Habari za Punde

Maoni ya Kamati ya katiba, Sheira na utawala bora, makadirio ya bajeti ya wizara hiyo


MUHTASARI WA HOTUBA YA MWENYEKITI WA KAMATI YA KATIBA, SHERIA NA UTAWALA YA BARAZA LA WAWAKILISHI, KUHUSU MAKADIRIO YA BAJETI YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA MWAKA 2015/2016
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutujaalia afya njema na kutuwezesha kukutana hapa kwa ajili ya kutekeleza wajibu wa kulijenga taifa letu. Aidha napenda kuchukua nafasi hii pia kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika kwa kunipa nafasi hii adhimu ya kutoa maoni ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2015/2016.

Mheshimiwa Spika,

Nitumie nafasi hii pia kumshukuru Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Abubakar Khamis Bakar, Katibu Mkuu ndugu Asaa Ahamad Rashid na Naibu Katibu Mkuu wake Ndugu Mdungi Makame Mdungi na watendaji wote wa Wizara ya Katiba na Sheria ambao kwa kipindi chote cha miaka miwili na nusu tumefanya nao kazi kwa mashirikiano makubwa. Naomba nikiri kuwa Wizara hii ni miongoni mwa Wizara ambazo zimefanikiwa sana katika utendaji wake kutokana na kupokea na kufanyiakazi kwa vitendo ushauri unaotolewa na kamati. Nidhamu hii ya utendaji ndiyo leo inanifanya kwa niaba ya Kamati, kuwapongeza watendaji wa Wizara hii, na kuwataka waendelee kudumisha mashirikiano baina yetu na wao.

Mheshimiwa Spika, 

Kazi yetu ya kupitia Bajeti ya Wizara hii isingekamilika bila ya mashirikiano ya hali ya juu ya wajumbe wote wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ambao walifanya kazi hii kwa kujitolea. Kazi kubwa imefanywa na Kamati hii chini ya uongozi wa Mwenyekiti wetu mahiri, Mheshimiwa Ussi Jecha Simai ambaye hivi sasa  anapata nafuu kutokana na mitihani wa maradhi, na tunamuomba Mwenyezimungu ampe afya njema na uzima ili arudi tena na kuungana na sisi katika kuwatumikia wananchi wetu.


Mheshimiwa Spika,

Naomba nitumie muda huu mchache, kuwatambuwa Wajumbe wote wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala huku nikithamini mchango wao mkubwa uliofanikisha Kamati hii kuwasilisha muhutasari huu wa hotuba. Naomba niwataje kama ifuatavyo:-
1. Mhe. Ussi Jecha Simai                          Mwenyekiti
2. Mhe. Abdalla Juma Abdalla                   Makamo Mwenyekiti
3. Mhe. Wanu Hafidh Ameir                      Mjumbe
4. Mhe. Nassor Salim Ali                          Mjumbe
5. Mhe. Bikame Yussuf Hamad                  Mjumbe
7. Mhe. Suleiman Hemed Khamis              Mjumbe

