Habari za Punde

HOTUBA YA MAONI YA KAMATI YA KUSIMAMIA OFISI ZA VIONGOZI WAKUU WA KITAIFA KUHUSIANA NA MAKADIRIO YA  MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA NCHI, OFISI YA RAIS NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017.

Mheshimiwa Spika,
Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa utukufu, kwa kutujaalia uzima na Afya njema tukaweza kukutana tena katika Baraza hili la Tisa kwa ajili ya kuendelea kuwatumikia wananchi wetu, aidha kukushukuru na kukupongeza wewe Mheshimiwa Spika kwa kuchaguliwa kwako kuliongoza Baraza hili tukufu, ni imani yangu kwamba utaliongoza Baraza hili kwa uadilifu wa hali ya juu na kuimarisha Demokrasia katika chombo hiki muhimu cha wananchi.

Mheshimiwa Spika,
Napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza wawakilishi wote waliomo katika Baraza lako Tukufu kwa kuchaguliwa kwao kuja kuwawakilisha wananchi, ni wazi kwamba wananchi wamejenga imani kubwa kwetu, nasi ahadi yetu kwao ni kwamba tutawatumikia kwa dhati kama ambavyo walivyotuamini kutuleta katika chombo hichi kwa lengo la kutetea maslahi yao.

Mheshimiwa Spika,
Sina budi pia kumshukuru Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na watendaji wake wote wakiongozwa na Katibu Mkuu kwa mashirikiano waliyotupatia wakati wa kupitia makadirio ya Bajeti ya Wizara hii lakini pia nawashukuru Wajumbe wa Kamati yetu kwa umoja wao na kazi nzuri waliyoifanya kiasi cha kunirahisishia kazi yangu ya kuongoza kikao kuwa nyepesi zaidi, kwa hakika ni wajumbe mahiri, ambapo licha ya upya wao katika Baraza hili na hususan katika Kamati hii wameweza kuijadili ipasavyo na kuhoji mambo mbali mbali kwa lengo la kuhakikisha kwamba fedha wanazoidhinisha zinatumiwa kwa matumizi yaliokusudiwa.

Mheshimiwa Spika,
Kwa heshima ya hali ya juu napenda kuwatambua Wajumbe hao kwa majina kama hivi ifuatavyo:-
1.     Mheshimiwa Omar Seif Abeid                                          Mwenyekiti
2.     Mheshimiwa Panya Ali Abdalla                                        M/Mwenyekiti
3.     Mheshimiwa Amina Iddi Mabrouk                                    Mjumbe
4.     Mheshimiwa Hussein Ibrahim Makungu                           Mjumbe
5.     Mheshimiwa Mohammed Said Mohammed                      Mjumbe
6.     Mheshimiwa Mussa Ali Mussa                                          Mjumbe
7.     Mheshimiwa  Mtumwa Suleiman Said                              Mjumbe
8.     Mheshimiwa Simai Mohammed Said                                Mjumbe

Aidha kamati yetu inafanyakazi na makatibu wawili ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakitusaidia sana katika kutekeleza majukumu yetu, makatibu hao ni:-
1.     Ndg Maryam Rashid Ali                                              Katibu
2.     Ndg Othman Ali Haji                                                   Katibu

Mheshimiwa Spika,
Ikumbukwe kwamba miongoni mwa majukumu ya msingi ya Kamati yetu ni kuchambua mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya Wizara husika ya mapato na matumizi ya kila mwaka, hivyo katika kutekeleza jukumu hilo lililoelezwa katika kanuni ya 114(e) kamati yangu ilikaa na kujiadili na hatimae kupitisha Makadirio ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi mnamo tarehe 10/05/2016 na leo hii kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Kamati nawasilisha maoni ya Kamati kuhusiana na Bajeti hiyo.

Mheshimiwa Spika,
Baada ya utangulizi huo mfupi sasa naomba nitekeleze jukumu nililopewa na Kamati la kuwasilisha maoni ya Kamati yetu hapa mbele ya Baraza lako tukufu moja kwa moja.

