Habari za Punde

Zanzibar Yaadhimisha Siku ya Wakunga Duniani.

Na Mwandishi Wetu. 
Makamo wa Pili wa Raisi wa Zanzibar Balozi Seifu Ali  Iddi  amewataka  Wakunga na Wauguzi  kutoa huduma bora kwa mama wajawazito bila kujali misingi ya Dini,Kabila,Rangi wala itikadi za kisiasa ili kuwajengea imani  na kupenda  kujifungulia hospitali na vituo vya afya.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Waziri wa Kilimo,Maliasili Uvuvi na  Mifugo Hamad Rashid Muhammed amesema wauguzi ni watu muhimu hivyo ni vizuri kutumia taaluma yao kwa kuzingatia misingi ya maadili ya maadili ya kazi hiyo.

Amesema pamoja na Wauguzi kufanyakazi  katika mazingira magumu amewataka  kufanyakazi kwa uzalendo na uadilifu ili kuwanusuru Wanawake kupta matatizo wakati wa kujifungua yakiwemo kupoteza Damu nyingi wakati wa kujifungua na kupata kifafa cha mimba.

Amefafanua kuwa wajawazito wanahitaji kupata Uangalizi wa karibu kabla na wakati wa kujifungua hivyo hakuna budi kwa Wakunga  kuwa  pamoja  nao kupata msaada wao .


Hamad Rashid ameshauri kutokana  na kazi kubwa wanazofanya Wakunga na Wauguzi hakuna budi kuingizwa katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili waweze kuwa na uhakika wa Maisha yao.

 Waziri wa Afya Zanzibar Mahmoud Thabit  Kombo amesema umuhimu wa kazi za Wakunga  zinaonekana na kila mtu na  wanapofanya vizuri  idadi ya vifo vya mama wajawazito na watoto itaendelea kupungua.  

‘’Kazi yenu ni muhimu na  mimi na mh. Hamad Rashid kama musingetekeleza kazi yenu vizuri tusingezaliwa,’’ aliongeza Waziri Mahmoud.

Ameyashukuru mashirika ya kimataifa  yanayosaidia sekta ya Afya wakiwemo WHO, UNICEF na Mashirika mengine  kwa michango yao mikubwa wanayotoa kwani amesema asilimia kubwa ya Mipango ya Bajeti ya Serikali katika Wizara ya Afya inategemea michango kutoka kwao.

Mapema akisoma Risala ya Siku ya Wauguzi Duniani Mwenyekiti wa Baraza la Wauguzi na Wakunga Zanzibar Prof. Amina Abdul-kadir amesema  Zanzibar imefanikiwa kupunguza idadi ya vifo vya mama wajawazito kutoka 285 mwaka 2011 na kufikia vifo 187 mwaka 2014 baada ya akinamama wengi kuwa na mwamko wa kujifungulia katika Hospitali na vituo vya Afya.

Ameongeza kuwa huduma mbali mbali  zimechukuliwa ikiwemo uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi na matiti na kufanya majadiliano juu ya huduma mbali mbali zinazowahusu wakunga na wauguzi.

Aidha amesema kumekuwa na changamoto katika kupata ufanisi mzuri zaidi  ikiwemo uhaba wa wataalamu wa fani ya uuguzi, Uhaba wa Vifaa vya kufanyiakazi, Mishahara midogo na Mazingira magumu ya kufanyia kazi.

Ujumbe wa mwaka huu katika maadhimisho ya siku ya Wakunga Duniani ni Wanawake na Watoto wachanga muhimili wa ukunga kwa pamoja tuepushe vifo vya mama na mtoto. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.