Mheshimiwa Spika,

Katika kipindi chote cha miaka miwili na nusu ya uhai wa kamati hii, shughuli zake zimekuwa zikiratibiwa na Makatibu wetu wa Kamati, ambao nawashukuru kwa kushirikiana nasi kwa kipindi chote hicho, pamoja na shukurani hizo naomba niwataje kama ifuatavyo:-
1.  Ndg. Aziza Wazir Kheir                         Katibu
2. Ndg. Khamis Hamadi Haji                      Katibu
Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya wajumbe wa kamati tunawashuru sana.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Katiba na Sheria ndiyo sehemu ya kielelezo cha utawala wa sheria katika nchi, kukosekana kwa Wizara hii kunapelekea utaratibu mbovu wa utekelezaji wa sheria za nchi. Wizara hii ndiyo inayoratibu uendeshaji wa moja ya mihimili mitatu ya dola ambao ni Mahakama, kutokana na jambo hilo ndiyo maana nikatangulia kusema kuwa Wizara hii ni sehemu ya kielelezo cha utawala wa nchi kutokana na umuhimu wake huu.
Mheshimwia Spika,
Katika bajeti ya mwaka huu inayotumia mfumo wa programu, Wizara ya Katiba na Sheria, imepangiwa programu kuu mbili katika fungu la Wizara, ambazo ni programu ya Usajili na Usimamizi wa Masuala ya Dini yenye programu ndogo nne, na programu ya Mipango na Uendeshaji wa Sekta ya sheria yenye programu ndogo tatu.
Mheshimiwa Spika,
Katika programu kuu ya kwanza, kamati imepitia programu zake ndogo nne, ambapo programu ndogo ya kwanza ya Usajili wa Matukio ya kijamii inayosimamiwa na Ofisi ya Mrajis wa Vizazi na Vifo, imewekewa lengo kuu ambalo ni kuimarisha mfumo wa usajili wa matukio. Katika kufikia lengo hilo ofisi ya Vizazi na Vifo imepangiwa kutumia Shilingi         421, 191,000. Kamati yetu imetazama changamoto za Ofisi hii na kuona kuwa kiwango hicho cha fedha ni kidogo kuweza kufikia malengo hayo kwa ufanisi, na kwa kuwa keki yetu haitoshelezi kamati yetu inaomba Serikali kuhakikisha kuwa hicho kidogo kilichokasimiwa kwa Ofisi hii basi kipatikane ili Ofisi hii ya Mrajisi wa Vizazi na Vifo iweze kufikia sehemu ya lengo na shabaha zilizomo katika programu iliyopangiwa.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yetu inachukuwa nafasi hii kutambuwa na kuipongeza Ofisi hii kwa kujitahidi kutanuwa wigo wa usajili kwa maeneo yote nchini. Takribani kila Wilaya sasa imeshawekwa Afisi za Usajili wa Vizazi na Vifo na kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi.