KUHUSU MFUMO WA BAJETI WA PBB
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuanzia mwaka wa fedha 2015/2016 imeanzisha mfumo wa bajeti unaozingatia programu yaani Program Based Budget (PBB) ambapo kwa bajeti hii itakuwa ni kipindi cha pili kutekelezwa, licha ya kuwa ilishaanza kutekelezwa kwa mwaka wa fedha uliopita bado mfumo huu unabakia kuwa mpya kwa Wajumbe wako ukizingatia kwamba asilimia kubwa ya Wajumbe wa Baraza hili ni wapya hivyo mfumo huu wa PBB imekuwa ni changamoto kwao kuweza kuufahamu kwa ghafla na kupelekea ugumu kidogo kuweza kumudu kufanya uchanganuzi wa vitabu vya Bajeti vilivyoletwa katika kamati zako, sambamba na hilo Wajumbe hawakupatiwa mafunzo ya kutosha, lakini hata hivyo wamejitahidi kadiri ya uwezo wao kuweza kuchambua bajeti hiyo kwa msaada wa makatibu wetu ambao kwa kweli  tunawashukuru sana.

Mheshimiwa Spika,
Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ina mafungu (vote) mawili ambayo ni A01 na A02 na imepanga kutekeleza Program kuu tano zenye Programu ndogo 14 ambazo kwa ujumla Fedha iliyoombwa kwa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ni TZS. 6,490,200,000 (Bilioni sita, Mia nne tisiini milioni na laki mbili).

Fungu A01 Ofisi ya Rais Ikulu ina jumla ya Programu kuu tatu na programu ndogo  tisa, Programu kuu ni kama zifuatazo:-
1.     Programu ya kusimamia Shughuli za Mheshimiwa Rais na kuimarisha Mawasiliano Ikulu.
2.     Programu ya Ushirikiano wa kikanda, kimataifa na uratibu wa Wazanzibari wanaoishi nchi za Nje (Diaspora).
3.     Programu ya Utawala na Uendeshaji wa Ofisi ya Rais Ikulu.
Program ndogo ni hizi zifuatazo:-
                   I.            Programu ndogo ya uratibu wa shughuli za Mheshimiwa Rais
                 II.            Programu ndogo ya kuimarisha mawasiliano baina ya Mheshimiwa Rais na Wananchi
              III.            Programu ndogo ya kuiwakilisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mikutano ya kikanda na kimataifa
              IV.            Programu ndogo ya uratibu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika masuala ya Diaspora
                V.            Program ndogo ya uratibu na usimamizi wa shughuli za Ofisi ya Rais Ikulu
              VI.            Program ndogo ya uratibu wa shughuli za Mipango, Sera na utafiti za ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
           VII.            Program ndogo  ya Kuratibu na kusimamia shughuli za uratibu na usimamizi wa shughuli za Ofisi ya Rais Ikulu na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Pemba
         VIII.            Programu ndogo ya usimamizi wa usalama wa watumishi wa Umma
              IX.            Programu ndogo ya ufuatiliaji na tathmini ya Sera na Maamuzi ya Serikali

PROGRAMU YA KUSIMAMIA SHUGHULI ZA MHESHIMIWA RAIS NA KUIMARISHA MAWASILIANO IKULU.

Mheshimiwa Spika,
Programu hii ina Jukumu la kusimamia shughuli za Mheshimiwa Rais pamoja na kuimarisha Mawasiliano, programu hii ina programu ndogo mbili ambazo ni programu ndogo ya uratibu wa shughuli za Mheshimiwa Rais ambayo imetengewa shilingi 2,667,003,000 (Bilioni mbili,mia sita sitini na saba Milioni, na elfu tatu) na shughuli zinazotarajiwa kutekelezwa ni pamoja na kufuatilia ahadi na maagizo ya Mheshimiwa Rais, kuratibu ziara za ndani na za nje za Mheshimiwa Rais, kutoa viburudishaji kwa wageni wa Mheshimiwa Rais, kuchapisha hotuba na mambo mengine ya Mheshimiwa Rais, na kutoa zawadi kwa wageni wa Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika,
 Programu ndogo ya pili ni ya kuimarisha mawasiliano baina ya Mheshimiwa Rais na Wananchi ambayo imepangiwa shilingi 200,351,000 (Milioni mia mbili, laki tatu na hamsini na moja elfu) na shughuli zinazotarajiwa kutekelezwa kwa fedha hizo ni pamoja na kutayarisha, kuchapisha na kusambaza Kalenda za Ofisi ya Rais, kutayarisha, kuchapisha na kusambaza Jarida la Ikulu, vipeperushi na machapisho mengine, kuimarisha tovuti ya Idara ya Mawasiliano, Kwa ujumla programu kuu ya kusimamia shughuli za Mheshimiwa Rais imepangiwa kutumia shilingi 2,867,353,000 (Bilioni mbili, mia nane sitini na saba Milioni, laki tatu hamsini na tatu elfu).

