Habari za Punde

‘Saratani tishio Zanzibar’

Na Salum Vuai, MAELEZO
WAKATI dunia ikiadhimisha siku ya saratani juzi Februari 4, imeelezwa kuwa idadi ya watu wanaougua magonjwa hayo hapa Zanzibar inazidi kuongezeka na kuwa tishio kwa wananchi.

Akizungumza katika hafla ya kuadhimisha siku hiyo iliyofanyika makao makuu ya maradhi yasiyoambukiza (ZNCDA) Mpendae mjini Unguja, Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wanaoishi na Saratani Zanzibar, Dk. Msafiri Marijani, alisema maradhi hayo sasa yanashambulia hata watoto wadogo.

Alifahamisha kuwa, takwimu zinaonesha kuwa, kila mwaka watu wasiopungua 1,000 kutoka Zanzibar wanaokwenda kufanyiwa uchunguzi katika hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam, hugundulika na aina mbalimbali za saratani.

Hata hivyo, alitanabahisha kwamba idadi hiyo ni ndogo kwani wapo wanaokwenda kuchunguzwa na kupatiwa tiba katika hospitali nyengine nje ya nchi, pamoja na wengine wanaoishi na saratani bila kutambua maradhi yanayowasumbua.

Alitaja baadhi ya mambo yanayosababisha ongezeko la magonjwa hayo, kuwa ni pamoja na uelewa mdogo wa wananchi juu ya viashiria vyake, na kutochukua juhudi ya kupima pale wanapoona alama zisizo za kawaida katika miili yao, na hivyo kuripoti hospitalini wakiwa katika hatua mbaya.


Aidha alisema, utafiti unaonesha kuwa, saratani inaua watu wengi pengine huliko hata maradhi ya UKIMWI, ambayo dunia imeyaelekezea nguvu nyingi kuyashughulikia.  

“Saratani ni miongoni mwa magonjwa manne makubwa yasiyoambukiza ambayo yanaathiri watu wengi na kusababisha vifo vingi duniani, ikiwemo kisukari, moyo na pumu,” alifafanua.

Hivyo aliiasa jamii kutopuuza tafauti zozote zisizo za kawaida zinazojitokeza katika miili yao, na kuwashauri waende katika hospitali na vituo vya afya kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi ili kubaini kama wanaugua saratani au ugonjwa mwengine wowote.

Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Mwanakhamis Mohammed ambaye anaishi na saratani ya titi kwa miaka minne sasa, alisema iko haja kwa serikali kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya kuwasaidia wanaougua magonjwa hayo, kwani vipimo na tiba zake ni ghali sana.

Alieleza kuwa, watu wengi hapa Zanzibar wanaogua saratani lakini wanashindwa kumudu gharama hizo na kubaki wakiendelea kusumbuka, kwa kuwa dawa hazipatikani na hata pale wanapoandikiwa, hawawezi kuzinunua kutokana na kutokuwa na fedha.

Aidha alisema ukosefu wa vifaa vya kupimia hapa nchini, wataalamu na wagonjwa kuchelewa kufika hospitalini kwa matibabu ni matatizo mengine yanayohitaji nguvu za serikali na kutanua wigo wa kutoa elimu kwa jamii juu ya hatari ya ugonjwa huo.

Naye Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mohammed Said Mohammed, aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, alikiri kuwa saratani ni maradhi thakili yanayohitaji muamko wa wananchi na nguvu za pamoja kuyakabili.

Alisifu hatua ya kuundwa kwa jumuiya hiyo inayokusanya watu wanaoishi na maradhi hayo, akisema ni muhimu iungwe mkono na pia kutangazwa ili watu wafahamu hatari iliyo mbele yao inayotokana na saratani.

Pamoja na ughali wa vipimo na tiba ya saratani, Mhe. Said aliiasa jamii kuacha utamaduni wa kukwepa kwenda hospitali na kuamini katika dawa za kienyeji, ambazo badala ya kutibu, huenda zikawaongezea ukubwa wa matatizo.


Aliahidi kuiunga mkono jumuiya hiyo iliyoundwa mwezi Julai 2012, ili iweze kuimarika na kutambulika zaidi kwa kuandaa matukio mbalimbali yanayolenga kuizindua jamii juu ya haja ya kujali afya zao ili kujiweka mbali na magonjwa ya saratani na mengine.

3 comments:

  1. Munapiga porojo Tu. Sasa kwanini musianzishe kitengo cha maradhi ya saratani na mukasomesha vijana wetu. Ocean Road inawahusu nini. Munachoma taka ovyo, nchi haina trash recycling plant. Ma used yamejaza uchafu Zanzibar. Vyakula vibovu expired. Umasikini uliokisiri. Waziri wa uvuvi na saratani wapi na wapi. Wacheni siasa na wizi tujenge nchi. Tanganyika inatuacha nyuma kimaendeleo kutokana na uzalendo wa nchi Yao.

    ReplyDelete
  2. Mukisha wamaliza wananchi kwa njaa na umasikini. Mutawasukumia kwenye Faith Treatments. Nasikia siku hizi Kuna madawa ya sunna. Halafu muwaambie hivi ndivyo Mwenyezi Mungu alivyowajaalia.

    ReplyDelete
  3. Tusibabaishwe na hao wakurupukwaji wasemao bila kuzingatia wakisemacho. mambo ni mengi yaletayo maradhi. tufanye uchunguzi na kuiomba Serikali ichukue hatua. Kwa vile sasa tushapata Jumuia yetu ZNCDA, tushikamane tushirikiane na tusaidiane kupambana na maradhi haya yasioambuzika.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.