MJASIRIAMALI anatengeneza bidhaa
zinazotokana na vyuma, ikiwa ni pamoja na milango, majiko na madirisha, Khamis
Ali Makame alieaajiri vijana watatu wenye ulemavu eneo la Wawi wilaya ya Chake
Chake Pemba, (Picha na Zainab Atupae,
Pemba).
VIJANA watatu wenye ulemavu wa viungo ambao
wameajiriwa na mjasiriamali wa kutengeneza bidhaa zinazotokana na vyuma Khamis
Ali Makame, wakishauriana jambo kalba ya kuanza kazi hiyo, kwenye afisi yao
iliopo Wawi Chake Chake Pemba, (picha na
Zainab Atupae, Pemba).
Amewaajiri wenye ulemvu watatu, apunguza
foleni ya ajira serikalini
Na mwandishi wetu- PEMBA
Khamis Ali Makame ni mjasiri amali wa
uchomaji vyuma katika kijiji cha Wawi ,
aliyefanikiwa kupata mafanikiyo yake kwa
kazi hiyo.
Aliezaliwa
katika kijiji cha Mchangani Vitongoji
Chake Chake, na sasa ana umri 30, na
alipata elimu yake ya msingi skuli ya Vitongoji, na kumaliza darasa la
saba na hakuendelea tena.
“Kiukweli
kusoma sikuwa na ari .….. kwani nimemaliza darasa la saba ila tokea zamani ilikuwa napenda niwe na kazi hii ya uchomaji vyuma na niliamini ikosiku nitapata”, alisema
mjasiri amali huyo.
Wahenga
walisha nena kuwa “jitihada wajada” yaani anaetafuta hakosi na ikosiku utapata,
usemi huu umemnufaisha vyema kijana Khamis.
“Hakuna kazi rahisi, maana hata hii yangu sio
nyepesi, maana wakati napewa ujuzi na kaka yangu, niliona ugumu
wake’’,aliniambia huku akikata chuma.
Huku
kijasho chemba mba kikimtiriri kwenye paji lake la uso, na ili kufanikisha kazi
yake, utaalamu na nguvu kidogo ni jambo la lazima.
Ofisi
hiyo inatengenezwa vitu tofati ikiwa ni
pamoja na kutengeza milango ya mageti, madirisha ya mageti, majiko ya vyuma na
misheki ya kutolea moto.
Kijana huyo mchakarikaji wa maisha,
alinihadithia kuwa, alianza kuvisarifu vyuma kwa kuchukuliwa na kaka yake kazini,
tokea mwaka 2005, akiwa miongoni mwa wanafunzi sita.
“Namini
kila aliye kwenda pale alikuwa na hamu ya kutaka kupata ule ujuzi, na kuhakisha
baadae anajiajiri mwenyewe.
Kadri
siku zilivyokuwa zikisonga mbele, na yeye kuendelea kujichotea ujuzi kwa kaka
yake, alianza kuona nuru ya maisha yake yakimsogolea.
Miaka
10 baade, baada ya kujiweza kimaisha, akiamini sasa hakuna chuma kinachomshinda
kukikata apendavyo kama papai, alianza taraibu kuondoka.
“Unajua
mwandishi, nilipofika miaka 10 ya kumfuata kaka kuusaka ujuzi wa kubena vyuma,
nilijiona kama sasa naweza kujitegemea’’,alidakiza kwa furaha.
Suali:
ni mwaka gani umeweza kujipatia ofisi
yako maalumu na kuweza kuwaajiri watu
wako.
Mwaka
jana, kijana Khamis sasa rasmi alikata shauri na kuamua kutafuta sehemu yake,
ili kujiendeleza na sasa akitaka kuyasahau machungu ya miaka 10.
“Unajua
maisha ni safari yenye changamoto, sasa usipojitambua unaweza kukata tamaa
mapema, mimi leo nnafuraha ya kua na ofisi yangu binafi bila ya kutegemea mtu”,alisema.
Oktoba
12 mwaka 2013 alipata kiwanja chake eneo la Wawi wilaya ya Chake Chake mita chache kabla ya
kukifikia kiwanda cha mafuta ya makonyo, ambapo ndipo alipoangusha nanga ya
maisha.