Mheshimiwa Spika,
Kamati yetu imeridhika na makadirio yaliopangwa katika programu hii na ilipendekeza mambo mbali mbali ambayo yatakapozingatiwa yataboresha kwa kiasi kikubwa kumtangaza Rais wetu na kumfanya awe karibu zaidi na wananchi wake waliopo hapa nchini lakini pia hata wanaoishi nchi za nje, Kwanza Kamati yangu katika kuona mawasiliano yanaimarika baina ya Rais wetu na wanachi ni vyema Idara ya Mawasiliano, mbali na kusambaza majarida na kalenda, imtangaze Rais kwa kutumia mfumo wa kisasa wa teknolojia na Mawasiliano kwa kutumia njia zinazoendana na dunia ya leo (New Media) kama vile facebook, twitter, youtube mfano clips muhimu za Rais,  shorts clips za sekunde 30 hadi sekunde 45 kwa ajili ya whatsApp, ili watu waone  shughuli anazozifanya Mheshimiwa Rais, pamoja na kutambulika katika ulimwengu mzima na kwa jinsia zote na rika zote.

Mheshimiwa Spika,
Aidha Kamati yetu inashauri kwamba Mheshimiwa Rais angelikuwa na utaratibu wa kuwaalika na kukaa pamoja na wawekezaji, wafanyabiashara na wadau mbali mbali wa maendeleo kwa lengo kuzungumza na badilishana nao mawazo lakini pia kuwashukuru wale ambao wamekuwa wakiisaidia nchi yetu kwa njia moja au nyengine, Jambo hili linaweza kuongeza hamasa kwa wafanyabiashara na wawekezaji kuwekeza zaidi katika sekta mbali mbali. Aidha pale ambapo kunatokezea mgeni mashuhuri ambae atastahiki kupewa zawadi basi zawadi atakayopewa iwe ni zawadi yenye asili na iliyotengenezwa kwa ubunifu na iambatanishwe pamoja na historia ya mtengenezaji, ili kuhakikisha kuwa Mgeni anapopewa zawadi hiyo basi anapata kujua historia ya Zanzibar ambayo wanaweza kuweka kumbukumbu katika makumbusho yao lakini pia itaitangaza nchi katika masuala ya utalii.

PROGRAMU YA USHIRIKIANO WA KIKANDA, KIMATAIFA NA URATIBU WA WAZANZIBARI WANAOISHI NCHI ZA NJE.

Mheshimiwa Spika,
Programu hii ina lengo la kuiwezesha Zanzibar kushiriki katika mikutano ya kikanda na kimataifa, na kuwashirikisha ipasavyo Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi yao. Programu hii ina programu ndogo mbili ambazo ni programu ndogo ya kuiwakilisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mikutano ya kikanda na kimataifa ambayo imepangiwa kutekelezwa kwa shilingi 264,673,000 (Mia mbili sitini na nne Milioini, laki sita na sabini na tatu elfu) ambapo miongoni mwa shughuli zitakazofanywa ni pamoja na kuimarisha ushiriki wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mikutano ya kikanda, kuendesha vikao vya ndani vya kisekta kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kushiriki katika mikutano ya mashauriano ili kupata msimamo mmoja wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kushiriki katika mikutano ya kikanda nje na ndani ya nchi na kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa mtengamano wa Jumuiya za kikanda.