Mheshimiwa Spika,
Kamati imeelezwa kuwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2015/2016, Wizara ya Katiba na sheria imetayarisha Mpango kazi wa utekelezaji wa Mkakati wa Mabadiliko ya Sheria (Zanzibar Legal Sector Reforms) ambapo pamoja na mpango kazi, miradi sita imeambatanishwa na Mkakati huo. Moja ya mradi huo ni Mradi wa kuimarisha Usajili wa Vizazi, Vifo, ndoa, talaka na kuasili mtoto. Kamati yetu inapongeza hatua hiyo kubwa iliyofikiwa, hofu yetu kubwa katika utekelezaji wake ni ile ile ya upatikanaji wa fedha za kutosha katika kuendesha Mradi huo.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inaiomba Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Ikulu na Utawala Bora kupitia Tume ya Mipango, ambayo miradi hiyo itapelekwa kwake kwa hatua zaidi, kukaa na Wizara ya Katiba na Sheria na kuona ni namna gani miradi hiyo itaingizwa katika mipango ya Serikali ili kupatiwa fedha na hatimaye iweze kutoa matokeo yanayokusudiwa kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika,
Kamati imepitia programu ndogo ya pili, ya usajili wa Biashara na Mali, ambayo katika bajeti ya mwaka huu 2015/2016, imetengewa shilingi 1,290,605,000, chini ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali. Katika kufikia lengo kuu la kuimarisha mfumo wa usajili wa biashara na mali, kamati inashauri Serikali kuitumia Ofisi ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali, kuweka mfumo mmoja wa usajili wa Kampuni, jumuiya na nyaraka kwa njia ya dijitali.
Mheshimiwa Spika,
Mfumo mmoja wa usajili wa Kampuni na jumuiya nyengine kwa njia ya dijitali ni muhimu katika kuimarisha ukusanyaji kodi na uwekaji wa takwimu kwa usahihi. Kamati imeona kuwa kampuni zinazosajiliwa nchini taarifa zake za usajili zinawekwa na Wakala wa Usajili wa Bishara na Mali, kampuni hizo hizo zinafanya biashara na kutakiwa kulipa kodi ambapo baadhi ya Kampuni hizo zinapopeleka marejesho katika taasisi za kodi, huwa hazipeleki baadhi ya taarifa muhimu kwa nia ya kukwepa kodi au kupunguza viwango vya matozo na kuikosesha mapato Serikali.
Mheshimiwa Spika,
Sote tunakumbuka kuwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ametutaka wajumbe wa Baraza hili kumsaidia kutambua vyanzo vya mapato na yeye atavishughulikia. Katika kutambua huko kamati yangu inaona kuwa uwepo wa mfumo mmoja wa usajili wa Kampuni kwa njia ya dijitali ni chanzo muhimu cha mapato na kitasaidia kuongeza mapato ya Serikali.
Mheshimiwa Spika,
Katika mfumo huo taarifa za Kampuni zote zitawekwa katika mfumo wa dijitali na Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali, ambapo taasisi nyengine za kodi kama TRA na ZRB zitaweza kupata taarifa hizo kwa usahihi kutoka kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali na kuweza kuzitoza kodi taasisi hizo kwa usahihi. Kamati yangu inaomba Serikali kuisaidia mipango ya kuanzishwa kwa mfumo huo ambao wataalamu wameshafanya ‘study’ kwa awamu ya kwanza, na hivi sasa umekwama utekelezaji wake katika hatua zilizobakia kutokana ukosefu wa fedha.
Mheshimiwa Spika,
Baadhi ya nchi za hapa hapa Afrika, zimefanikiwa katika kuimarisha mapato yake ya ndani kupitia mfumo huu wa usajili wa Kampuni na Jumuiya nyengine kwa mfumo mmoja wa dijitali, mfano mzuri wa nchi hizo ni jirani zetu Rwanda, ambapo wao wameanza kupata mafanikio katika mfumo huu. Kamati imeona kuwa katika bajeti ya mwaka huu 2015/2016, kuna Mradi wa Mageuzi ya Mfumo wa Usajili wa Biashara umetengewa shilingi bilioni moja, kamati inasisitiza sana fedha hizo zipatikane ili mfumo huo uanzishwe.


