Habari za Punde

Dr Shein awaambia watendaji Taasisi za fedha: Kuweni waadilifu na zitunzeni amana za wananchi


  
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                           21.4.2015
---
WATENDAJI wa Taasisi zote za Serikali hasa wale wanaosimamia masuala ya fedha wamehimizwa kushikamana na maadili ya kazi na kuwa waaadilifu katika kuzitunza amana za wananchi zilizo chini ya dhaman zao.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Ali Mohamed  Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa Mkutano wa kwanza wa Wadau wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) katika ukumbi wa Salama, Hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar.

 Katika hotuba  yake, Dk. Shein aliwasisitiza  watendaji hao kushikamana na maadili ya uongozi kama Sheria za nchi na kazi zinavyoelekeza kwa kutambua kuwa kila siku kiongozi huwa ndio mfano wa tabia njema.

Aliwataka viongozi kutambua kuwa wananchi wanawatazama na wanawapima wakiwa kazini, katika maisha yao nje ya kazi na watambue kuwa viongozi wote wanawajibika kwa wananchi akiwemo yeye mwenyewe hivyo kuna haja ya kutekekelza wajibu wao ili wananchi waendelee kuwa na imani na Serikali yao.

Dk. Shein alisema kuwa katika kuziongoza taasisi hizo, viongozi hawana budi kwenda sambamba na mabadiliko ya kijamii na teknolojia huku wakiwa mbele kwa maslahi ya wadau au wananchi wanaowahudumia.


“Mna wajibu wa kuhakikisha kuwa sheria zinazoongoza taasisi zinakidhi mahitaji na uhalisia wa hivi sasa, viongozi imara katika kuyafanyia kazi malalamiko ya wananchi juu ya taasisi zenu, hasa suala la ucheleweshaji wa utoaji wa huduma”,alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein aliwaeleza washiriki hao kujifunza kutoka katika nchi nyengine, ambazo taasisi kama ZSSF huwa mstari wa mbele katika kuwekeza kwenye miradi mbali mbali yenye tija, jambo ambalo ni muhimu katika kukuza uchumi na soko la ajira.

Alisema kuwa Waajiri wa sekta binafsi ni vyema wakahakikisha wanawasilisha michango kwa wakati ili kurahisihsa shughuli za uendeshaji wa taasisi hii bna kijenga misingi mizuri kwa wafanyakazi wao wakati wanapostaafu.

Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwataka Jumuiya ya Waajiri Zanzibar (ZANEMA) ambao ni wadau wakubwa wa mkutano huo kuwakumbusha waajiri juu ya jukumu hilo la kisheria ili kujenga mustakbali mzuri baina ya waajiriwa, ZSSF na waajiri.

Katika mkutano huo, Dk. Shein alizindua mfumo wa ZSSF wa kutoa fao la uzazi kwa maana ya kwamba akina mama wanaokwenda kujifungua watakuwa wanalipwa na ZSSF.

Dk. Shein alieleza kuwa utolewaji wa mfao hayo ya uzazi ni faraja kubwa kwa wanafamilia mabo ni wanachama wa ZSSF kwani kila mmoja anaelewa taabu wanayopata akina mama katika kipindi cha kujifungua.

“Uamuzi huu wa kutoa fao na uzazi unakwenda sambamba na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali za kuimarisha ustawi wa kinamama wajawazito pamoja na kupunguza vifo vya watoto ambavyo baadhi ya wakati husababishwa na umasikikini unaopelekea watoto wakiwa matumboni kukosa mahitaji ya msingi kwa afya zao au huduma muhimu wakati wanapozaliwa na mara baada ya kuzaliwa”alisema Dk. Shein.

Pamoja na uzinduzi huo Dk. Shein pia, alizindua Mfumo wa kujichangia kwa hiari, ambapo kutatoa fursa nzuri kwa wananchi wengi wa Unguja na Pemba, shamba na mijini, walio katika sekta zisizo rasmi  kuweza kujiwekea  kinga ya kipato ambayo itakuwa na umuhimu mkubwa hasa kwa maisha yao ya uzeeni.

Alisema kuwa mwanachama  atapata fursa ya kumsajili mtoto na kumchangia mafao ya elimu ili yaje yamsaidie mtoto huyo wakati wa kujiendeleza na elimu ya juu, utaratibu ambao utatoa fursa ya pekee kwa wazee wenye dhamira njema ya kuwekeza kwa maendeleo ya elimu ya watoto wao.

Dk. Shein aliutaka uongozi wa ZSSF kuongeza kasi ya utoaji wa elimu juu ya namna ambavyo wananchi wanaweza kujiunga katika mfumo huo mpya wa kuchangia kwa hiyari pamoja na fursa watakazonufaika nazo.

Mapema  Mwenyekiti wa Jumuiya ya ZANEMA Bwana Mohamed Bhaloo akitoa salamu za jumuiya hiyo alisema kuwa ZANEMA itahakikisha inaweka maslahi mbele kwa wajiriwa kuwa na mustakbali mwema na waajiriwa wao ili waweze kunufaika na matunda ya ZSSF na hatimae kuimarika kiuchumi na kuweza kupambana na umasikini.

Nae Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSSF  Makame Mwadini Silima alisema mafao ya uzazi yatalipwa kwa wanachama wanawake waliotimiza vigezo vya  kuchangia kwa muda wa miezi 36, miezi sita iwe mfululizo kutoka tarehe anayoomba mafao, uthibitisho wa madaktari wenye kutambulika, vielelezo vya ushahidi wa kuthibitisha madai ya mafao, awe mjamzito ambae ujauzito wake umefikia miezi 28, awe kajifungua mtoto aliehai.

Aidha, alisema kuwa kigezo cha malizpo hayo ya mafao hayo ya uzazi ni asilimia 30 wastani wa mshahara wa mwezi wa wanachama wote wa Mfuko kwa mwezi na kusisitiza kuwa Mfuko utatangaza kiwango cha wastani wa msghahara utakao tumika kukokotoa mafao ya uzazi kila baada ya kufanyiwa tathmini ya Afya.

Viongozi mbali mbali walighudhuria katika Mkutano huo wakiwemo kutoka katika Mifuko ya Hifadhi, Mashirika na Taasisi mbali mbali za fedha kutoka Zanzibar na nje ya Zanzibar ambapo Dk. Shein alikabidhi  hundi ya fao la uzazi kwa wanachama wa ZSSF pamoja na kutoa zawadi kwa wachangiaji bora wa Mfumo wa kujichangia kwa hiari.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.