Habari za Punde

Dk Shen awahakikishia wananchi kwamba haki ya kila mpiga kura itaheshimiwa na kulindwa

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                             27 Agosti, 2015
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza tena dhamira ya kweli ya serikali ya kufanya uchaguzi huru na wa haki hivyo kuwahakikishia wananchi wote wenye haki ya kupiga kura kuwa wataweza kutumia uhuru wao kuwachangua viongozi wanaowapenda.

“kila mwananchi mwenye haki ya kupiga kura haki yake italindwa. Tutafanya uchaguzi huru na wa haki wala wananchi wasitiane hofu” alisema Dk. Shein jana wakati akizungumza na wana CCM na wananchi wa kijiji cha Kangagani,Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Dk. Shein, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, alisimama katika tawi la CCM la Kangagani wakati alitokea mji wa Wete ambako asubuhi alizindua Mradi wa Hifadhi ya Misitu Asili (HIMA) huko katika kijiji cha Makangale.    

Aliwaeleza wananchi hao kuwa wakati wote wa kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake amekuwa akihimiza sana upendo na mshikamano miongoni mwa wana CCM na baina ya wana CCM na wanachama na wapenzi wa vyama vingine kwa kuamini kuwa wananchi wa Zanzibar ni watu wamoja hivyo hawana sababu za kuhitilifiana kwa sababu za kisiasa.

“Nitashangaa sana nitakapowaona wananchi wa Pemba wanashikana mashati kutokana na tofauti zao za kisiasa wakati wa uchaguzi” Dk. Shein alieleza.


Kwa hivyo alitoa wito kwa wananchi wote kuwa watulivu na kuishi kwa upendo miongoni mwao na kuwanasihi kuacha kuchukiana, kufarakana wala kujenga chuki miongoni mwao kwa sababu za itikadi za vyama na kusisitiza kuwa uchaguzi utakapofika washindane kwa “sera si kwa matusi wala kukashifiana”.

Dk. Shein ambaye anagombea tena nafasi ya urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi aliwahakikishia wananchi hao kuwa vyombo vya dola vipo kwa ajili ya kuwatumikia kwa kuwapatia ulinzi na usalama wao na mali zao na kamwe havina ugomvi nao.

Hata hivyo alionya kuwa si vyema wananchi kupimana misuli na vyombo hivyo hasa vijana hivyo akawatahadharisha dhidi ya kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani.

“Wazee na kinamama mara nyingi wamekuwa watulivu lakini wako baadhi ya vijana wanafanya vitendo vya uvunjifu wa amani kwa makusudi na kuvilazimisha vyombo vya dola kutumia nguvu. Nawatahadharisha hivyo sivyo” Dk. Shein alionya.

Akizungumzia kwa ujumla uongozi wake wa serikali ulio katika mfumo wa umoja wa kitaifa, Dk. Shein aliwaeleza wananchi hao kuwa ilikuwa changamoto kubwa kwake lakini ameweza kuanzisha na kuiongoza kwa mafanikio makubwa.

“Nakumbuka wakati nilipofika hapa kuomba kura mwaka 2010 niliwaeleza kuwa mkinichagua changamoto ya kwanza ni kuunda serikali yenye mfumo wa umoja wa kitaifa lakini niliwaahidi kuwa nitalifanya hilo kwa mafanikio makubwa na kwa hakika nimeweza kwani sasa tumekaribia mwisho wa safari yenyewe kwa awamu hii ya miaka mitano” Dk. Shein alieleza.

Katika kipindi cha uongozi kinachomalizika, Dk. Shein aliwaeleza wananchi hao kuwa serikali imeweza kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa zaidi ya asilimia 90 na kuwataka wana CCM wasiwe wanyonge kwani Ilani yao ndio iliyoendesha serikali pamoja na mipango mengine ya maendeleo ikiwemo MKUZA II na Dira ya Maendeleo 2020.

Aliwafafanulia wananchi hao kuwa Ilani ilitoa maelekezo kwa kila sekta ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii hivyo wanapaswa kujivunia utekelezaji wa Ilani yao kwa kiwango hicho kikubwa.

Nao wanaCCM na viongozi wa chama hicho walimuhakikishia Dk. Shein kuwa wataendelea kuiunga mkono CCM sambamba na kumuunga mkono yeye pamoja na wagombea wote wa katika uchaguzi mkuu ujao.

Dk. Shein yupo kisiwani Pemba kwa ziara ya siku nne kuangalia miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali. Hadi sasa amezindua miradi mine yote katika wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskzini Pemba.

Miradi hiyo ni Tawi la Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar-SUZA huko Mchangamdogo, Mradi wa Maji Safi na Salama na Hifadhi ya Mazingira huko Taif, barabara za Wete –Gando na Wete-Konde na mradi wa hifadhi ya Mazingira ya Misitu ya Asili-HIMA huko katika kijiji cha Makangale.

Akiwa katika siku yake ya tatu ya ziara yake kisiwani humu leo Dk. Shein anatarajiwa kuzindua Kiwanja cha Kufurahishia watoto kilichoko Tibirinzi wilaya ya Chake-Chake na baadae mchana atakwenda wilaya ya Mkoani kuweka jiwe la msingi la hospitali ya Abdalla Mzee ambayo inajengwa upya kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya watu wa China.

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.