STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 26 Agosti , 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amezindua mradi mkubwa wa Maji na Usafi wa Mazingira Zanzibar na kusifu
jitihada za Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati kwa namna inavyotekeleza
miradi ya kuwapatia wananchi maji safi na salama.
Alieleza
kuwa jitihada za wizara hiyo zimewezesha Zanzibar kuzalisha lita milioni 163 za
maji ikiwa ni asilimia 76 ya mahitaji yake ambayo hadi Disemba mwaka jana
yalikuwa ni lita 214,580,240 hivyo kuwa na upungufu wa asilimia 24.
Dk.
Shein aliwaambia mamia ya wananchi na wageni waliohudhuria uzinduzi wa mradi
huo uliofanyika jana katika kijiji cha Taif, Wilaya ya Wete, mkoa wa Kaskazini
Pemba kuwa lengo la mradi huo ni kuimarisha upatikanaji wa huduma za maji na
kuimarisha usafi wa mazingira mijini na
vijijini zikiwemo skuli.
Utekelezaji
wa Mradi huo alibainisha kuwa ni miongoni mwa hatua za utekelezaji wa ahadi
zake kwa wananchi alizozitoa wakati akiomba ridhaa yao kuongoza Zanzibar katika
uchaguzi wa mwaka 2010 kupitia mipango mbalimbali ya maendeleo.
Aliitaja
mipango hiyo kuwa ni pamoja na Dira ya Maendeleo 2020, MKUZA II na Ilani ya
Uchaguzi 2010-2015 ambazo zote zimetilia mkazo suala upatikanaji wa maji safi
na salama kwa waanchi katika maeneo wanayoishi.
Dk.
Shein alisema ni jambo la kujivunia kuona kuwa huduma za maji safi na salama
zinazidi kuimarika hivyo kutekeleza kwa vitendo malengo ya Mapinduzi ya mwaka
1964.
Mradi
huo Maji na Usafi wa Mazingira Zanzibar
unajumuisha pia Ujenzi wa Miundombinu ya Kuimarisha na Kuendeleza huduma
ya Maji na Usafi wa Mazingira katika miji mitatu ya Pemba(Chake-Chake, Mkoani
na Wete).
Aliitaka
wizara hiyo pamoja na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kujidhatiti zaidi katika
kutekeleza miradi ya maji na kutoa wito kwa wananchi kufuatilia kwa karibu
taarifa kuhusu huduma za maji ambazo hutolewa mara kwa mara katika televisheni
na redio.
Sambamba
na wito huo, aliwataka wananchi
kuhakikisha kuwa wanatunza miundombinu ya maji
na vyazo vya maji na kuwatanabahisha kuwa miradi hiyo inagharimu fedha nyingi
hivyo ni rasilimali muhimu kutunzwa na kuhifadhiwa kwa manufaa ya taifa.
Aliwaeleza
wananchi hao kuwa mradi huo ambao umegharimu jumla ya shilingi bilioni 67.73
kuwa sehemu kubwa ya fedha hizo ni mkopo ambao unapaswa kurejeshwa hivyo ni
wajibu wao kuutunza mradi huo na kuwakumbusha kuwa wanaorejesha mkopo ni
serikali na wananchi wenyewe.
Alibainisha
kuwa wakati huu ambapo uchumi unaruhusu kukopa, Serikali haitasita kufanya
hivyo ili kuhakikisha kuwa inafikia azma na malengo ya Mapinduzi ya kumpatia
kila mwananchi popote alipo huduma ya maji safi na salama.
Dk.
Shein aliwashukuru washirika wa maendeleo na taasisi nyingine pamoja na watu
binafsi kwa mchango wao mkubwa katika kusaidia miradi ya maji nchini na kueleza matumaini yake kuwa
washirika hayo wataendelea kuziunga mkono juhudi za Serikali na wananchi wa
Zanzibar.
Akitoa
maelezo ya kitaalamu ya maradi huo, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji
na Nishati Ali Khalil Mirza alieleza kuwa mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira
Zanzibar ambao ulitekelezwa kwa pamoja kati ya Benki ya Maendeleo ya Afrika
(AfDB),Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-Habitat) na Serikali
ulihusisha maeneo makuu manne.
Aliyataja
maeneo hayo kuwa ni Kuijengea uwezo Mamlaka ya Maji ili kuiwezesha kutoa huduma
bora, ujenzi wa miundombinu ya kusambaza huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira
vijijini Unguja na Pemba, Ujenzi wa Miundombinu ya Kuimarisha na Kuendeleza
huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira katika miji mitatu ya Pemba na Kuimarisha
na Kuvitunza vyanzo vya Maji Unguja na Pemba.
Kuhusu
gharama za mradi alieleza kuwa umegharimu jumla ya shilingi bilioni 67.73
ambapo shilingi bilioni 50.85 ni mkopo toka benki ya AfDB na benki hiyo ilitoa
fedha nyingine shilingi bilioni 6.10
zilikuwa ni msaada. UN-Habitat ilitoa msaada wa shilingi bilioni
2.50
Kwa
upande wake Serikali ilitumia shilingi bilioni 8.28 kwa ajili ya kulipa fidia
mali na mazao ya wananchi yaliyathirika na ujenzi wa maradi pamoja na kupeleka
umeme katika vituo vya maji.
Alifafanua
kuwa kukamilika kwa Ujenzi wa Miundombinu ya Kuimarisha na Kuendeleza huduma ya
Maji na Usafi wa Mazingira katika miji mitatu ya Pemba (Chake-Chake,Mkoani na
Wete) tayari kumewezesha wananchi 70,852 kupata huduma hiyo.
Alibainisha
kuwa sehemu hiyo ya mradi ilihushisha uchimbaji wa visima 18 pamoja na ujenzi
wa vituo na kufunga pampu,kuchimba misingi na kulaza mabomba kilomita 83.5 na
ujenzi wa matangi 6 ya ardhini na ya minara yenye uwezo wa kuhifadhi lita
7,600,000 kwa pamoja.
Alieleza
matangi mawili yamejengwa Taifu -eneo ulipozinduliwa mradi na Mtemani katika
wilaya ya Wete, Machomane Chake-Chake na Uweleni Mkoani.
Kwa
upande wake Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Bwana Sabas
Marandu mbali ya kueleza kuridhishwa kwake na ushirikiano ambao Benki yake
imeupata kutoka serikalini na ZAWA wakati wote wa utekelezaji wa mradi huo
alimhakikishia Mheshimiwa Rais kuwa fedha za mradi huo zimetumika kama
ilivyopangwa.
Dk.
Shein yuko kisiwani Pemba kwa ziara siku nne kuanzia jana kukagua shughuli za
maendeleo ikiwemo kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbali mbali katika
sekta za elimu, maji, barabara na mazingira.
Postal Address: 2422 Tel.:0776 613 015 Fax:
024 2231822
No comments:
Post a Comment