Habari za Punde

Mama Mwanamwema Shein: Tushikamane ili tupige hatua kimaendeleo

 
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Pemba                                       9.11.2016
---
MKE wa Rais wa  Zanzibar Mama Mwanamwema Shein ameeleza kuwa ili nchi ipige hatua katika kuimarisha maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ni lazima suala la umoja na mshikamano lipewe kipaumbele.

Mama Mwanamwema Shein aliyasema hayo huko katika ukumbi wa Ikulu ndogo Chake Chake Pemba, wakati alipokuwa na mazungumzo na Wajumbe wa Umoja wa Wake wa Viongozi wa Majimbo kutoka Pemba.

Katika maelezo yake, Mama Shein ambaye ndio mlezi wa Umoja huo, alisema kuwa kuna kila sababu kuzidisha ushirikiano miongoni mwa wajumbe wa Umoja huo ili uweze kufikia lengo lililokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuendelea kuisaidia jamii.

Mama Shein, aliwasisitiza wake hao wa viongozi pamoja na wajumbe wote wa Umoja huo, kuwa ni lazima juhudi za makusudi za kimaendeleo zikachukuliwa katika kipindi hichi ili kuviachia vizazi vijavyo uchumi na maendeleo endelevu.

Nae Mama Asha Balozi, Mke wa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Wajumbe hao umuhimu wa Umoja huo sambamba na malengo na madhumuni yake katika kuisaidia jamii, kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi pamoja na kuileta nchi maendeleo.

Mapema Mama Fatma Karume alieleza haja kwa mashirikiano na maelewano mema kwa wake wa viongozi kwa kutambua kuwa na wao ni sehemu ya viongozi hivyo, hawana budi kushirikiana na jamii  jambo ambalo sio geni katika kwa Zanzibar tokea wakati wa kudai uhuru wake.
Nao Wajumbe hao wa Umoja huo kutoka Pemba waliahidi kuendeleza mashirikiano katika kuhakikisha Zanzibar inapata maendeleo na Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kushika hatamu.

Wajumbe hao walimuhakikishia Mama Shein kuwa wataendelea kumuunga mkono na kushirikiana nae kwa nguvu zao zote ili kuhakikisha umoja huo unaimarika.

Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Maudline Castico aliwaeleza wanajumuiya hao kuwa  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Kohamed Shein itaendelea kuwaunga mkono na kuwasaidia, wazee, vijana, wanawake na watoto katika kutatua changamoto zinazowakabili.

Pamoja na mambo mengineyo Umoja huo wa Wake wa Viongozi ambao pia, huwashirikisha Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Kuteuliwa na wale wa Viti Maalum, uliwachagua viongozi mbali mbali kwa upnde wa Pemba akiwemo Zulfa Mmaka kuwa Naibu Katibu wa Umoja huo, Msaidizi Mshika fedha Tatu Mohammed na Makamo Mwenyekiti Zume Ali Othman.

Mama Shein amerejea leo Unguja kutoka kisiwani Pemba ambapo akiwa kisiwani humo alikutana na Wawakilishi wa Majimbo ya Pemba, viongozi na wajumbe wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) wa Mikoa yote ya Pemba, alikutana na viongozi wa madhehebu ya dini ya Kikristo pamoja na kuchangia ujenzi wa Madrasatul Nuur Juhud iliyopo Micheweni na hatimae kukutana na wake wa Wawakilishi wa Majimbo ya Pemba hapo jana.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.