Habari za Punde

Dk.Shein Arejesha Fomu na Kusema: Tumejiandaa vya Kutosha Kushinda Uchaguzi

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                    05 Septemba, 2015
---

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mgombea nafasi ya Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amerejesha fomu ya kugombea nafasi hiyo Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na kuwahakikishia wanachama na wapenzi wa CCM pamoja na wananchi wa Zanzibar kuwa chama hicho kimejiandaa vya kutosha na kimejidhatiti kuhakikisha kinashinda uchaguzi na kushika dola kwa mara nyingine.

Akizungumza katika Ofisi Kuu ya chama hicho Kisiwandui akitokea Ofisi za muda za Tume ya Uchaguzi Zanzibar huko katika Hoteli ya Bwawani Dk. Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Mapinduzi, alisema chama hicho kimejiandaa na kiko tayari kwa uchaguzi.

“”Sisi tuko tayari kwa uchaguzi, tumekamilika katika kila idara, tutaanza kwa gia kubwa na hatufanyi utani lazima (wapinzani) waisome namba” alisisitiza Dk. Shein.

Akielezea mchakato mzima wa kujaza na kurejesha fomu ZEC, Dk. Shein alisema haikuwa kazi rahisi kwa kuwa nyaraka za Tume ni nyingi na zilihitaji umakini mkubwa.

“Ninawashukuru viongozi na wanachama wa chama chetu katika ofisi zetu zote Unguja na Pemba pamoja na wananchi wengine kwa kunisaidia kufanikisha mchakato huu na hatimae leo nimeweza kurejesha fomu hizo” Alieleza Dk. Shein.

Mara baada ya kuwasili katika ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui akitokea Hoteli ya Bwawani, Dk. Shein alisalimiana na wanachama na wapenzi wa chama hicho pamoja na wananchi waliokuwa wakimsubiri katika ofisi hizo.

Wakati huo huo Mgombea wa CCM kwa nafasi ya Urais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein ameelezea matumaini yake kuwa uchaguzi mkuu ujao utakuwa huru na wa haki.

Akizungumza huko katika Hoteli ya Bwawani mara baada ya kurejesha fomu ya kugombea Urais wa Zanzibar kupitia CCM leo, Dk. Shein alisema kuwa Tume ya Uchaguzi ni huru na anatarajia itaendelea kusimamia haki katika uchaguzi kama ambavyo imekuwa ikifanya huko nyuma.

Katika mnasaba huo alisema ana matumaini makubwa kuwa wananchi wa Zanzibar wataweza kutumia vyema haki yao ya kupiga kura kuwachagua viongozi wanaowataka.

Kuhusu ujazaji wa fomu Dk. Shein alimthibitishia Mwenyekiti wa Tume na Makamishna wake kuwa alijaza fomu hizo kwa kufuata maelekezo yote aliyopewa pamoja na maelezo mengine yaliyomo katika fomu hizo.

Dk. Shein aliwasili katika Hoteli ya Bwawani saa nne kasoro dakika tano na kwenda moja kwa moja ukumbini ambako alipokelewa na viongozi wa ZEC wakiongozwa na Mwenyekiti wake Bwana Jecha Salum Jecha pamoja na viongozi wa Chama cha Mapinduzi wakiongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho Balozi Seif Ali Iddi ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 
                                                

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.