STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
26 Agosti , 2015

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Wizara
ya Miundombinu na Mawasiliano pamoja na Mfuko wa Barabara wametakiwa
kuhakikisha kuwa wanakuwa na mpango maalum wa kuzifanyia matengenezo barabara
nchini ili barabara hizo ziweze kudumu kwa muda mrefu.
Akizungumza
mara baada ya kuzindua rasmi barabara za Wete-Gando na Wete Konde jana Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alisema
kumekuwa na ulegevu katika kuzifanyia matengenezo barabara na matokeo yake ni
barabara hizo huachwa hadi kufikia hali ya kuharibika kabisa.
Katika
hafla hiyo iliyofanyika huko katika kijiji cha Ukunjwi, wilaya ya Wete, Mkoa wa
Kaskazini Pemba, Dk. Shein alibainisha kuwa azma ya serikali ni kuhakikisha
kuwa kisiwa cha Pemba sasa kinaunganishwa kwa barabara kila upande kama ilivyo
kwa kisiwa cha Unguja hivyo serikali imo mbioni kutekeleza mradi wa ujenzi wa
barabara ya Ole hadi Kengeja (35 km) ambayo ilibuniwa na Rais wa Kwanza wa
Zanzibar Mzee Abeid Amani Karume.
Alieleza
pamoja na barabara hiyo, serikali inaifanyia marekebisho makubwa barabara ya
Ole hadi Konde ambayo ni ya kiwango cha lami kuimarisha uwezo wake na pia
barabara ya zamani kutoka Chake-Chake hadi Wete (22.1 km) ujenzi wake utaanza
hivi karibuni kupitia fedha za mkopo wa Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya Uchumi ya Afrika (BADEA) na Mfuko
wa Maendeleo wa Saudi Arabia(Saud Fund).
Dk.
Shein alitoa wito kwa wananchi kuzitunza barabara hizo kwa kuepuka vitendo
vinavyopelekea kuharibu barabara ikiwemo uchimbaji wa mchanga na mawe maeneo ya
barabara pamoja na kutoondoa alama za barabarani yakiwemo mabango mbalimbali
yanayoelekeza watumiaji wa barabara hizo.
Kuhusu
kukamilika kwa ujenzi wa barabara za Wete- Gando na Wete- Konde
Dk. Shein
aliwapa changamoto wananchi kwa kuwataka kuzitumia barabara hizo kujiimarisha
kiuchumi kwa kupanua shughuli zao za uzalishaji mali ikiwemo kilimo cha matunda
na mbogamboga.
Aidha
aliwakumbusha kuwa kwa kukamilika barabara hizo maana yake ni kuvifungua vijiji
hivyo kwa watu kutoka nje hivyo wajiandae kuwapokea wageni na kuwakumbusha
kuendeleza utamaduni na sifa ya ukarimu za wananchi wa Unguja na Pemba.
Aliwatahadharisha
wananchi dhidi ya kukaidi amri ya serikali ya kutojenga katika maeneo
yaliyotengwa kwa ajili ya upanuzi wa barabara yaani hifadhi ya barabara kwa
kuwa kufanya hivyo ni kinyume na sheria.
Aliagiza
Wizara ya Miundombinu kuwataka wananchi wanaokaidi amri hiyo kuvunja majengo
yao wao wenyewe vinginevyo Wizara ichukue hatua za kuyavunja majengo hayo.
Aidha
aliwataka kuacha na vitendo vya kulala barabarani nyakati za usiku kwa kuwa kufanya hivyo
kunahatarisha maisha yao kwani barabara hizo hutumika kwa vyombo vya usafiri
wakati wote.
Dk.
Shein alitumia fursa hiyo kuushukuru uongozi wa Ufalme wa Saudi Arabia pamoja
na Uongozi wa BADEA kwa kuendelea kuiunga mkono jitihada za
Serikali na
wananchi wa Zanzibar za kujiletea maendeleo.
Katika
maelezo yake kumkaribisha Mgeni, Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano
Issa Haji Ussi (Gavu) alieleza kuwa Wizara yake inakusudia kuweka taa za
kuongozea magari katika makutano ya
barabara ya Gando, Chake-Chake na Kizimbani.
Aidha
aliongeza kuwa Wizara hiyo imeweka viguzo maalum za kuonesha mipaka ya barabara
na kutoa wito kwa wananchi kuheshimu maeneo hayo yaliyotengwa.
Kuhusu
fidia Naibu Waziri huyo alikiri kuwa bado wizara yake haijakamilisha ulipaji wa
fidia kwa baadhi ya wananchi walioathriwa na ujenzi wa barabara ya Wete – Gando
na kwamba fidia hiyo italipwa.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Dk. Juma Akil
alieleza kuwa barabara hizo zenye urefu wa kilomita 30.2 ni utekelezaji wa
Awamu ya Kwanza ya ujenzi wa barabara tatu za mkoa Kaskazini Pemba zenye urefu
wa kilomita 52.2.
Alifafanua
kuwa Awamu ya Pili itakuwa ni ujenzi wa barabara ya Wete- Chake-Chake ambao
ujenzi wake unaanza mara moja baada ya kukamilika ujenzi wa Awamu ya Kwanza.
Dk.
Akil alifafanua kuwa ujenzi wa barabara hizo ambao uliofanywa na Kampuni ya
Mwananchi Engineering and Contractors Limited (MECCO) ya Tanzania umegharimu
jumla ya shilingi bilioni 36 badala ya shilingi bilioni 23.7 zilizopangwa awali
kutokana na sababu mbalimbali.
Alizitaja
baadhi ya sababu hizo kuwa ni ucheleweshaji wa malipo ya fidia kwa wananchi na
kuchelewa malipo ya hati mbalimbali za madai ya malipo za mkandarasi kutoka
pande zote zinazogharamia mradi huo.
Alibainisha
kuwa mchango wa serikali katika mradi huo ni kulipa fidia wananchi ya nyumba,
vipando na uhamishaji wa huduma za jamii ikiwemo mabomba ya maji, umeme na simu
na kulipa asilimia 28.6 ya kila hati ya malipo ya mkandarasi.
Postal Address: 2422 Tel.:0776 613 015 Fax:
024 2231822
No comments:
Post a Comment