STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 2.07.2016

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amesema kuwa nia na malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kuimarisha sekta ya elimu ni makubwa hivyo kujitokeza kwa wanannchi na taasisi
mbali mbali kuiunga mkono sekta hiyo ili izidi kuimarika ni jambo la faraja.
Dk. Shein aliyasema hayo wakati wa
mazungumzo kati yake na viongozi na Masheikh wa Jumuiya ya Khoja Shia
Ithna-asheir wakiongoza na Rais wa Jumuiya hiyo Mohammed Raza waliofika Ikulu
mjini Zanzibar kumkabizi Rais msaada wa madawadi yaliotolewa na uongozi huo
pamoja na familia ya Rais wa Jumuiya hiyo kwa ajili ya wanafunzi wa Zanzibar.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini na imekuwa ikichukua juhudi
za makusudi katika kuhakikisha sekta ya elimu inaimarika na ndio maana Rais wa
Kwanza wa Zanzibar mara baada ya ukombozi alitangaza elimu bure.
Dk. Shein alisema kuwa katika ukanda wa
Afrika Mashariki na Kati Zanzibar ina historia kubwa ya elimu ya dini na dunia
kwani ndio nchi iliyokuwa ya mwanzo kuwa na elimu ya dini mnamo miaka 1890 na
elimu ya dunia kuanzia mwaka 1905 kwa kuanzisha skuli licha ya kuwa elimu hiyo ya
dunia waliipata watu wachache.
“Tumefarajika sana, tunajiona hatupo peke
yetu tupo na wenzetu katika kulitafutia ufumbuzi suala hili, madawati ni muhimu
kwa ajili ya wanafunzi wetu.....ipo siku Zanzibar itakuwa haina shida ya
madawati” alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alieleza kufarajika
kwake na mwanzo mzuri uliooneshwa na Jumuiya hiyo pamoja na familia ya Mohamed
Raza kwa kutoa mchango wa madawati hayo ambayo yatasaidia katika kuimarisha
sekta ya elimu hapa nchini kwa kuwasaidia wanafunzi kupata vikalio vya uhakika
maskulini.
Mapema Rais wa Jumuiya ya Khoja Shia
Ithna-asheir Zanzibar, Mohammed Raza alimueleza Dk. Shein kuwa Jumuiya yake
imetoa msaada wa madawati 50 na mtoto wake Hassan Mohammed Raza ametoa madawati
50 yenye thamani ya Tsh. milioni 12 kwa ajili ya wanafunzi wa skuli za Zanzibar
huku akiahdi kuwa misaada hiyo itakuwa endelevu.
Katika maelezo yake Raza alisema kuwa
msaada huo una lengo la kuunga mkono azma ya Dk. Shein ya kuhakikisha suala la
upatikanaji wa madawati linapatiwa ufumbuzi hapa nchini hali ambayo ilimpelekea
Rais kuunda Kamati ya Kitaifa ya watu 12 ikiongozwa na Waziri wa Katiba na
Sheria ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi Haroun Ali Suleiman.
Rais huyo wa Jumuiya ya Khoja Shia
Ithna-asheir ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini alisema kuwa Jumuiya
yake itaendelea kutoa misaada katika sekta zote za maendeleo ikiwemo elimu,
afya na nyenginezo huku akiahidi kuwa atahakikisha kwa kushirikiana na Waziri
wa Elimu anachukua juhudi kusafiri hadi nje ya Zanzibar kwa ajili ya kulipatia
ufumbuzi suala hilo.
Nao Masheikh kutoka Jumuiya hiyo
wakiongozwa na Sheikh Maulana Dhishan
Haidar walitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Dk. Shein kwa uongozi wake mahiri
sambamba na juhudi zake za kuendelea kusimamia amani na utulivu hapa Zanzibar.
Viongozi hao walieleza azma yao ya
kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kuendelea
kumuunga mkono Rais Dk. Shein katika kuimarisha sekta mbali mbali hapa nchini.
“Zanzibar imeweza kupata maendeleo...watu
wake wanapendana....amani na utulivu umeimarika kwa kiasi kikubwa haya yote
yanatokana na uongozi bora wa Dk. Shein”,alisema Maulana Haidar.
Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali
Riziki Pembe Juma alitoa pongezi na shukurani kwa Jumuiya na Familia ya
Mohammed Raza kwa kutoa msaada huo wa madawati ambayo yatawasaidia wanafunzi wa
hapa Zanzibar katika kuweza kujipatia elimu bora kwa ufanisi zaidi.
Waziri Pembe alisema kuwa Wizara kwa
upande wake inatoa shukurani kubwa na inathamini mchango huo na kueleza kuwa
kwa vile Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina nia nzuri juu ya jambo hilo
anamatumaini makubwa kuwa mafanikio yatapatikana.
Waziri huyo wa Elimu alitumia fursa hiyo kupongeza
juhudi zinazochukuliwa na Dk. Shein katika kuimarisha sekta mbali mbali za
maendeleo ikiwemo sekta ya elimu na kuwaomba wananchi na taasisi nyengine
kuendelea kutoa michango yao ya vifaa hivyo kwa ajili ya wanafunzi wa Zanzibar.
Hivi karibuni Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar iliwasilisha rasimu ya uchangiaji na upatikanaji wa madawati maskulini
ili kuweza kupunguza upatikanaji wa madawati katika skuli za Zanzibar katika
Baraza la Wawakilishi.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment