Habari za Punde

Tanzania Yautaka Umoja wa Mataifa Kuzingatia Misingi Iliyojiwekea.

Mwakilishi wa  Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akizungumza wakati wa  Mkutano wa Bodi za Mashirika na  Mifuko ya Umoja wa Mataifa  siku ya jumatatu, ambapo pamoja na mambo mengine ameutaka Umoja wa Mataifa kutekeleza majukumu yake  kwa  kuzingatia misingi iliyojiwekea na pia kutowapa  nafasi  watendaji  wenye ushabiki na  wanaoweka mbele maslahi binafsi. Walioketi nyuma ni  Maafisa wa Uwakilishi  Bw. S. Shilla  na Bi, Lilian Mkasa

Na  Mwandishi Maalum, New  York
Wakati  Tanzania ikipongeza, kusifu na kushukuru uhusiano na ushirikiano wake na Umoja wa Mataifa kupitia Mifuko na Mashirika yake ya Maendeleo,  imeutaka pia Umoja huo kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia, kanuni, taratibu, sheria na misingi iliyojiwekea ili iendelee kujijengea heshima.

Hayo yameelezwa jana jumatatu na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, wakati wa mkutano wa Bodi za Mashirika ya Umoja wa Mataifa UNDP, UNFPA na  UNOPS.    Tanzania ni mjumbe wa Bodi katika Mashirika hayo.

Katika siku ya kwanza ya mkutano ,uliofunguliwa na Mtendaji Mkuu wa UNDP, Bi Helen Clark, Balozi Manongi amesisitiza kwamba,  ili Umoja wa Mataifa uendelee kujijenga heshima na kuheshimika,  unapaswa kutoruhusu watendaji wenye ajenda na maslahi binafsi kufanyakazi katika Mashirika ya Umoja wa Mataifa.
“ Umoja wa Mataifa wakati wote umekuwa sehemu na mdau mkubwa katika uimarishaji na ujenzi wa utawala bora katika nchi nyingi, Tanzania  ikiwamo.

Wajibu wa Umoja wa Mataifa utabaki kuwa halali na wenye nguvu endapo wale ambao wamepewa dhamana ya kutenda kwa niaba yake watatambua na kuheshimu imani na wajibu uliotukuka ambao wamepewa  kuutekeleza” akasisitiza Balozi Manongi.

Akaongeza kwamba, mashabiki hawapaswi kupewa nafasi, wala kuvumiliwa na kuwa sehemu ya miongoni mwa watendaji wa chombo hicho wasipewe nafasi,wala wasivumiliwe kuwa miongoni mwa watendaji wa chombo hicho.


Akizungumzia kuhusu rasimu ya Taarifa ya Mpango wa Utekelezaji kuhusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Country report) kwa kipindi cha 2016-2021) ambayo imewasilishwa mbele ya Wajumbe wa Bodi ya UNDP,  Balozi Manongi amesema, mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu na ambayo imeshirikisha wadau mbali mbali inajumuisha mawazo na mapendekezo kutoka pande zote za Muungano na imetokana na misingi ya ushirikiano kati ya UNDP na Serikali ya Tanzania.

Vile vile akasema rasimu hiyo imejumuisha vipaumbele vinavyoainishwa katika Dira ya Taifa ya 2025 kwa upande wa Tanzania Bara ,Dira ya  2020 kwa upande wa  Zanzibar,  mkakati wa kupunguza umaskini kwa pande zote za Muungano pamoja na Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano.

“Tunaishukuru UNDP- Ofisi ya Tanzania kwa ushirikiano wake katika utekelezaji wa mipango mbali mbali ya maendeleo ikiwano mikakati ya kupunguza umaskini, ushirikiano huu umekuwa mzuri ingawa unachangamoto zake” akasisitiza Balozi Manongi.

Akaeleza kwamba, kutokana na umuhimu wa mwaka huu wa 2016 ambao pamoja na mambo mengine ni kuanza kwa utekelezaji wa Agenda ya Maendeleo Endelevu ( Agenda 2030) Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na  UNDP katika utekelezaji wa  Agenda hiyo huku mkazo ukiwa ni katika kupungua kuondoa umaskini uliokithiri kwa makundi mbali mbali ya jamii hususani wanawake.

Akasema,Serikali imejipanga vema katika utekelezaji wa mipango mbali mbali inayolenga katika kuboresha maisha ya wananchi  wake.Ikiwa ni pamoja na kutatua tatizo la uhamaji wa wananchi wake  kutoka vijijini na kwenda katika miji mikuu hususani vijana kwa lengo la kutafuta ajira na hali bora  ya maisha.

Akasema kuwa wajibu au  madhumuni ya msingi  UNDP ni kupunguza umaskini, ni kwa sababu hiyo Tanzania ingependa kuiona UNDP ikijielekeza zaidi katika jukumu lake hilo la msingi kama inavyoelekezwa katika maazimio mbali mbali ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Kwa upande wa ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu zinazohusu maeneo mbali mbali,  Balozi Manongi amesisitiza kwamba  UNDP inapaswa kufanyakazi kwa karibu na kwa ushirikiano na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kile alichosema ndicho chombo cha serikali chenye dhamana juu ya masuala yote ya husuyo takwimu.

Na kwa sababu hiyo akasema Tanzania inaridhishwa na taarifa ya kwamba UNDP itashirikiana na Ofisi hiyo ya Taifa ya Takwimu katika Nyanja mbali mbali zikiwamo za uwezeshaji kwa lengo  la kusaidia katika uhuishaji wa takwimu.

Aidha  Tanzania imesisitiza kuhusu umiliki katika uendeshaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo pamoja na kiushauri  UNDP kuhakikisha kwamba fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinakwenda kufanyakazi iliyokusudiwa na sivinginevyo.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.