STATE HOUSE
ZANZIBAR
OFFICE OF THE
PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
13 Novemba,2014
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
WASHIRIKI
wa warsha ya mahusiano na mipaka kati ya viongozi wa kisiasa na kiutendaji wameahidi
kuyafanyia kazi mafunzo waliyoyapata na kusisitiza kuwa mabadiliko makubwa
yatarajiwe kutokea katika utendaji wao wa kazi ikiwa ni pamoja na kuendelea
kudumisha Muungano uliopo wa Tanganyika na Zanzibar.
Maelezo hayo waliyatoa katika ufungaji wa Warsha
hiyo ya siku tatu iliyowashirikisha Wakuu wa Mikoa, Wilaya pamoja na Maofisa
Tawala wa Mikoa na Wilaya wa Zanzibar na baadhi kutoka Tanzania Bara
iliyofanyika katika hoteli ya Sea Cliff nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Katika maelezo yao washiriki hao walieleza kuwa
warsha hiyo imewasaidia kwa kiasi kikubwa katika kutoa mwanga kwenye utendaji
wao wa kazi sambamba na kuwa chachu katika kufikia malengo waliyojiwekea.
Walieleza kuwa mbali ya mafunzo walioyoyapata pia,
warsha hiyo imeweza kujenga uhusiano na mashirikiano mazuri kati ya viongozi wa
Mikoa wa Zanzibar na wale wa Tanzania Bara hatua ambayo itaimarisha zaidi
Muungano uliopo kati ya pande mbili hizo.
Viongozi hao pia walipongeza juhudi za Dk. Shein
katika kuwaletea maendeleo wananchi anaowaongoza sambamba na ushauri na
miongozo mbali mbali anayotoa kwa viongozi akiwa na azma ya kuleta ufanisi
katika utekelezaji wa majukumu yao.
Pamoja na hayo, viongozi hao walipongeza hotuba ya
ufunguzi wa warsha hiyo iliyotolewa na Dk. Shein ambayo walieleza kuwa ilikuwa
ni dira katika mafunzo yao ya siku tatu.
Katika hutoba yake ya ufungaji, Waziri wa Nchi,
Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar Mhe. Haji Omar Kheir aliwataka washiki kuitumia warsha hiyo kuwa ni
fursa ya kuendeleza, kuimarisha na
kudumisha mashirikiano baina yao.
“Tushirikiane katika kubadilisha uzoefu kwa
kutembeleana na pia, kuanzisha na kutekeleza mipango na program za pamoja kwa
ajili ya kuwaletea maendeleo watu wetu katika maeneo yetu… mkutano huu uwe ni
kichocheo cha kudumisha Muungano wetu”alisema Mhe. Kheir.
Aidha, Mhe. Kheir alisema kuwa mafunzo hayo yamekuwa na umuhimu mkubwa sana
kwani yameonesha njia na mbinu za kukabiliana na changamoto zilizopo baina ya
viongozi wa kisiasa na kiutendaji katika Mikoa na Wilaya.
Alieleza kuwa lengo kubwa la warsha hiyo ni kuongeza
ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao na kueleza matumaini yake juu ya
warsha hiyo ni kuwa waliyojifunza yatapelekea kufikia lengo hilo hali
itakayothibitisha wazi pale itakapoonekana migogoro baina ya wanasiasa na
watendaji imepungua ama kumalizika kabisa, ambapo ndiyo matarajio makubwa ya
warsha hiyo.
Pia, alisisitiza kuwa mafunzo hayo yameongeza uelewa
wa viongozi katika kutambua mipaka ya kazi zao, jambo ambalo litaimarisha
Utawala Bora na kutoa wito kwa washiriki hao kwamba taaluma waliyoipata katika
mafunzo hayo waitumie vyema katika kujenga mahusiano mazuri wakati wa
kutekeleza majukumu yao.
Sambamba na hayo, Mhe Kheir alieleza haja ya
kuendeshwa warsha kama hiyo kwa Waheshimiwa Mawaziri na Makatibu Wakuu wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ili kupunguza changamoto zinazojitokeza katika
taasisi zao.
Akitoa neno la shukurani katika warsha hiyo Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Meja Mstaafu
Juma Kassim Tindwa alieleza kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kwa kiasi kikubwa na
kuahidi kufanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na kuleta mabadiliko makubwa katika
utendaji wao wa kazi.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Comrade Said Mwambungu
alieleza kuwa mbali ya mafunzo waliyoyapata katika hiyo, pia ushirikiano kwa
viongozi wa Mikoa wa Tanzania Bara na Zanzibar nao umeweza kuimarika na kuahidi
kuendeleza kushirikiana ili kuimarisha Muungano uliopo.
Katibu Mkuu
Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI Jumanne Sagini alieleza azma ya Wizara hiyo katika kutoa mafunzo kwa viongozi
wake wote wakiwemo viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika
kuhakikisha wananfanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment