa huduma ya chakula cha msaada,ambapo alidai waathirika
waliohifadhiwa na jamaa,maraiki na ndugu hawapatiwi msaada wowote.
“Tangu kutokea kwa mafuriko mahema yaliyokuja
kambini ni 24 tu leo ndio unaona hivi ujenzi wa mahema unafanyika ili kupunguza
idadi ya watu katika hema moja,cha kushangaza zaidi ni kamati ya maafa ya wilaya
kutotushirikisha sisi kamati ya kijiji,tunapata wasiwasi chakula na mahitaji
mengine yanapokwenda,”alisema.
“Tangu maafa kutokea ni kilo 24.5 ndizo tulizopewa
na hizo tunaambiwa ni kwa mwezi mmoja,hivi ndugu mwandishi kilo hizo kwa mwezi
mzima zinatosheleza kweli,wakati tunasikia watu wengi wanatoa misaada,”alisema.
Waathirika wa mafuriko hayo Shabani Ndunda,Kigolo
Abdallah na Idd Chidako, kwa nyakati tofauti waliitaka serikali kuwa na uazi
wakati wa ugawaji wa misaada ili kuondoa hofu kwa waathirika.
Pamoja na kushukuru kwa misaada inayotolewa na
wahisani,waliishauri serikali kuwasaidia ujenzi wa nyumba za kudumu, badala ya
kuendelea na ujenzi wa mahema.
Akizungumzia madai yaliyotolewa na waathirika hao
mkuu wa mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, alisema misaada inayotolewa na wahisani inahifadhiwa katika ghala maalumu
kwa maandishi na kutolewa kwa utaratibu kwenda
kwa waathirika.
Aliwaondoa hofu Watanzania kuhusu misaada ya
waathirika wa mafuriko kwa madai kuwa ugawaji wa chakula cha msaada umepangwa
kwa kuzingatia wilaya zote tatu zilizoathiriwa na mafuriko.
No comments:
Post a Comment