Habari za Punde

TIB Corporate Bank Yatangaza Mikopo Yenye Masharti Nafuu kwa Wakandarasi Wazawa.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa TIB Corporate Bahati Minja (aliyesimama) akitoa ufafanuzi kuhusu huduma zinazotolewa na TIB Corporate Bank wakati wa mkutano wa Wakandarasi unaofanyika Jijini Mwanza

TIB Corporate Bank imesema imekusudia kuwawezesha kifedha wakandarasi wa ndani ili waweze kutekeleza vema majukumu yao ya kikandarasi.

Akizungumza wakati wa mkutano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi nchini (CRB) uliofanyika jijini Mwanza, Mkuu wa Kitengo cha Mauzo ya Mikopo wa Benki ya TIB, Theresia Soka amesema benki yake imekuja na suluhisho la kutatua changamoto za wakandarasi wazawa.

TIB Corporate Bank imemua kurahisisha taratibu zake za kutoa mikopo kwa wakandarasi wa ndani kwa kuwataka kuwasilisha vielelezo tu vinavyomtambulisha kuwa amesajiliwa kisheria ili aweze kupata mkopo.

‘Tumeamua kurahisisha utaratibu wetu wa utoaji mikopo ili kuwawezesha wakandarasi na hivyo kuchangia ukuaji wa maendeleo nchini katika sekta hii muhimu ya ujenzi’ alisema Bi Soka. 

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa TIB Corporate Bahati Minja, alisema benki hiyo inayomilikiwa na Serikali, imeboresha huduma zake za kibenki ili kuwawezesha wakandarasi wazawa.

‘Lengo kubwa la Benki ya TIB Corporate ni kuhakikisha wakandarasi wanawezeshwa kifedha ili wawe na vitendeakazi vya ujezi’ alisema Bi Soka.  

Hata hivyo wakandarasi waliohudhuria mkutano huo ambao miongoni mwao wamefadhiliwa na benki hiyo, waliupongeza uongozi wa Benki ya TIB Corporate kwa kuamua kuwawezesha kwa mikopo ya kikandarasi. 

Wakandarasi hao walisema uwezeshwaji huo wa mikopo nafuu inayotolewa na benki hiyo, itawasaidia kuendesha kampuni zao za ujenzi kwa ufanisi zaidi.

Mkutano huo wawakandarasi wenye kauli mbiu ya ‘Kuwajengea Uwezo Wakandarasi wa Ndani kwa ajili ya Uchumi Endelevu', utafuatiwa na mkutano mwingine utakaofanyika jijini Dar es salaam katika ukumbi wa Daimond Jubilee kuanzia tarehe 26 hadi 27 mwezi huu wa tano.


TIB Corporate Bank imefanya mabadiliko ya kitaasisi ili kuweza kuwa kituo cha huduma zote za kibenki kwa kushughulikia mahitaji ya wawekezaji wa ndani kwa lengo la kusukuma maendeleo ya uchumi wa Taifa

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.