Mheshimiwa Spika,
Katika programu ndogo ya Usimamizi wa Hakimiliki, imewekewa lengo la kuimarisha Usimami wa upatikanaji wa haki za wasanii na wabunifu. Kamati yangu inaipongeza Ofisi ya Hakimiliki na Mkurugenzi wake kwa kazi kubwa anayofanya ya kusimamia haki za wasanii na wabunifu licha ya uchanga wake na changamoto kadhaa zinazokabili Ofisi yake.
Mheshimiwa Spika,
Programu hii ndogo ya Usimamizi wa Hakimiliki imetengewa shilingi 240,000,000, ambazo hizo zimekusudiwa kuleta matokeo yaliyolengwa kwa Ofisi hii. Kamati yangu imekuwa ikitafakari kwa kiasi gani fedha hizo zitaweza kutatuwa changamoto za Ofisi, mbali ya kufikia malengo yaliyokusudiwa. Kamati imetembelea Ofisi hii na imebaini kuwa kuna baadhi ya vitendea kazi muhimu vinakosekana kama vile usafiri. Kama tunavyojua kazi za Ofisi hii siyo za Ofisini tu, pia inahitajika kufatilia ukusanyaji wa mirahaba katika vyombo mbali mbali vya habari na mahoteli. Kamati inashauri Serikali kuiongezea bajeti Ofisi hii ili iweze kutatua changamoto hizo na kufikia malengo yake.
Mheshimwa Spika,
Ofisi ya Msajili wa Hakimiliki ina upungufu wa wataalamu mbali mbali hasa katika fani ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, tokea mwaka 2012 Ofisi hii imekuwa ikiomba kupatiwa wataalamu hao na wengine katika fani mbali mbali, lakini hadi hivi sasa bado Tume ya Utumishi Serikali haijafanikisha kupatakana kwa nafasi hizo.
Mheshimiwa Spika,
Kamati inaitanabahisha Serikali kuwa isitegemee mfumo huu wa bajeti wa PBB ulete matokeo wanayokusudia kwa haraka bila ya kwanza kuziwezesha taasisi zinazosimamia progamu hizo, kwa kuzipatia nyenzo na wataalamu wa kufanikisha mipango hiyo. Tunaitaka Tume ya Utumishi ya Serikali kuwapatia wataalamu hao ili lengo lililowekwa katika Programu hii ndogo ya Usimamizi wa Hakimiliki liweze kufanikiwa.
Mheshimiwa Spika,
Kamati imebaini changamoto nyengine ya usimamizi wa hakimiliki kwa vyombo vya sheria hasa baadhi ya mahakama zetu ambazo wanapopelekwa watuhumiwa wanaonyonya haki za wasanii sheria hazifatwi ipasavyo. Kamati yangu inataarifa ya kesi ambayo inamuhusisha mtu mmoja aliyetumia kinyume na sheria hakimiliki na mtu huyo kutakiwa kulipa na akakataa. Jambo la kusataajabisha, wakati mtu huyo anapelekwa mahakamani akajisifu kuwa atatumia uwezo wake wa kifedha kuachiwa, na kweli kesi ilipofika mahakamani mtu huyo aliachiwa kwa sababu zinazotia shaka.
Mheshimiwa Spika,
Mambo haya ndiyo tunayoyapigia kelele kila siku katika Baraza hili ya vyombo vyetu vya kusimamia haki vifuate sheria, haiwezekani mtu anapelekwa mahakamani anajisifu kutumia uwezo wake wa kifedha na kuachiwa na huku ameshadhulumu haki ya mtu. Kamati inaomba Wizara kulichunguza suala hili kwa kumchukuliwa hatua za kinidhamnu Hakimu aliyehusika na kadhia hii ya aibu kwa mujibu wa sheria. Aidha, tunaiomba Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi ilifuatilie suala hili kwa kuwasiliana na Taasisi ya Hakimiliki, na hatua stahiki zichukuliwe ili kukomesha mambo haya yasijitokeze tena na kuvunja moyo juhudi za wasanii na Ofisi zetu zinazosimamia haki zao.
Mheshimiwa Spika,
Programu ndogo ya Usimamizi wa Masuala ya Dini imewekwa chini ya Kamisheni ya Wakf na Mali ya Amana na Ofisi ya Mufti ambapo Kamisheni ya Wakf imekasimiwa shilingi 587,800,000 na Ofisi ya Muft imetengewa shilingi 357,612,000. Kiasi hicho cha fedha ni kidogo kwa taasisi hizo zenye majukumu makubwa yanayogusa jamii moja kwa moja. Kamati yangu inashauri kuwa katika kuhakikisha kuwa Taasisi hizo mbili angalau ziweze kufanya majukumu yake ya kawaida basi zipatiwe fedha hizo kwa wakati na kama zilivyokasimiwa.

