Habari za Punde

ZECO yailipa TANESCO 500m/- kila mwezi

Na Mwandishi wetu
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Madini na Nishati, Eliakim Maswi, amekanusha tuhuma za Shirika la Umeme (TANESCO) kwamba linaidai Zanzibar kiasi cha shilingi bilioni 47 kutokana na matumizi ya umeme.

Alisema wamekuwa wakipokea shilingi milioni 500 kila mwezi kutoka Shirika la Umeme Zanzibar, ikiwa ni malipo ya umeme  unaotumiwa Zanzibar.

Maswi alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya kuwasilisha mada kwa Wahariri na waandishi wa habari kuhusu mikakati inayochukuliwa kuhakikisha kunakuwa na uhakika wa umeme utakaokidhi matakwa ya Mradi wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) unaotazamiwa kuanza kutekelezwa mapema mwezi ujao hadi mwaka 2033.

“Kwanza niwaambie (waandishi wa habari),deni hili ni la zamani sana ila ,SMZ imekuwa ikilipa kila mwezi na hata hivi sasa tumepokea  shilingi milioni 500 za malipo ya umeme kwa Zanzibar tu,” alisema.


“Nawaambia mkawaambie wote wanaosema kwamba Zanzibar inadaiwa na TANESCO kuwa huo ni uongo na kama mtu hajafanya utafiti hana haki ya kuzungumza,” alisema.

Pia,aliwataka wananchi kutowasikiliza watu aliodai kuwa ni wanafiki kutokana na kuamua kuzungumzia mambo ya TANESCO  nje bunge.

Aliwataka wanasisasa  wanaosema kuhusu nishati na madini kuhakikisha  hawapotoshi ukweli.

Aidha alisema TANESCO na  Wizara ya Madini na Nishati, zimekubaliana kutekeleza mipango waliyojipangia ikiwa ni pamoja na kuhakikisha umeme unapatikana kwa uhakika na kwa bei nafuu ili ifikapo 2025  na asilimia 75 ya Watanzania  wawe wanatumia nishati hiyo.

Alisema,Juni 30 mwaka huu,wataipatia  TANESCO shilingi bililioni 80 ikiwa ni ruzuku kuhakikisha inapata uwezo wa kujiendesha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.