Habari za Punde

Dk Shein: alifungua soko jipya la matunda Wete


Atamka: wanaokusanya mapato sio yao aahidi kuwashughulikia, sasa basi udokozi
Na Haji Nassor, Pemba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe: dk Ali Mohamed Shein, amewashukia makusanyaji mapato katika mabaraza ya miji na halmashauri nchini, kuwa fedha wanazokusanya sio mali yao, bali ni za serikali na kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Alisema wapo baadhi yao, wamekuwa na mikoba miwili wanapokusanya mapato hayo na kuyagawa kwa kuingiza kwenye mifuko ya makoti na mashati yao, na nyengine ndio huziingiza serikalini.
Dk: Shein alitoa angalizo hilo mjini Wete Mkoa wa kaskazini Pemba, mara baada ya kulifungua soko na ofisi mpya ya baraza la mji wa Wete, ikiwa ni sehemu ya shamra shamra za maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi Zanzibar.
Aliwatahadharisha wakusanya mapato hao kwa kuwambia “mti na macho’ akiwaashiria kuwa suala la kukusanya mapato, hayataki ubabaisha uliokuwa umezoeleka hapo awali.
Dka Shein alieleza kuwa, anazotaarifa rasmi juu ya wakusanya mapato katika mji wa Wete, kuwa wapo baadhi yao ni wababaishaji, na kuwataka sasa waache tabia hiyo mara moja.
Alisema sio vyema mapato wanayoyakusanya kuyaingiza kwenye mifuko yao binafasi, na mengine ndio kuyaingiza kwenye mfuko wa serikali, na sasa hatomvumilia yeyote atakaebainika kuchupa taratibu zilizopo.
“Mnaokusanya mapato kwenye mabaraza ya miji, halimashauri na taasisi nyengine, acheni mtindo wa kuwa na mifuko miwili wakati mnapokusanya mapato, na badala yake, eleweni kuwa fedha hizo hutakiwa kuingizwa serikali pekee’’,alifafanua.
Katika hatua nyengine Rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapidnuzi, alisema tayari serikali, imeshatenga shilingi milioni 600 kwa ajili ya kuwafikisha huduma ya umeme wananchi wa Kisiwa cha Fundo wilaya ya Wete.
Alisema tayari visiwa kadhaa vidogo vidogo vinavyoishi watu, vimeshafikishiwa umeme kikiweo cha Mwambe shamiani, Kisiwa panza na Makoongwe, hivyo aliwata wananchi hao wa kisiwa cha Fundo, kuondoa shaka.
Alifafanua kuwa sasa kilichobakia ni mazungumzo ya mwisho na Shirika la Umeme la Zanzibar ZECO, na anatarajia sana katikati ya mwaka huu, huduma hiyo iwe imeshafika kisiwani humo.
Alisema miongoni mwa azma na malengo ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, ni kuhakikisha wananchi wote wapata huduma za lazima bila ya ubaguzi.
Alisema waasisi wa mapinduzi hayo, walishaamua kuwakomboa wananchi, ambao kwa muda mrefu walikuwa wametawaliwa, na chama cha ASP ndio kilichowakomboa kwa wakati huo.
“Sasa tumeshajitawala wenyewe, hivyo hakuna sababu kwa wananchi wetu wa Fundo wasipate huduma muhimu ya nishati ya umeme kama wenzao’’,alisema.
Hata hivyo rais huyo wa Zanzibar, alisema malengo ya Mapinduzi matukufu, yameshafika vilivyo Mkoa wa kaskazini Pemba, kwa kuwepo miundo mbinu ya barabara za kiwango cha lami kila kijiji.
“Nani engetarajiwa kuwa siku moja mkoa wa kaskazini Pemba, ungeng’ara kwa barabara na huduma nyengine, kama za elimu, lakini haya yamekuja baada ya sisi kjitawala na leo twasherehekea miaka 53 ya Mapinduzi’’,alifafanua.
Katika hatua nyengine rais huyo wa Zanzibar, aliitumia nafasi hiyo, kuwahakikisha wananchi kuwa, wasiwe na wasiwasi wowote, hakuna uchaguzi mwengine hadi mwaka 2020.
Alifafanua kuwa, uchaguzi umeshakamilika na wala hakuna Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa mwenye nguvu na mamlaka wa kuiondoa serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliochaguliwa kihalali.
“Sisi Zanzibar tunakatiba yetu na sheria zetu, Umoja wa mataifa una taratibu zake na sheria zake, sasa hakuna haki wala sheria kwa Umoja wa mataifa kuingilia mambo ya ndani ya nchi yetu’’,alisema.
Akizungumzia kuhusu soko hilo jipya, aliwataka wafanyabiashara, kuomba nafasi zilizopo ili kulitumia kwa kutoa huduma kwa wananchi.
“Nimeelezwa kuwa ndani ya soko hili jipya mna vikuta 78 na milango ya maduka kiasi 36, sasa ombeni nafasi ili mfanyebiashara, muendeshe maisha yenu’’,alifafanua.
Mapema Katibu Mkuu wizara ya fedha na mipango Khamis Mussa Omar, alisema ujenzi wa soko hilo jipya ni mradi maalum, ambo ni fedha za mkopo nafuu kutoka benki ya dunia ‘W.B’.
Alisema mradi huo, upo wilaya zote nne za Pemba na manispaa ya zabnzibar,  kwa ujenzi wa masoko, ukuta, vidaraja vya kupitia wananchi, chinjio na kulifanyia ukatabati mkubwa ofisi ya baraza la mji Mkoani Pemba.
Alisema ujenzi wa soko hilo la Wete, pamoja na ofisi ya baraza la mji Wete, pia umehusisha ujenzi wa maegesho ya gari, ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukua gari 30 za abiria kwa wakati mmoja.

Soko la matunda na mboga mboga la Mjini Wete, limejengwa upya, baada ya lililokuwepo lililojengwa mwaka 1954 kuchakaa, ambapo shilingi billion 1.73 zimetumika ikiwa ni mkopo wa masharti nafuu kutoka benki ya dunia (WB) na sasa pana vyoo 14 vikiwemo vya watu wenye ulemavu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.