Mheshimiwa Spika,
Programu ndogo ya pili ni ya uratibu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika masuala ya Diaspora, ambayo imepangwa kutekelezwa kwa shilingi 239,847,000 (Mia mbili thelathini na tisa milioni, laki nane na arobaini na saba elfu)  na shughuli zilizopangwa kutekelezwa ni pamoja na kushiriki  katika mkutano wa mashauriano wa Diaspora  na Idara inayoshughulikia masuala ya Diaspora Dar es Salaam, kutoa elimu kwa jamii juu ya dhana ya Diaspora na umuhimu wake,kushiriki mkutano wa wadau wa Maendeleo kujadili ajenda za Diaspora, kuandaa kongamano la Watanzania wanaoishi nchi za nje na kusimamia shughuli za kila siku za Idara ya Ushirikiano wa kimataifa na uratibu wa Diaspora. Kwa ujumla Programu ya Ushirikiano wa Kikanda, Kimataifa na Uratibu wa Wazanzibari wanaoishi Nchi za Nje imekadiriwa kutekelezwa kwa shilingi 504,520,000 (Milioni mia tano na nne, laki tano na ishirini elfu).

Mheshimiwa Spika,
Katika kuona azma ya kuwepo kwa idara ya uratibu wa wazanzibari wanaoishi nchi za nje inazaa matunda, kamati yangu inashauri kwamba wafanyakazi wote wanaokwenda ziara nchi za nje au kushiriki mikutano nchi za nje wawasilishe ripoti za ziara au safari hizo kwa ujumla wake Serikalini ili ripoti hizo zifanyiwe kazi ili kuleta mafanikio kwa taifa letu, sambamba na hilo safari hizo ziweze kuleta tija ya kuibua miradi mbali mbali kutoka kwa wahisani lakini pia, wanapokwenda huko waitangaze vyema nchi yetu ili wawekezaji wavutike kuja kuwekeza katika sekta mbali mbali.

Mheshimiwa Spika,
Kamati yetu katika suala zima la safari za nje wanazokwenda mawaziri na watendaji mbali mbali wa Serikali inataka kusisitiza juu ya ripoti hizo wanazoziwasilisha  Mawaziri husika katika Baraza la Mawaziri ziambatane na ripoti za utekelezaji wake ili tuone tija ya kweli inapatikana kwa nchi yetu, aidha kamati  ilitaka kujua juu ya ziara za Viongozi wakuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaposafiri kwenda safari za nje na kushauri kwamba wakati viongozi hao wanaposafiri ni vyema wakajitayarisha na kuzingatia faida pamoja na fursa watakazozipata ziinufaishe na Zanzibar.

Mheshimiwa Spika,
Aidha kamati iliishauri Serikali kuwa na mashirikiano ya karibu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa katika Wizara ambazo hazihusiani na Muungano lakini zenye sura ya Kimuungano kwa mfano Afya, Elimu, Utalii nk. Kamati pia ilihoji juu ya uhusiano uliopo baina Comoro na Zanzibar hususan katika suala la Kampuni inayoitwa hairu ambayo ni kampuni ya uvuvi iliyokuwa ije kuwekeza Zanzibar katika masuala ya uhifadhi wa Samaki ambapo Kamati ilipatiwa taarifa kwamba mipango inaendelea katika kufanikisha mradi huo.

PROGRAMU YA UTAWALA NA UENDESHAJI WA OFISI YA RAIS IKULU.

Mheshimiwa Spika,
Programu hii ina malengo ya kuimarisha shughuli za mipango, kuandaa na kuchambua sera na utafiti pamoja na kuimarisha uwezo wa kiutendaji na uratibu wa shughuli za Ofisi ya Rais Ikulu, program hii ina program ndogo tano,ambazo ni program ndogo ya uratibu na usimamizi wa shughuli za Ofisi ya Rais Ikulu, ambayo imepangiwa kutekelezwa kwa shilingi 1,126,326000 (Bilioni moja, mia moja ishirini na sita milioni, laki tatu na ishirini na sita elfu) ambazo zinakadiriwa kutumika katika shughuli za  kusimamia uendeshaji wa Ofisi ya Rais Ikulu kwa kulipa mishahara, kununua vifaa vya usafiri, kuboresha na kukarabati vitendea kazi, ofisi na Majengo, kutoa huduma za kiutawala, kutoa mafunzo kwa waajiriwa wapya 12 na nyenginezo kama zinavyoonekana katika kitabu cha makadirio ya Mapato na Matumizi ya cha mwaka 2016/2017.

Mheshimiwa Spika,
Katika program ndogo hii Kamati yangu inashauri kwamba ili jengo la Ikulu ya Mnazi Mmoja liweze kuwa na haiba na mvuto zaidi kwa shughuli za Mheshimiwa Rais, ni vyema lifanyiwe ubunifu katika sehemu yake ya nyuma iliyo mkabala na bahari kwa kujengwa jet ambayo itaingia katika eneo la ufukwe wa bahari uliopo na kusanifiwa katika mtindo wa utamamduni wetu ambao sehemu hiyo ataitumia Rais anapokuwa na wageni wake mashuhuri ili kupata utulivu katika hewa nzuri ya upepo wa bahari ya hindi na kuwafanya wageni  wavutike kuja kuwekeza Zanzibar.

Mheshimiwa Spika,
Program ndogo ya pili ni ya uratibu wa shughuli za Mipango, Sera na utafiti za ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambayo imekadiriwa kutekelezwa kwa TZS 300,778,000 (Milioni mia tatu, laki saba na sabini na nane elfu) zitakazotumika kwa kulipa mishahara kwa wafanyakazi na stahiki nyengine, kutoa mafunzo ya muda mrefu,kusimamia na kuhuisha tovuti ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kufanya tathmini hali ya Tehama katika Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kuandaa na kuratibu vikao vya matayarisho ya hotuba ya Bajeti nk.

Mheshimiwa Spika,
Program ndogo ya tatu ni ya Kuratibu na kusimamia shughuli za uratibu na usimamizi wa shughuli za Ofisi ya Rais Ikulu na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Pemba, program hii imekadiriwa kutumia TZS 663,113,000 (milioni nia sita sitini na tatu, laki moja na kumi na tatu elfu) ambazo zinatarajiwa kutumika kwa kutoa na kuratibu huduma za utawala, kulinda, kuhifadhi na kutoa huduma kwa Ikulu na nyumba za Serikali zilizoko Pemba, kulipa mishahara na stahiki kwa wafanyakazi wa Pemba, kutoa huduma za usafiri, zana na matengenezo yake, kukarabati majengo ya Ofisi na ununuzi wa thamani za Ofisi.

Mheshimiwa Spika,
Kamati yetu kupitia Programu ndogo ya uratibu na usimamizi wa ofisi ya Rais Ikulu na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Pemba inashauri kwamba jengo la Ikulu ya Chake Chake kufanyiwa ukarabati mkubwa kwani haifanani na hadhi ya kuwa nyumba ya kukaa kiongozi mkubwa wa nchi kwani hali yake hairidhishi. vile vile Kamati inapendekeza kuondoshwa kwa maofisa wa Serikali ikiwa ni pamoja na maofisa wa Mahakama wanaokaa katika nyumba iliopo katika eneo la Ikulu,  ili nyumba hiyo iweze kufanyiwa ukarabati. Sambamba na hilo Kamati yangu ilitaka kujua juu ya matengenezo ya nyumba ya Ikulu ya Mkokotoni ambayo nayo inahitaji kujengewa uzio kwa ajili ya kuzuia uingiaji ovyo wa watu katika eneo hilo.  Aidha Kamati inashauri kwamba Wizara hii ikae pamoja na Waziri anaehusika na vikosi ili kukarabati sehemu ambayo askari wa KMKM wanakaa wakati wanapofanya kazi zao za ulinzi, ili iendane na eneo hilo la Ikulu.

Mheshimiwa Spika,
Programu ndogo ya nne ni ya usimamizi wa usalama wa watumishi wa Umma ambayo imekadiriwa kutumia TZS 40,000,000 (Milioni arobaini) ambazo fedha hizo zinatarajiwa kutumika katika usalama wa mali na majengo ya Serikali kwa Unguja na Pemba, kufanya ukaguzi wa kiusalama wa muda mfupi na endelevu kwa wafanyakazi, kuendesha mafunzo na semina kwa watumishi. Kamati inashauri kwamba ili wafanyakazi wafanyekazi katika mazingira yalio salama zaidi ni vyema ukaguzi wa kiusalama wa majengo ukafanyika mara kwa mara kwani kuna taasisi na idara mbali mbali ambazo wanafanya kazi katika majengo ambayo sio salama na hivyo kuhatarisha usalama wa wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika,
Kwa ujumla wake Programu kuu ya Programu ya Utawala na Uendeshaji wa Ofisi ya Rais Ikulu imekadiriwa kutumia TZS 2,126,326,000, (Bilioni mbili mia moja ishirini na sita milioni laki tatu na ishirini na sita elfu) ambazo kamati yangu inaona bado ni fedha chache kutengwa kwa Ofisi kubwa kama hii, hususan ukizingatia uchakavu wa nyumba za Ikulu zinazohitaji kufanyiwa ukarabati ili ziweze kuendana na hadhi ya Rais wetu

Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu pia imepitia Fungu A02 Ofisi ya Baraza la Mapinduzi, ambalo ni fungu linalojitegemea na kusimamiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi, Fungu hili lina program kuu mbili na program ndogo tano, program kuu ni:-
1.     Programu ya usimamizi wa Majukumu ya kikatiba na kisheria ya Baraza la Mapinduzi
2.     Programu ya Utumishi na Utawala wa Ofisi ya Baraza la Mapinduzi,
Kwa upande wa program ndogo ni:-
       I.            Programu ndogo ya Uratibu na Usimamia shughuli za Baraza la Mapinduzi na kamati zake
     II.            Programu ndogo ya tathmini ya uwajibikaji na utendaji kazi wa Taasisi za Umma
  III.            Programu ndogo ya kukuza ufanisi wa kitengo cha Teknologia ya Habari na Mawasiliano
  IV.            Program ndogo ya utumishi na uendeshaji wa Ofisi ya Baraza la Mapinduzi
    V.            Program ndogo ya pili ni uimarishaji uwezo wa Ofisi katika kusimamia Sera, Sheria na Utumishi wa Umma

PROGRAMU YA USIMAMIZI WA MAJUKUMU YA KIKATIBA NA KISHERIA YA BARAZA LA MAPINDUZI NA KAMATI YA MAKATIBU WAKUU

Mheshimiwa Spika,
Programu ya usimamizi wa Majukumu ya kikatiba na kisheria ya Baraza la Mapinduzi na Kamati ya Makatibu Wakuu ambayo kwa ina lengo la kutayarisha na kusimamia vikao vya Baraza la Mapinduzi na Kamati ya Makatibu Wakuu, programu hii ina Programu ndogo tatu, programu ndogo ya kwanza ni ya kuratibu na kusimamia shughuli za Baraza la Mapinduzi na kamati zake ambayo imekadiriwa kutekelezwa kwa TZS 109,200,000 (Milioni mia moja naTisa na laki mbili) ambazo zitatumika katika kutayarisha vikao 12 vya BLM na Kamati zake, kutayarisha vikao 12 vya Kamati za Baraza la Mapinduzi kutayarisha vikao 8 vya dharura vya BLM na 8 vya kamati ya Makatibu Wakuu wa SMZ, kutoa mafunzo ya kujenga uwezo kwa Viongozi wa kisiasa na Sekretarieti ya Baraza la Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika,
Program ndogo ya pili ni ya tathmini ya uwajibikaji na utendaji kazi wa Taasisi za Umma, ambayo imekadiriwa kutekelezwa kwa TZS 35,360,000 (Milioni thelathini na tano laki tatu na sitini elfu) ambazo zitatumika katika shughuli za kutayarisha mikutano miwili ya tathmini ya utendaji kazi kati ya Mheshimiwa Rais na Viongozi wa Wizara za SMZ, kusaidia shughuli za kijamii na masuala mtambuka kupitia Mawaziri wasio na Wizara maalum.

