Na Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kujenga skuli Mpya Tisa za Ghorofa Unguja na Pemba, ambapo kati ya hizo Skuli Tatu zitajengwa katika Wilaya mbili za Mgharibi “A” na “B” Unguja.
Alisema Serikali imetoa kipaumbele cha kuongeza skuli katika Wilaya hizo mbili kutokana na ongezeko kubwa la Idadi ya Watu ili zitakapomalizika zipunguze au kuondosha kabisa msongamano wa wanafunzi uliopo hivi sasa kwenye skuli nyingi za Wilaya hizo.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati wa hafla maalum ya uzinduzi wa ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Kwarara uliokwenda sambamba na uzinduzi wa ujenzi wa Kituo cha Habari na mawasiliano cha Tumaini kwenye skuli hiyo hapo Kwarara Wilaya ya Magharibi “B”.
Alisema kazi kubwa iliyopo hivi sasa mbali ya kuongeza upatikanaji wa nafasi kwa wanafunzi ni kuwekeza katika kuimarisha ubora wa elimu wanayoipata wanafunzi kwa kuongeza walimu wenye sifa zinazokubalika sambamba na kuboreshwa kwa maslahi ya walimu hao.
Hata hivyo Balozi Seif alisema ushiriki wa washirika wa maendeleo kuunga mkono jitihada za Serikali ni muhimu na mazingira ya ushiriki wao tayari umeshaandaliwa vyema ili waweze kutoa mchango wao wa elimu kwa ufanisi na mafanikio makubwa.
Alieleza kuwa sera ya elimu ya mwaka 2006 imetamka wazi kwamba watoto wote wa Zanzibar wana haki ya kupata elimu ya lazima kwa muda wa miaka 12, kuanzia elimu ya maandalizi,msingi na ile ya elimu ya sekondari ya awali ya miaka minne.
Balozi Seif alisema Serikali iliamua kufanya hivyo kwa kutambua maendeleo ya Taifa yanayotegemea sana uwepo wa nguvu kazi ya Vijana walioelimika na ndio maana awamu ya sita ya SMZ ikawekeza kwenye ngazi hizo kuanzia maandalizi hadi sekondari.
Alisisitiza kuwa yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana akatolea mfano wa mwaka 2015 katika ngazi ya elimu ya msingi wapo wanafunzi wapatao Laki 261,212 sawa na asilimia 98.4 ya watoto wote wanaotakiwa kupata elimu hiyo.
Katika ngazi ya elimu ya sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha Nne Balozi Seif alisema wapo wanafunzi 84,211 sawa na asilimia 62.9 ya wanafunzi wanaotakiwa kupata elimu husika.
Alieleza kwamba hayo ni mafanikio makubwa yakujivunia kwa wananchi wote wa Zanzibar kwani hata baadhi ya mataifa ambayo yana uwezo mkubwa wa kiuchumi kuliko Zanzibar lakini bado hayajaweza kuwapatia elimu wananchi wake kwa asilimia kubwa kama iliyofikia Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza wananchi kwa kutambua umuhimu wa elimu kwa watoto wao, kwani pamoja na uhaba wa nafasi katika skuli mbali mbali lakini bado wamekuwa na mwamko mkubwa wa kuwaandikisha watoto wao kwa wingi.
Alisema kwa vile Serikali inatambua kuwa watoto ndio rasilmali muhimu kwa Taifa, rasilmali hiyo itaienzi, itaitunza na kuiendeleza ili isipotee na kuwanasihi Vijana watakaopata fursa ya kujiunga na skuli hiyo mpya ya Kwarara baada ya kukamilika waitumie nafasi pekee ya kujijengea uwezo wa kujitegemea na kujikomboa.
Akigusia Kituo cha Habari na Mawasiliano cha Tumaini kitakachojengwa kwenye skuli hiyo ya Sekondari ya Kwarara Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amelipongeza Shirika la Habari la Korea Kusini { Seoul Broadcausting System } kwa wazo lake la ujenzi wa Kituo hicho.
Balozi Seif alisema katika ulimwengu wa sasa wa sayansi na teknolojia matumizi ya vifaa vya Habari na Mawasiliano vina umuhimu mkubwa katika utoaji wa elimu hasa ndani ya karne hii ya 21.
Alisema Skuli ya Sekondari ya Kwarara iliyobahatika mwanzo ndani ya Zanzibar kuwa na mpango wa ujenzi wa kituo cha Habari kitakachokuwa na uwezo wa kurikodia matangazo ya Redio na Televisheni kina muelekeo wa Dunia inavyokwenda hivi sasa.
“Nafuraha kubwa kusikia kwamba Kwarara itakuwa skuli ya kwanza na ya aina yake hapa Zanzibar kuwa na Kituo cha Habari na Mawasiliano na huo ndio muelekeo wa Dunia ya leo na ndio hali halisi ”. Alisema Balozi Seif.
Aliushauri Uongozi wa kamati ya Skuli utakaobeba jukumu la kuongoza skuli hiyo kuutaka kukitumia kikamilifu kituo hicho cha Habari na Mawasiliano katika kuandaa vipindi mbali mbali vya kufundishia wanafunzi sio tu kwa skuli hiyo bali pia kwa wanafunzi wa skuli nyengine hapa Nchini.
Mapema Mwakilishi wa Shirika la Good Neighbors Bwana Hwang Sungju, Mwakilishi wa Shirika la Habari la Korea Kusini {SBS } Bwana Lee Woongmo pamoja na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Korea Kusini KOICA wamesifu mashirikiano makubwa waliyoyapata kutoka kwa Wananchi wa Zanzibar.
Wawakilishi hao walisema ushirikiano huo umesaidia kupatikana ufanisi mzuri wa mwanzo wa ujenzi wa Skuli hiyo mpya na kuahidi kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha maendeleo ya elimu Nchini.
Walisema watendaji wa mashirika hayo wanaelewa changamoto zinazowakabili wanafunzi wakati wa kufatufa elimu hasa suala la umbali wa skuli unawasumbuwa baadhi ya wanafunzi hao.
Walieleza kwamba changamoto hizo ndizo zilizosababisha mashirika hayo kuanzisha mradi maalum wa ujenzi wa skuli za kisasa ulimwenguni wakielekeza zaidi nguvu zao katika bara la Afrika.
“Tumeshajenga skuli zipatazo 100 katika nchi mbali mbali Barani Afrika ikiwemo Ethiopia, Kenya, Chad, Malawi, Tanzania Bara na sasa hapa Zanzibar ”. Walisema wawakilishi wa mashirika hayo.
Akitoa salamu Balozi wa Korea ya Kusini Nchini Tanzania Bwana
Song alisema uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya Nchi yake na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla utazidi kuimarishwa hasa katika sekta za Maendeleo ikiwemo ile muhimu ya Elimu.
Balozi Song alisema Korea ya Kusini imefanikiwa kupiga hatua kubwa Kitaalamu hali ambayo imeamua ujuzi huo kuutoa kwa kusaidia nchi marafiki hasa zile za Bara la Afrika.
Ujenzi wa Skuli ya Ghorofa ya Kwarara pamoja na Kituo cha Habari na Mawasiliano uliowekwa jiwe la msingi utakaokuwa na madarasa 12, maabara, Maktaba pamoja na huduma nyengine muhimu unatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi Bilioni 4 sawa na USD za Korea Bilioni 1.6.
No comments:
Post a Comment