Habari za Punde

Waongoza watalii watakiwa kuanza kujifunza lugha ya kihindi

 Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar Said Ali Mbarouk akimueleza  jambo Mkurugenzi wa Kituo cha Kukuza Utalii  kati ya India na Zanzibar Jilesh Babla (hayupo pichani) walipokuwa na mazungumzo  Ofisini kwake Kikwajuni.(Picha Na Miza Othman- Maelezo Zanzibar).
 Waandishi wa Habari wakifuatilia  habari hizo kwa makini katika Ofisi ya Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar.( Picha Na Miza Othman- Maelezo Zanzibar).
 Mkurugenzi wa  wa Kituo cha Utalii kati ya India na Zanzibar Jilesh Babla  akiwa pamoja na   Mkurugenzi wa Utumishi wa Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo Joseph Kilangi wakati wa mazungumzo hayo.(Picha Na Miza Othman- Maelezo Zanzibar).
Picha ya pamoja   ya Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar Said Ali Mbarouk (katikati) pamoja na Mgeni wake   Jilesh Babla  (kushoto) na Mkurugenzi wa Utumishi wa Wizara hiyo Joseph Kilang.(Picha Na Miza Othman- Maelezo Zanzibar).

Mwashungi Tahir na Maryam Kidiko, Maelezo 
                                                                               
Waziri wa Habari  Utamaduni Utalii na Michezo Mhe Saidi Ali Mbarouk  amewataka wananchi wa Zanzibar  na hasa waongozaji wa watalii kujifunza lugha ya kihindi  ili waweze kuwahudumia watalii kutoka nchi hiyo ambao wanatarajiwa kutembelea  Zanzibar kwa wingi hivi karibuni.

Hayo ameyasema leo huko ofisini kwake   Kikwajuni wakati alipokuwa na mazungumza na Mkurugenzi wa Kituo cha kukuza Utalii kati ya India na Zanzibar Jilesh Babla.

Amesema  kufunguliwa  kwa kituo cha kukuza utalii katika Mji wa Mumbai nchini India, Zanzibar itapokea wageni wengi ambao watahitaji huduma muhimu za mawasiliano wakiwa  nchini.


Amesema  kuanzia msimu ujao wa  utalii  unaoanza mwezi wa Juni  wanakadiriwa  kupata kiasi  cha Watalii   500  kutoka India  na watahitaji huduma  mbali mbali.

“Miezi michache ijayo tunatarajia kupokea  watalii makundi kwa makundi wakiwemo kutoka India na hii ni  ishara njema ya kuwepo mashirikiano mazuri kati ya Zanzibar na India,” alisema Saidi Ali Mbarouk.

Nae Mkurugenzi wa Utangazaji  wa Utalii Mumbai  Jilesh Babla amesifu mashirikiano mazuri yaliyopo baina ya  Ofisi yao iliyopo mjini Mumbai na Wizara ya Habari ambayo yataanza kuleta mafanikio muda mfupi ujao.

Ameyataja mashirika ya ndege ya Kenya, Oman, Ethiopia na Italy  ambayo mashirika  watashirikiana nayo ili kuweza kuleta watalii jambo ambalo  litaweza kurahisisha shughuli za kitalii hapa nchini na kuleta faraja kubwa.

Mr Babla aliziomba  hoteli za Zanzibar  kujitokeza kwa wingi ili waweze kujitangaza  na kuweza kujulikana ili watalii watapokuja waweze kuyafahamu yale mahoteli

Sambamba na hayo mkurugenzi huyo aliomba kuwepo mashirikiano makubwa kati ya wafanya biashara wa India na Zanzibar ili kuweza kupata maendeleo visiwani humu.

1 comment:

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.