-
|
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
Kitalu Na. 8, Mtaa wa Luthuli
S.L.P 2643, DAR ES SALAAM
Simu: +255 22 2135747/8; 2137125; 2135222
Faksi: +255 22 2111281
B/Pepe: chragg@chragg.go.tz
Tovuti: www.chragg.go.tz
|
Mei 31, 2016
TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
Tamko la THBUB
kukemea wimbi la vitendo vya mauaji vilivyoanza kushamiri nchini
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
(THBUB) imesikitishwa kupokea taarifa za vitendo vya mauaji ya kikatili
vinavyoendelea kutokea katika maeneo mbalimbali nchini, hususani kanda ya Ziwa,
Mkoa wa Pwani, na Dar es Salaam.
Wimbi hili la matukio ya vitendo vya
mauaji na ukatili uliojitokeza kwa kufuatana mwezi Mei 2016 yanavunja haki ya
kuishi ambayo ndio msingi wa haki zote za binadamu kwa ujumla wake.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora
inalaani vikali mauaji haya yote na matendo yote ya kikatili dhidi ya mwanadamu
yanapotokea popote nchini.
Baadhi ya matukio hayo kwa mujibu wa
taarifa zilizoifikia Tume yametokea usiku wa Mei 11, 2016 katika kitongoji cha
Nyigumba, Kijiji cha Sima Wilayani Sengerema, Mwanza, ambako watu watano (5) wa
familia moja waliuwawa kwa kukatwa mapanga; Mei 18 watu watatu (3) pia waliuwawa
kwa kukatwa mapanga wakiwa katika nyumba ya ibada, Msikiti wa Rahman, eneo la
Ibanda relini, mtaa wa Utemini, Kata ya Mkolani,Wilaya ya Nyamagana, Mwanza; Usiku
wa Mei 25, mwanamume mmoja na mkewe waliuwawa kwa kukatwa mapanga kijijini
Manzavi, Wilayani Butiama, Mara.
Aidha, mnamo Mei 22, Mwenyekiti wa Serikali
ya Mtaa wa Bulale, Kata ya Buhongwa, Mwanza, Bwana Alphonce Musanyenzi aliuawa.
Mauaji mengine yametokea Mei 18, Mkoani Pwani, Askari Polisi, Sajenti Ally
Salum Kinyogoli alipouwawa kwa kupigwa risasi na watu wasiofahamika. Mei 23,
jijini Dar es Salaam, eneo la Kiwalani, watu wanne (4) waliuawa kwa kuchomwa
moto wakiwa wamelala ndani ya nyumba yao; Mei 26, Bi. Anathe Msuya aliuawa kwa
kuchinjwa akiwa nyumbani kwake Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Matukio haya ya ukatili yanakiuka haki
ya kuishi iliyoainishwa katika ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977, Sheria za nchi, matamko na mikataba mbalimbali ya haki
za binadamu ya kikanda na kimataifa.
Kufuatia wimbi hili la mauaji
linaloonekana kuendelea nchini, Tume inalaani na kukemea vikali vitendo hivyo vya
kikatili.
Mbali ya ukiukaji mkubwa wa haki ya
msingi ya kuishi, mauaji haya na matukio haya pia ni kinyume na mafundisho ya imani
zetu mbalimbali, hivyo yasifumbiwe macho na kuachwa yaendelee, kwani yanaweza
kuleta mazoea mabaya ya kuona suala la kuuwa ni jambo la kawaida na hivyo
kuhatarisha amani, maisha ya watu na jamii.
Hivyo, Tume inashauri
yafuatayo:
1. Serikali
kupitia Jeshi la Polisi ichukue hatua mahsusi kuhakikisha ulinzi wa wananchi
dhidi ya mauaji na vitendo hivi, kwani jukumu la kwanza la kuhakikisha usalama
wa wananchi ni jukumu la serikali. Jeshi la Polisi lihakikishe watu wote waliohusika
kutekeleza mauaji haya wanakamatwa ili sheria ichukue mkondo wake.
2. Tume
inawataka pia wananchi wahakikishe wanashirikiana na vyombo vya dola kufichua
maovu na kubaini uvunjifu wowote wa sheria na haki za binadamu ndani ya jamii, na
kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuzuia matukio kama haya kujirudia, au
kusaidia upelelezi wa mauaji haya na matendo mengineyo ya uvunjifu wa sheria.
3. Jamii
ijenge utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu.
4. Mamlaka
za Serikali za mitaa katika ngazi zote ziwe na mipango madhubuti ya kuhakikisha
ulinzi na usalama katika maeneo yao.
5. Tume
inatoa rambirambi kwa ndugu, jamaa na wanafamilia waliopoteza wapendwa wao
katika matukio haya na pole kwa majeruhi.
Jukumu la ulinzi na utetezi wa haki za binadamu ni letu
sote!
Imetolewa na:
(SIGNED)
Mhe. Bahame Tom Nyanduga
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA
UTAWALA BORA
Mei 31, 2016
No comments:
Post a Comment