Mheshimiwa Spika,
Kamisheni ya Wakf, imekuwa ikikusanya fedha kutoka katika ada za huduma mbali mbali wanazotoa kama vile mirathi, hata hivyo, fedha hizo hivi sasa zimepunguzwa kiwango chake na  hicho kilichobaki kinakusanywa na ZRB. Hatua hiyo imedhoofisha Kamisheni ya Wakf, ambayo imekuwa ikizitumia fedha hizo kutatua baadhi ya changamoto za kiofisi kama vile kufatilia mali za Wakf, mirathi zakka na sadaka. Shughuli hizo zote zinaweza kuzorota ufuatialiji wake iwapo fedha hizo zitaendelea kuingizwa katika mfumo wa Serikali kupitia ZRB.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inaiomba sana Wizara ya Fedha, kufikiria upya makusanyo ya fedha za Mirathi kuzibakisha kwa Kamisheni ya Wakf ili ziendelee kusaidia uendeshaji wa shughuli zao muhimu ambazo zinakwama kutoka na uingizwaji mdogo wa fedha za matumizi mengineyo.
Mheshimwa Spika,
Hivi karibuni kumekuwa na mizozo mingi inayohusu mali za wakf na mirathi na kupelekea hata mahakama zichukuwe hatu kali zidi ya wahusika ambao mara nyingi wamekuwa ni wana ndugu wa familia. Mnamo mwezi Febuari, mwaka 2015 kumeripotiwa katika vyombo vya habari hapa nchini, ikiwemo ZBC, kuhusu uamuzi wa Mahakama kuwafunga gerezani kwa muda wa wiki mbili wanafamilia wa familia moja maarufu nchini, kwa kupinga maamuzi ya mahakama kutoka na kesi ya Wakf iliyohusu wanandugu wa familia hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Uwepo wa Kamisheni ya Wakf ulitegemewa matukio kama hayo yasiwepo au yasijitokeze katika hali kama hiyo, kwa vile Kamisheni inajukumu la kusimamia na kutoa elimu ya kutosha kwa jamii kuhusu namna ya usimamizi wa mali za wakf na mirathi na kuweka dawati maalumu la ushauri wa kitaalamu kwa familia zinazokinzana ili kabla ya familia hizo kufikisha mashauri yao mahakamani ziweze kwanza kupata ushauri kutoka kamisheni ya Wakf na ikishindikana ndiyo hatua nyengine zifuate. Kwa kufanya hivyo, mheshimiwa Spika, tutaweza kupunguza migogoro ya familia kuhusu mali za mirathi na wakf na kupunguza utitiri wa kesi katika mahakama zetu.
Mheshimiwa Spika,
Katika kufikia lengo la programu hii ndogo ya usimamizi wa masuala ya dini, Ofisi ya Mufti inajukumu kubwa la kuhakikisha kuwa jamii inaepukana na vitendo viovu na mpromoko wa maadili. Kamati yangu inashauri Ofisi ya Mufti kutambuwa jukumu lake na kusaidia kubainisha mambo mbali mbali katika jamii yanayosababisha mporomoko wa maadili kwa kushirikiana na miskiti na madrasa kuyakemea kwa nguvu zote na kuyaondoa.
Mheshimiwa Spika,