Mheshimiwa Spika,
Program ndogo ya tatu ni ya kukuza ufanisi wa kitengo cha Teknologia ya Habari na Mawasiliano ambayo nayo imepangiwa kutekelezwa kwa TZS 31,930,000 (Milioni thelathini na Moja, laki tisa na thelathini elfu) katika kutekeleza shughuli za kusimamia huduma za mkonga wa Taifa wa Mawasiliano katika Ofisi, Kwa ujumla Programu kuu ya usimamizi wa Majukumu ya kikatiba na kisheria ya Baraza la Mapinduzi na Kamati ya Makatibu Wakuu kwa mwaka wa fedha 2016/2017 imekadiriwa kutumia 176,490,000 (Milioni Mia moja sabini na sita laki nne na tisiini elfu).
PROGRAMU YA UTUMISHI NA UTAWALA WA OFISI YA BARAZA LA MAPINDUZI
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu pia katika Fungu A02 ilipitia Programu kuu ya Utumishi na Utawala wa Ofisi ya Baraza la Mapinduzi yenye lengo la kuimarisha mazingira ya kazi, mahusiano ya umma na kuwaongezea ujuzi wafanyakazi wa Ofisi, Program hii ina program ndogo mbili ambazo ni program ndogo ya utumishi na uendeshaji wa Ofisi ya Baraza la Mapinduzi na program ndogo ya uimarishaji uwezo wa Ofisi katika kusimamia Sera , sheria na Utumishi wa Umma, Programu ndogo ya utumishi na uendeshaji imepangiwa kutekelezwa kwa TZS 1,179,210,000 (Bilioni moja, mia moja sabini na tisa Milioni, laki mbili na elfu kumi) ambazo zimepangwa kutekelezwa katika shughuli mbali mbali, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya Ofisi, majengo pamoja na mazingira yake, kuiwakilisha Ofisi katika mikutano, warsha pamoja na makongamano ya ndani na nje ya nchi, na  kurahisisha ufanisi wa shughuli za kiofisi.

Mheshimiwa Spika,
 Program ndogo ya pili ni uimarishaji uwezo wa Ofisi katika kusimamia Sera, Sheria za Utumishi wa Umma, program hii imepangwa kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha kwa TZS 136,300,000 (Mia moja thelathini na sita milioni na laki tatu) ambazo zimepangwa kutumika katika kuendesha shughuli za uanzishaji wa Maktaba ya Baraza la Mapinduzi, uimarishaji wa kitengo cha uhifadhi wa kumbukumbu za Baraza la Mapinduzi, kutayarisha ripoti ya mwaka ya hali ya utumishi wa umma pamoja na ukusanyaji na ufuatiliaji wa Sera,Sheria na Miongozo ya Baraza la Mapinduzi. Kwa ujumla wake Programu kuu ya Utumishi na Utawala wa Ofisi ya Baraza la Mapinduzi katika mwaka wa fedha 2016/2017 imekadiriwa kutumia TZS 1,315,510,000 (Bilioni moja,mia tatu kumi na tano Milioni, laki tano na elfu kumi).

Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu baada ya kuzipitia Programu zote nilizozitaja hapo kabla imeona fedha hizo ni kidogo kutengwa kwa ofisi kubwa kama hii ambayo ndio muhimili wa Serikali yetu, ambayo  bado ina changamoto nyingi zinazohitaji kufanyiwa kazi zikiwemo zile za ubovu na uchakavu wa majengo ya nyumba za Ikulu, uhaba wa vitendea kazi, uhaba wa usafiri kwa ajili ya Idara mbali mbali. Hivyo Kamati inashauri kwamba hali itakaporuhusa katika Bajeti ya mwaka ujao 2017/2018 watengewe fedha ambazo zitaweza angalau kupunguza changamoto zinazoikabili Wizara hii muhimu hasa ile ya kukarabati nyumba za ikulu ikiwemo nyumba ya Kupumzikia ya Mkokotoni ambayo inahitaji kujengewa uzio na ile ya Chake Chake ambayo iko katika hali isiyoridhisha.

Mheshimiwa Spika,
Mwisho napenda kukushukuru tena kwa kunipa nafasi ya kuwasilisha maoni ya Kamati yangu kwa niaba ya Kamati pamoja na kuwashukuru Wajumbe wa Baraza lako Tukufu kwa kunisikiliza, sasa niwaombe Wajumbe wa Baraza lako waijadili na hatimae  waiunge mkono  bajeti hii ili wamuwezeshe Waziri kufanikisha na kutekeleza yale waliojipangia katika mwaka huu wa Fedha.

Mheshimiwa Spika,
Kwa niaba yangu na kwa niaba ya Kamati ya kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa kitaifa naunga mkono hoja na naomba kuwasilisha.


Mhe. Omar Seif Abeid,
Mwenyekiti,
Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa,
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.