“Kila
penye nia pana njia, Mungu alinipa uwezo wa kupata sehemu yangu ya kujiendeleza na kuwatafuta watu ambao nilikuwa na nia nao ya kuwajiri katika ofisi yangu’’,alifafanu.
Mjasiriamali
huyo, wakati akiwa kwenye mafunzo ya kuchoma na kukata vyuma, alijiwekea
malengo ya kuwajiri watu wenye ulemavu, akiamini kwamba ndio kundi lililokosa
uwangalizi.
“Husikia kwenye vyombo vya habari, kwamba
wenzetu wenye ulemavu, wanakosa ajira hata kama watakuwa na sifa, ndio maana
mimi nimeamua kuwaleta hapa kusaka nao maisha”,alieleza.
Roho
ya mjasiriamali huyo, kwa sasa imetulia tuli, kama maji mtungini, maana
ameshajiekeza kwenye ofisi yake na amewaajiri vijana watatu kuendelea kuvitesa
vyuma.
Vijana
hao ambao nao ni wataalamu wa kukifanya chuma kama karatasi, alianza nao kusaka
ujuzi, miaka 10 iliopita na baada ya yeye kujiona anajiweza ndio akawatupia
jicho.
Wafanya
kazi wanaokula mzigo kwenye ofisi hiyo ambao wanaulemavu, ni kijana Said Ali
Saadun, Salum Bakar pamoja na Rashid Salum.
Kwa
pamoja wenyewe walisema hawaamini kwamba kijana Khamis, amewachukua kwenye
ofisi hiyo na kuendelea na kazi ya kuvichekecha vyuma .
“
Sisi hapa twashukuru sana, maana tupo tunaganga njaa na mwenzetu, maana
tulikuwa tumeshakwama kimaisha, hivyo fursa aliotupa Khamis twashukuru’’,walieleza
kwa furaha.
Mjasiriamali
huyo kwa kushirikiana na wapiganaji wake, wakiwa wanajikita kwenye kutengeneza
bidhaa zote za vyuma, kama milango ya mageti, anafurahia kazi wanazozifanya.
“Sisi
ambao tunajidanganya kwamba hatuna ulemavu, hatuna huruma na wenye walemavu, hatutaki
kuwasaidia kisha tukadai hawezi
kufanya kazi”, alisema kwa uchungu.
Katika
kufanikisha kazi zao, alisema amewashawapangia bei kila bidhaa, ili wanapofika wateja, wawe na kauli
moja.
Kwa
sasa kwenye ofisi hiyo ya mjasiriamali Khamis Makame Ali, mlango mmoja wa geti hupatikana kati ya shilling 200,000 hadi
shilingi 250,000 wakati na dirisha moja kutegemeana
na ukubwa na aina, huanzia shilingi 80,000.
Jiko
la kawaida kwa mjasiriamali huyo huuza kati ya shilingi 10,000 na mchoteo wa
mkaa (mshebeki) hupatikana kwa shilingi 2,000.
“Unajua
kila penye mafanikio, elewa na changamoto
hazichezi mbali, maana wateja kwanza
ndio kilio chetu’’,alieleza.
Bei
ni ndogo ukilinganisha na gharama inayotumika katika kutengeza bidhaa, na hata
hutokezea siku nyengie kukosa mteja hata mmoja.
Kijana Khamis alianza na mtaji wa shilingi laki 800,000
kwa kujinunulia malighafi ambapo kwa sasa anabidhaa ambazo kama akiziuza
anaweza kujipatia shilingi laki 400,000 hadi laki 500,000.
Hata
hivyo, aliahidi kuendelea kujitengenezea njia ya maisha na anaamini iko siku
atafikia malengo yake kwenye kazi hiyo.
Haridhishwi
hata kidogo kuona vijana wenye nguvu na maarifa wakiishia vijiweni, kwa vile
zipo kazi za kujishughulisha na kujipatia walau shilingi ya chakula.
Kijana
huyo kwa kauli yake, alisema anashangaa kuona wapo watu na taasisi za umma
wakiendelea kuwatenga watu wenye ulemavu, na kuwajengea dhana kwamba hawawezi.
Ameishauri
Serikali na viongozi wengine kuwapa kipaumbele watu wa kundi hilo, ili kuona
wanapata mitaji kupitia ofisi yake..
No comments:
Post a Comment