Aidha tunaitaka Serikali kushirikiana na Ofisi ya Mufti katika kuchukuwa hatua dhidi ya vitendo viovu vinavyochangia mporomoko wa maadili ya jamii yetu katika jamii. Sote tunatambuwa kuwa jamii yetu imejengeka katika maadili mazuri ya heshima na ustaarabu wa hali ya juu. Haitawezekana kuacha mporomoko wa maadili uendelee katika jamii kama vile hakuna mshughulikiaji, Ofisi ya Mufti ilibebe jukumu hili kwa nguvu zote na wananchi watowe ushirikiano na Ofisi ya Muft katika kupiga vita vitendo vyote vinavyopelekea mporoko wa maadili katika jamii bila ya kuona haya waka muhali.
Mheshimiwa Spika,
Katika programu kuu ya pili ya Mipango na Uendeshaji wa Sekta ya Sheria jumla ya shilingi bilioni tatu, milioni kumi na mbili na tisini na mbili elf, (3,012,092,000) zimepangwa kwa uendeshaji wa programu ndogo za Uongozi na  uendeshaji wa Sekta ya sheria, Mipango, Sera na Utafiti na Uendeshaji wa Wizara Pemba. Kamati haina tatizo na Programu hii, isipokuwa tunasisitiza kuwa maslahi ya wafanyakazi wa Mahakama hasa kwa Mahakimu wa Mahakama za mwanzo yatazamwe upya. Kamati yangu inashauri Serikali kuharakisha sera ya malipo ili mahakimu wa mahakama za mwanzo nao wapatiwe nyongeza stahiki.
Mheshimiwa Spika,
Jengo jipya la Wizara ya Katiba na Sheria, liliopo Mazizini limekamilika na tunaipongeza Serikali kwa hatua ile kubwa ya kimaendeleo. Katika kukamilisha ujenzi ule bado kuna changamoto ndogo ndogo ambazo Mheshimiwa Waziri amezieleza na sisi kamati tunaisisitiza zitatuliwe hata kwa kubana vifungu ili jengo lile lihamiwe.
Mheshimiwa Spika,
Katika fungu G 02, la Mahakama Kuu, kuna programu kuu mbili, ya kwanza ni Usimamizi wa Upatikanaji wa haki ambayo ina progamu ndogo moja ya usimamizi wa upatikanaji wa haki. Progamu ya pili ni ya usimamizi wa shughuli za uendeshaji na utawala wa Mahakama ambayo ina programu ndogo za uendeshaji na utawala wa Mahakama Unguja na Uendeshaji wa shughuli za Mahakama Pemba.
Mheshimiwa Spika,
Programu zote hizo zimepangiwa jumla ya shilingi bilioni tano, milioni mia moja na arobaini na tatu na laki moja, (5,143,100,000). Kamati yangu imetazama vizuri programu ndogo ya pili ya kusimamia shughuli za Mahakama Pemba, ambayo imepangiwa shilingi  bilioni moja, milioni mia tano na tisini na nne, laki tano na kumi na tisa elfu, (1,594,519,000)  ambapo kamati imeona kuwa kiasi hiki cha fedha hakitawezesha kukamilisha hatua ya ukarabati wa jengo la Mahakama Kuu, Chake Chake ambapo kwa mwaka huu wa fedha ilihitajika kiasi cha kutosha cha fedha ili kuwezesha kukamilika kwake. Kamati inataka kujuwa ni kiasi gani katika fedha hizi zilizotengwa kitaweza kufanikisha kukamilisha ukarabati wa jengo la mahakama ya Chake Chake.


Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu imeshapiga kelele sana tokea bajeti ya mwaka jana 2014/2015 kuwa jengo la Mahakama ya chake chake Pemba lipo katika hali mbaya, wanaofanyaka kazi pale ni banaadamu wenzetu, wanastahiki kufanyakazi zao katika mazingira salama na sivyo Kama lilivyo hivi sasa.
Mheshimiwa Spiaka,
Kamati yangu ilitegemea sana katika bajeti ya mwaka huu Serikali ingeona umuhimu wa kuweka fedha za kutosha ili ukarabati wa jengo lile ukamilike. Kamati haijaridhika na kasma hii ndogo katika programu ndogo ya kusimamia shughuli za Mahakama Pemba, tunaitaka Serikali kubana vifungu vya matumizi mengine na kusaidia kupatikana fedha ya kutosha ili ukarabati wa Mahakama Pemba ukamilike.
Mheshimwa Spika,
Katika fungu G 03, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar, kuna progaramu kuu mbili ambazo zimetengewa jumla ya shilingi bilioni moja, milioni kumi na laki mbili (1,010,200,000). Kamati yangu imebaini changamoto kadhaa zinazokabili Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ambazo zinaweza kuathiri utekelezaji wa programu hizo kwa kiwango hicho cha fedha kilichowekwa. Moja wa changamoto hizo ni uhaba wa fedha na kutoingizwa kwa fedha kwa mujibu wa maombi wa ‘cash flow’ iliyopelekwa Wizara ya Fedha. Kamati yangu bado inasisitiza kuwa Serikali izingatie sana umuhimu wa taasisi zinazosimamia haki, hasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ambayo inasimamia kesi zote za madai za Serikali. Kamati inatanabahisha kuwa shughuli za Ofisi hii zinapokwama athari yake ni kubwa kwani Serikali inaposhindwa kesi italazimika kulipa gharama kubwa za kesi hizo.
Mheshimiwa Spika,
Changamoto nyengine kubwa ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ni  kutopata ushirikiano wa kutosha kwa baadhi ya taasisi za Serikali ambazo zimeshitakiwa Mahakamani. Ofisi ya mwanasheria Mkuu imekuwa ikifanya mawasiliano na taasisi hizo kuwatanabahisha juu ya athari za kutotoa ushirikiano ambazo hupelekea Serikali kushindwa kesi na kulipa fedha nyingi kama fidia.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inaitaka Serikali kutoka toleo kwa taasisi zote za Serikali kuhakisha kuwa kila taasisi ambayo ina kesi inayosimamiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwapeleka maafisa wa Sheria wa Taasisi hizo kuripoti kila inapohitajika kwa mwanasheria Mkuu na kuhakikisha kuwa ushauri unaotolewa na Mwanasheria Mkuu unafanyiwa kazi na maafisa hao kwa kushirikiana na wakuu wa taasisi hizo.
Mheshimiwa Spika,
Aidha, tunaitaka Serikali kutumia vyema sheria namba 3 ya mwaka 2010, sheria ya Mwenendo wa Mashitaka ya au Dhidi ya Serikali, katika kifungu cha 7 cha sheria hiyo, kumuwajibisha Afisa yoyote wa umma ambaye kwa uzembe wake atasabisha Serikali ishindwe Kesi mahakamani, ikiwemo kutotoa ushirikiano kwa Mwanasheria Mkuu, na kumtaka Afisa huyo kulipa fidia ambayo Serikali itatakiwa ilipe kwa mujibu wa sheria hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Katika fungu G 04, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nayo imepangiwa programu Kuu mbili za Uendeshaji na Usimamizi wa kesi za jinai na Mipango na Uendeshaji ambazo kila moja ikiwa na programu ndogo mbili, jumla yake ni shilingi bilioni moja , milioni mia sita na ishirini na saba na laki moja (1,627,100,000).
Mheshimiwa Spika,
Programu zinazosimamiwa na Ofisi hii ni kubwa na kiwango cha fedha kinachoingiziwa hakilingani na ukubwa wa Progamu hizo, Ofisi hii inalazimika kufanya kazi zake kwa vile ni wajibu wake lakini kamati tumeona kuwa inafanya kazi hizo katika hali ngumu.

