Habari za Punde

Balozi wa Comoro, Karume wazungumzia uhusiano




BALOZI wa Visiwa vya Comoro nchini Tanzania Dk. Ahamada El Badaoul Mohamed (kushoto), akizungumza na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Zanzibar, Mhe. Ali Abeid Karume, mbele ya watendaji wa wizara na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika makao makuu ya wizra hiyo huko Kisauni Wilaya ya Magharibi B leo. (Picha na Salum Vuai-Maelezo).


Na Salum Vuai, MAELEZO

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar na Jamhuri ya Visiwa vya Comoro, zina nafasi kubwa ya kubadilishana uzoefu katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Aidha, nchi hizo zimeelezewa kwamba zinapaswa kuimarisha zaidi ushirikiano wao wa miaka mingi unaoambatana na udugu wa damu kati ya watu wa pande mbili hizo. 

Balozi wa Comoro nchini Tanzania Dk. Ahamada Badaoul Mohamed, aliyemtembelea Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Mhe. Ali Abeid Karume leo, amesema udugu wa Comoro,  Zanzibar na Tanzania kwa jumla, unapaswa kuongezewa nguvu.

Amesema nchi hizo zinapaswa kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.


Alieleza, kwa kuwa nchi hizo ni visiwa, kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika usafiri wa baharini ambao kwa muda mrefu umekabiliwa na uhaba wa miundombinu ya uhakika.

Dk. Badaoui amemueleza Waziri Karume kuwa, baada ya Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kutembelea visiwa vya Comoro miezi kadhaa iliyopita, nchi hizo zilisaini mkataba wa ushirikiano unaofungua milango ya kuimarisha sekta za uchumi kati yao.

Kupitia makubaliano hayo, alisema nchi yake na Zanzibar ambazo zina vivutio vingi vya utalii, zinalazimika kuvitumia kuongeza mapato yao kupitia safari za kitalii miongoni mwao.  

Kwa upande wa sekta ya elimu, alifahamisha kuwa, wanafunzi wa Zanzibar wanakaribishwa kujiunga na elimu ya juu katika vyuo vya Comoro, kama wanafunzi wa nchi yake wanavyoweza kuja kusoma katika vyuo mbalimbali vilivyoko hapa nchini.

“Udugu wetu wa damu na ushirikiano wa miaka mingi, ni mambo yanayotuunganisha na lazima sote kwa pamoja tutafute njia za kuuimarisha na kuudumisha,” alifahamisha.

Aidha alisema Zanzibar na Comoro zinafanana kwa mengi, ikiwemo dini na tamaduni zake, na kwamba nchi yake inaangalia uwezekano wa kuleta wanafunzi wake hapa nchini kwa ajili ya kujifunza muziki hasa wa taarab.
Kwa upande wake, Waziri Karume alieleza kufarijika na ujio wa Balozi huyo, na kumtaka ajisikie yuko nyumbani kutokana na muingliano wa watu wa pande mbili hizo.

Waziri Karume amesema, hatua ya Zanzibar kununua meli mpya ya MV Mapinduzi II, ni mwanzo mzuri wa kurejesha safari za kibiashara na za kutembeleana kati ya watu wa nchi hizo.

Alisema Zanzibar imekumbwa na misukusuko kadhaa ya ajali za baharini, lakini sasa hilo litabaki kuwa historia, kwani MV Mapinduzi II ina uwezo mkubwa kuhimili vishindo vya safari kutokana na muundo wake wa kisasa.
Balozi Karume alieleza kuwa mafungamano kati ya wananchi wa Zanzibar na Comoro kwa upande wa dini, tamaduni na ndoa, ni daraja muhimu la kuimarisha uhusiano wao uliodumu kwa miaka mingi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.