Habari za Punde

Wakulima wa Halizeti Pemba kupatiwa mashine


Na Haji Nassor, Pemba

WAKULIMA wa zao la halizeti kisiwani Pemba, wametolewa shaka na Wizara ya Kilimo na Maliasili Zanzibar, kuhusu kupatikana kwa mashine ya kukamulia mafuta ya halizeti, mara baada ya uvunaji wa zao hilo.

Akizungumza na wakulima wa zao hilo katika uzinduzi wa uvunaji wa halizeti kwa wakulim wa bonde la Dobi Wawi Waziri wa Kilimo na Maliasili Zanzibar dk. Sira Ubwa Mamboya alisema, serikali kupitia wizara hiyo itahakikisha wakulima wanapata mashine baada ya muda mfupi ujao.

Alieleza, serikali italeta mashine kubwa na ambayo itaweza kutoa mafuta yenye kiwango, hivyo ni vyema wakulima wakaotesha kwa wingi, ili lengo liweze kufikiwa.

Alisema, kwa sasa wizara itaweza kuleta mashine moja pekee katika kisiwa cha Pemba, kutokana na kuwa bado uzalishaji ni mdogo, lakini mara baada ya kuongezeka zitawekwa kila wilaya.

‘’Zao la halizeti ni geni katika visiwa vya Zanzibar, lakini endapo wakulima wataweza kuotesha vizuri wanaweza kufaidika na kulipa umaarufu muda mfupi tu ujao’’, alisema Waziri.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Maliasili Zanzibar Affan Othman Maalim alisema, wakati umefika sasa kwa wakulima kuibua kilimo ambacho kitaingia katika biashara, ili kujinasua katika wimbi la umasikini.

Alieleza, kilimo chochote kwa sasa lazima kilimwe kibiashara kutoka na hali ya uchumi wa dunia, ili wakulima waweze kufaidika kwa namna moja au nyengine kupitia zao hilo.

‘’Endapo mutalima kibiashara na kuhakikishieni mutaweza kufaidika, kwani kilimo ni ajira pekee ambayo inaweza kuajiri walio wengi’’, alieleza Katibu Mkuu.

Nae, Afisa mdhamini wizara hiyo Suleiman Sheha Muhamed aliwahikikishia wakulima hao kuwa, watakwena sambamba kwa kila hali, ili kuhakikisha wanafikia lengo walilojiwekea.

Alifahamisha, zao la halizeti halina kinyongo kwani mahali popote linaweza kustawi vizuri, hivyo ni jukumu lao wakulima kuhakikisha kuwa wanaotesha kwa wingi kwa maslahi yao na taifa kiujumla.

Akisoma risala kwa niaba ya wakulima wenzake Khamis Mohamed Yahya, alizitaja changamoto ambazo zimewakali katika kuotesha zao hilo na kusema, ni pamoja na ukosefu wa taaluma na pembejeo.

Alisema, ni vyema serikali kupitia wizara husika kuyaangalia kwa kina matatizo hayo na badala yake kuyapatiwa ufumbuzi kwani wameamua kuotesha zao hilo kwa kupata maslahi.

Ushirika huo wa ukulima wa zao la halizeti una jumla ya  wanachama 19 wakiwemo wanaume 13 na wanawake 6 na hii ni mara ya mwanzo kuvuna zao hilo katika ushirika wao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.