Habari za Punde

Mansour Yussuf Himid kugombea jimbo la Chukwani badala ya Kiembesamaki: ni kula matapishi yake au bao la kisigino?


Na Mwandishi maalum

Wakati vuguvugu la uchaguzu likikaribia na zikibaki ziku chache kabla ya  firimbi kupulizwa kuanza kampeni za uchaguzi ambao utafanyika hapo Okotba 25 kuna mengi yamejitokeza na ya kufurahisha ya kushtukiza pamoja na mengine ya kushangaza.  Viashiria vyote hivyi vinaonesha uchaguzi wa mwaka huu unaweza ukaleta matokeo ya kushangaza sana na yasiyotarajiwa

Moja katika mpambano  wa kisiasa uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu ulikuwa katika jimbo la Kiembesamaki ambapo Mwakilishi aliepo Mahmoud Thabit Kombo ambaye ni naibu Waziri wa afya alitarajiwa atapambana na kukutana uso kwa uso na Mwakilishi aliepoteza jimbo hilo baada ya kuvuliwa uanachama wa CCM, Mansour Yussuf Himid.

Ulikuwa ni mpambano wa aina yake kutokana na historia inayofanana ya vijana hawa wawili waliozaliwa na kulelewa na wanamapinduzi. Mahmoud ni mtoto wa aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu wa ASP Thabit Kombo Jecha na mwanamapinduzi, Mansour ni mtoto wa aliyekuwa mwanamapinduzi brigerdier Yussuf Himid Mkuu wa Kwanza wa Vikosi vya SMZ baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964.

Mahmoud na Mansour wote wamewahi kuwa mawaziri katika serikali ya Rais Amani Karume, wajumbe wa NEC ya CCM na wawakilishi wa majimbo ya Mpendae na Kiembesamaki kabla ya Mahmoud kuhamia Kiembesamaki baada ya kufukuzwa uanachama wa CCM kutokana na kwenda kinyume na maadili.

Kwa historia hii na mazingira ya jimbo la Kiembesamaki ambalo CUF wameona uwezekano wa kulinyakua kupitia turufu ya Mansour wakati CCM wakihakikisha linabaki katika mikono ya CCM kwa turufu ya Mahmoud.

Mpambano huu ulitarajiwa utokee kwenye uchaguzi mdogo wa jimbo la kiembesamaki ila Mansour, sijui ni kwa kushauriwa ua kwa kusoma alama za nyakati, hakupendekezwa na chama chake kipya cha CUF alichojiunga kugombania uwakilishi wakati huu.


Mansour aliwahi kunukuliwa akisema ikiwa ataamua kurudi tena kwenye ulingo wa siasa atawania katika Jimbo la Kiembesamaki ambako amewekeza na anadai anakubalika.

Wakati majina ya wagombea uwakilishi yakisubiriwa kwa hamu hasa kwa jimbo la Kiembesamaki na CUF kutangulia kutangaza majina ya wagombea 04/06/2015, Mansour alitajwa kwamba atagombea jimbo la Kiembesamaki. Tulipowasubiri CCM kutangaza nao pia walitangaza kwamba Mahmoud atagombea jimbo la kiembesamaki tarehe 13/08/2015. Tuliokuwa tukisubiri mpambano huu tukaona sasa mambo yamewiva tutaweza kushuhudia tukio la kihistoria kwenye kampeni na mpaka kwenye uchaguzi.

Wakati haya yakitokea Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ikatangaza majimbo mengine mane mapya na kuwa 54 badala ya 50 yaliyokuwepo. Moja katika jimbo jipya ni jimbo la Chukwani.

Ujio wa jimbo la Chukwani ulifungua mlango mwengine ambao haukutarajiwa kwa vyama vyote viwili kwani ZEC ilifanya siri kubwa kuyatangaza majimbo mapya na kuyaunganisha mengine kutokana na jinsi ya mji unavyokuwa na watu kuhama na kuhamia sehemu nyengine. Pia CUF walipotangulia kutaja majina ya wagombea kabla ya ZEC kutangaza majimbo kumeleta sintofahamu kidogo ambayo inaweza kuwa ni neema pia.

Pengine CUF waliiona hii ni fursa nzuri ya kujihakikishia kuepuka mpambano kati ya Mahmoud na Mansour wakaamua kurusha taula kabla ya mpambano kuanza, kumuachia jimbo Mahmoud ambae ninaamini amepata kupumua sana kwa kuwa angelikuwepo Mansour, ingebidi itumike nguvu kubwa sana kwenye kampeni. Pia ni kama kula matapishi yake Mansour ambae alituhakikishia kwamba akirudi kwenye siasa atagombea jimbo hili. Hivyo CUF walipotangaza tena majina ya wagombea, Mansour atagombea jimbo la Chukwani badala ya Kiembesamaki.


Ila kwa upande mwengine wa shilingi, naamini huu ni mkakati ambao ninaweza kusema ni ‘bao la kisigino’ kwani Mansour kugombea jimbo jipya la Chukwani dhidi ya mgombea wa CCM, Mwanaasha Khamis Juma, uwezekano wa kulichukua CUF jimbo hili ni mkubwa endapo CCM halitopiga ‘bao la mkono’ kama ilivyo kwa Mahmoud kushinda jimbo la Kiembe Samaki dhidi ya mgombea wa CUF, Mohammed Nassor Mohammed pia kwa ‘bao la kisigino’ na hatohitaji ‘bao la mkono’.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.