Habari za Punde

Meli ya Shirika la Meli Zanzibar MV MAPINDUZI II Yarejea Zanzibar ikitokea Mombasa Kenya.

Na Kijakazi Abdalla Habari Maelezo.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetumia kiasi ya dola 90 elfu kuifanyia matengenezo ya kawaida Meli ya MV Mapinduzi ll iliyopelekwa Chelezoni Mombasa.

Akizungumza na waandishi wa Habari Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji  Mustafa Aboud Jumbe mara baada ya kuwasili Bandarini Malindi amesema itaanza safari zake za kawaida Pemba kuanzia kesho ili kupunguza usumbufu wa usafiri uliojitokeza baada ya kuondoaka meli hiyo. 

Alisema kuwa meli hiyo imefanyiwa matengenezo ya kawaida  na hakuna kitu kilicho badilishwa na baada ya  matengenezo hayo itakuwa  chini ya Mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoka kwa udhamini wa mtengenezaji.

Hata hivyo Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji  amesema hivi sasa Serikali imo katika mchakato wa kununua meli nyengine mbili mpya, moja  kwa ajili ya abiria na mizigo na nyengine itakuwa ya mafuta
 Mapema Nahodha wa Meli hiyo Abdulrahman  Mzee amesema matengenezo ya meli yaliyofanyika yamekwenda sambamba na muda uliopangwa na  yamefanywa kwa hali ya ubora kabisa

Amesema kuwa kufanyika kwa matengenezo ya meli hiyo ni jambo la kawaida kwa chombo chochote cha usafiri jambo linalokipa ubora chombo husika.
Meli ya MV Mapinduzi ll iliondoka Zanzibar  wiki mbili zilizopita kwenda chelezoni  Mombasa na imerejea  Zanzibar leo kupitia  Pemba ikiwa imechukua  abiria 1200 pamoja na mizigo.                                       

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.