Habari za Punde

Balozi Seif Afungua Mafunzo kwa Vijana Wanaojifunza Taalum ya Mitandao ya Teknolojia ya Habari.

Na.Othman Khamis Ame. OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaasa Vijana wanaojifunza Taaluma ya Mitandao ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kuwa makini katika matumizi bora ya mfumo huo mpya ili kulinda mila na Tamaduni zao za asili.

Alisema si vyema kuthubutu kufanya matumizi maovu way mfumo huo akijua kwamba yatawashawishi kujiingiza katika matendo yatakayowapelekea kuwa na maamuzi ya kufanya vitendo vilivyo nje ya utamaduni wao.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha hizo wakati akiyafunga Mafunzo ya Miezi Mitatu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Zanzibar { TEKNOHAMA } yaliyoendeshwa kwa pamoja kati ya Umoja wa Madereva na Utingo Zanzibar { UMUZA } na Jumuiya ya kupambana na changamoto na kuwaendeleza Vijana Zanzibar { ZAFAYCO } hapo katika Majengo ya Skuli ya Sekondari Donge Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema Dunia imekuwa na Mabadiliko makubwa ya Teknolojia ya Kisasa ya Mawasiliano inayokwenda kwa haraka kiasi kwamba Jamii za Kimataifa popote pale zilipo hupata fursa za kuwasiliana, kushirikiana na hata kupashana taarifa kupitia mfumo huo.

Akisoma Risala Mkuu wa Mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Nd. Abdullah Othman Ali alisema kwa kuelewa matatizo na changamoto zinazowakabili vijana katika maeneo mbali mbali Nchini Taasisi hizo zimebuni mradi huo kwa kuwakusanya pamoja vijana ili kuwapatia mafunzo yanayowawezesha kujiepuisha na makundi maovu.

Naye Mratibu wa Mradi wa mafunzo hayo wa Jumuiya ya kupambana na changamoto na kuwaendeleza Vijana Zanzibar { ZAFAYCO } Nd. Abdi Hamid Abeid alisema Jamii inaweza kupunguza uchafuzi wa mazingira endapo itakijika katika katumizi zaidi ya Kompyuta.

Alisema Wanafunzi wa Skuli za Sekondari na Vyuo Vikuu hivi sasa wamekuwa wakitumia kumbu kumbu za vitabu na baadhi ya maandisi na machapisho kupitia mtandao huo badala ya mfumo wa zamani wa kutumia vitabu vilivyokuwa vikitengenezwa kwa karatasi zinazotokana na kukatwa kwa miti.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.