Na Maryam Kidiko-Maelezo
Mwanaharakati wa Masuala ya Wanawake wa Jimbo la Mwana kwerekwe Bi Rihi Haji Ali amewataka Wanawake wenzake kujitokeza kwa wingi kugombania nafasi mbali mbali za Uongozi ili kuweza kutetea haki zao .
Hayo ameyasema huko Mwanakwerekwe wakati akizungumza na Waandishi wa habari katika suala zima la wanawake kuacha woga na kujitokeza kwa wingi kugombania ili waweze kujisemea wenyewe na kupata haki zao za kimsingi.
Hata hivyo amesema wakati umefika kwa Wanawake kujisemea wenyewe na kuacha tabia ya kusemewa matatizo yao jambo ambalo linarudisha nyuma na kuchelewa kupata haki zao za msingi wanazokusudia.
Amesema kuwa Wanawake watapojitokeza kwa wingi na kuwa na ushirikiano mkubwa wataweza kutetea haki zao za msingi hasa katika suala zima la udhalilishaji unaojitokeza hapa Nchini kwa wanawake hao.
Vile vile amesema indapo watajitokeza Wanawake kugombani nafasi hizo watatoa ushirikiano mkubwa wa kumpigia kura ili kuwapa hamasa wanaume na wao waweze kuwaunga mkono katika kugombania nafasi hizo.
“Mwanamke yoyote akijitokeza kugombania Uongozi tutatoa ushirikiano mkubwa na kuhakikisha anapita katika ushindani huo”Amesema mwanaharakati huyo.
Amefafanuwa kuwa wanajitahidi kutoa Elimu sehemu mbali mbali na kuwaelimisha Wanawake jinsi ya kugombea na kuacha imani potofu zinazosemwa Katika Jamii.
Hata hivyo amesema wataunda Kamati Ndogo ndogo ili kuhakikisha kila Mwanamke aliyekuwa na vigezo vya kugombania nafasi yoyote ya uongozi kuweza kupata nafasi hiyo.
Mwanaharakati huyo ameishukuru Jumuiya ya Waandishi wa habari Wanawake Tanzania (TAMWA) pamoja na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Kwakuweza kuwatetea Wanawake na kuhakikisha wanapata haki zao za msingi.
Sambamba na hayo amevitaka Vyombo vinavyotoa Elimu kuhusu masuala ya Wanawake na kuzidi kutoa Elimu kwa Wanawake na kuwataka Wanawake kutoa mashirikiano pamoja na kupendana ili kutimiza lengo walilokusudia.
No comments:
Post a Comment