Mheshimiwa Spika,
Uendeshaji wa mashitika unataka ufanisi na ufanisi unatokana na matayarisho kwa waendesha mashitaka, kuimarishwa kwa maslahi yao ili kuwajenga nguvu na morali kwa kazi ngumu ya kupambana na wahalifu, hivyo, kamati bado inarejesha kilio kwa Serikali kuwatazama vizuri kimaslahi wanasheria wa DPP ambao tunawetegemea sana kutuondolewa wezi, majambazi, wabakaji, matapeli n.k katika jamii, kwa kuthibitisha mashitaka yao mahakamani na kufungwa gerezani.
Mheshimiwa Spika,
Tujiulize iwapo kama waendesha mashitaka hao, kama hawatafanya kazi hiyo kwa ufanisi, jamii yetu itakalika? Tusisahau kuwa kwa sababu hiyo tu, Waendesha mashitaka wengi wenye uwezo mkubwa katika Ofisi ya DPP, wameshaacha kazi na kutafuta shughuli nyengine za kufanya. Kamati yangu bado inasisitiza tena kuwa Serikai ione umuhimu wa vijana wetu hawa kuwaongezea maslahi yao ili tusiendelee kuwapoteza.
Mheshimiwa Spika,
Mashitaka hayathibitiki mahakamani bila ya ushahidi, na ushahidi katika dunia ya leo siyo ule wa kuona kwa macho na kusikia, matendo mengi ya jinai yanayofanywa na wahalifu kama vile udhalilishaji na mauwaji, hufanyika kwa namna ambayo siyo macho wala masikio yanaweza kushuhudia, isipokuwa kwa vyombo maalumu ambavyo hutumika kushuhudia matokea ya jinai hizo, mfano wa vyombo hivyo ni mashine ya vinasaba ya DNA.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mara nyengine, kamati yangu inarejesha kilio chetu kwa Serikali kuhakikisha kuwa mashine ya DNA inapatikana ili Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka iweze kuthibitisha makosa hayo mahakama kwa  njia za kitaalamu na kupatikana hatia kwa wahalifu. Sote tunafahamu hali ya vitendo vya udhalilishaji ilivyo nchini kwetu na namna tunavyokerwa na hali hiyo, kama ni hivyo basi, kamati yangu inaikumbusha Serikali kuwa kama ilivyofanya kwenye mkakati wa ununuzi wa meli mpya ambayo karibuni itawasilia nchini na mkakati kama huo ufanyike ili mashine ya DNA ipatikane, hilo linawezekana tukitimiza wajibu wetu.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu pia inataka maelezo kutoka kwa Waziri, vipi bajeti ya DPP imezingatia upatikanaji wa jengo la kudumu kwa Afisi ya DPP kisiwani Pemba, pamoja na hatua za kumalizia ujenzi wa nyumba za waendesha mashitaka Mkokotoni. Kamati inataka kujuwa ni vipi Wizara kwa kushirikana na wizara ya Fedha, itasaidia kupatakana fedha kwa ajili ya kukamisha ujenzi wa nyumba hizo ili ule mpango wa kuendesha mashitaka kiraia uweze kuenea katika Wilaya zote za Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Spika,
Tume ya kurekebisha Sheria, imepangiwa jumla ya shilingi milioni mia tano na ishirini na saba (527, 000,000) kwa ajili ya kuendesha programu kuu mbili za Mapitio ya Sheria na Utawala na Uendeshaji. Mafanikio makubwa yamepatikana tokea kuimarishwa kwa Tume ya Kurekebisha Sheria chini ya Mwenyekiti wake Jaji Mshibe Ali Bakari na Katibu wake ndugu Asma Jidawi. Kamati inawapongeza sana pamoja na watendaji wao wote na tunataka waendeleze juhudi za kuisaidia Serikali kuwa na sheria nzuri zinazotekelezeka.
Mheshimiwa Spika,
Nitumie fursa hii kuzitaka taasisi za serikali ambazo zinafanya mapitio ya Sheria zao kwa nia ya kufanya marekebisho kushirikiana na Tume kwani wao ndiyo wenye jukumu la kisera na utaalamu kufanyakazi hiyo. Aidha, kamati inaipongeza Tume ya Kurekebisha Sheria kwa kurejea kuwa mwanachama hai katika Umoja wa Tume za Kurekebisha Sheria za Afrika Mashariki na Kati (ALRAESA) na kufanikiwa kujiunga na Umoja wa  Tume za Kurekebisha Sheria za nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola (CALRAs) pamoja na kuanzisha ushirikiano na taasisi mbali mbali za kimataifa zenye jukumu sawa na Tume. Kamati yangu inaishauri Tume kutumia vyema fursa hizo katika ngazi ya kimataifa ili iweze kupata utaalamu na uzoefu katika kukabiliana na changamoto za maboresho ya sheria.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu ina mengi ya kueleza katika Wizara hii ambayo, lazima nikiri tena kuwa imekuwa ikipokea na kutekeleza kwa vitendo ushauri wa Kamati lakini kutokana na muda naomba nimalizie kwa kukushukuru na kuwashukuru wajumbe wako kwa utulivu wao wakati wote wa kuwasilisha muhtasari wa maoni haya ya kamati ya Katiba, Sheria na Utawala. Nawaomba wajumbe tushirikiane katika kuichangia kwa kutoa ushauri, maelekezo na hatimaye kuipitisha ili Mheshimiwa Waziri apate kutekeleza programu alizopangiwa katika bajeti hii.
Mheshimiwa Spika, baada ya hayo machache nakushukuru na naunga mkono hoja.

Ahsante

……………………
Abdalla Juma Abdalla
Makamo Mwenyekiti,
Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala,
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.